Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO yaomba wafanyakazi na wafanyabiashara nchini Uturuki na Syria wasaidiwe

Ajira kwa watoto huko Türkiye na Syria zinaweza kuongezeka kufuatia tetemeko la ardhi la Februari.
© UNICEF
Ajira kwa watoto huko Türkiye na Syria zinaweza kuongezeka kufuatia tetemeko la ardhi la Februari.

ILO yaomba wafanyakazi na wafanyabiashara nchini Uturuki na Syria wasaidiwe

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la ajira ulimwenguni ILO limetoa ripoto inayosema matetemeko ya ardhi yaliyozikumba nchi za Syria na Uturuki mapema mwaka huu yamesababisha biashara nyingi kufungwa na kuharibika kwa kiasi kikubwa na matokeo yake mamia kwa maelfu ya watu katika nchi hizo hawana ajira za kuwapatia kipato ili waweze kujikimu.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert Houngbo amesema ukuzaji wa ajira ndio kitovu cha kufikia mafanikio ya kujibu changamoto zilizoletwa na matetemeko hayo na kwamba watu wataweza kujenga upya maisha yao ikiwa wataweza kujenga upya namna ya kujipatia riziki.

“Ukuzaji wa ajira ni kitovu cha jibu lenye mafanikio na shirikishi kwa janga hili” amesema Houngbo huku akiieleza jumuiya ya kimataifa kuwa kwa pamoja wana deni kwa wale ambao wamepoteza sana katika matetemeko hayo ya ardhi la kuhakikisha kwamba kanuni za haki ya kijamii na kazi yenye heshima zimeingizwa kwa uthabiti katika mchakato wa ufufuaji na ujenzi mpya wa mataifa hayo.

Ripoti hizo mbili zinaeleza kwamba makadirio ya takwimu ni ya awali, ambayo yamejumuisha pamoja maelezo ya ziada kutoka kwenye takwimu za kabla ya tetemeko la ardhi na yanabadilika kulingaana na muda.

Takwimu za Uturuki

Takwimu za awali kutoka Uturuki zinaonyesha tetemeko la ardhi liliwaacha zaidi ya wafanyakazi 658,000 wasiweze kujikimu kimaisha. Serikali inasema kuwa zaidi ya maeneo 150,000 ya kazi hayatumiki kwa sasa.

ILO inakadiria kuwa wafanyakazi hawa walioathiriwa wanakabiliwa na hasara ya wastani ya mapato ya zaidi ya dola za Kimarekani 230 kwa mwezi kila mmoja.

Kwa ujumla, atahri za tetemeko nchini humo zinaweza kupunguza mapato ya wafanyakazi na wakarejea majumbani kwao na pungufu ya karibu dola milioni 150 kwa mwezi katika maeneo yaliyoathiriwa.

Mikoa iliyoathiriwa huko Uturuki ni nyumbani kwa zaidi ya wafanyakazi milioni 4, ambao wengi wao wanafanya kazi katika sekta za kilimo, utengenezaji, biashara au huduma zingine zilizoongezwa thamani ya chini.

Huko Malatya 58.8% ya saa za kazi inakadiriwa kupotea, huku Adıyaman idadi ni 48.1% na Hatay idadi ni zaidi ya 45.2%.

Mbali na upotevu wa ajira, tathmini ya ILO kuhusu Uturuki inaonya kuhusu ongezeko la hatari kwa usalama na afya kazini, pamoja na ajira ya watoto.

Takwimu za Syria

Nchini Syria, ambapo kwa miaka 12 kumekuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo tayari vilikuwa vimeathiri sana uchumi na soko la ajira, tathmini inakuta kwamba wafanyakazi wapatao 170,000 wamepoteza kazi kutokana na matetemeko ya ardhi.

Hali hii imeathiri moja kwa moja karibu kaya 154,000 na zaidi ya watu 725,000.

Takriban biashara ndogo ndogo 35,000, na za kati pia zimeathirika. ‘Ukosefu wa ajira’ huu wa muda umesababisha hasara ya jumla ya mapato ya wafanyakazi sawa na takriban dola za milioni 5.7 kwa mwezi.

Majimbo matano ya Syria yaliyo athiriwa zaidi ni Aleppo, Hama, Idleb, Lattakia na Tartous ambayo yalikuwa makazi ya wastani wa 42.4% ya jumla ya watu nchini humo. Hii ilijumuisha takriban watu milioni 7.1 wenye umri wa kufanya kazi (16 au zaidi), kati yao milioni 2.7 walikuwa kwenye ajira (rasmi na isiyo rasmi). 22.8% ya hawa walikuwa wanawake.

ILO imefanya nini?

Mara tu baada ya matetemeko ya ardhi kutokea, ILO ilishirikiana na watu walioathirika ili kushughulikia mahitaji ya dharura ya wafanyakazi na familia zao.

Nchini Uturuki, ILO inapanga na kutekeleza, kwa ushirikiano wa karibu na mamlaka ya kitaifa, na wadau mbalimbali ili kusaidia soko la ajira na kufufua biashara. Mipango iliyopangwa ni pamoja na mipango ya biashara ya dharura inayotegemea wafanyakazi na kufanya kazi na biashara ili waweze kutoa kazi nzuri na endelevu huku wakidumisha mwendelezo wa biashara.

ILO pia inasaidia mashirika ya biashara na vyama vya wafanyakazi kufanya kazi na kutoa huduma muhimu kwa wanachama wao.

Mipango ya kujitolea itazingatia wafanyakazi wa kilimo wa msimu, wafanyakazi wa watoto na wakimbizi.

Zaidi ya hayo, usaidizi utatolewa kwa washirika wa kijamii ili kuhakikisha kwamba wanaweza kuendelea kushiriki katika ufufuaji na mipango ya ujenzi kama wahusika wakuu wa mazungumzo ya kijamii ya kitaifa.

Nchini Syria, ILO inaboresha mazingira ya usalama na afya kazini kupitia mfululizo wa kampeni za mafunzo kwa wahandisi, pamoja na kazi zinazoendelea zinazohitaji ajira katika vitongoji vilivyoathirika vya Aleppo.

ILO pia inatoa ruzuku kwa wadau wake wa kijamii ili kuwasaidia wafanyakazi na biashara zilizoathirika, pamoja na kuboresha usalama na mazingira ya afya kazini.