Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN itusaidie tupate ukweli na haki kwa kuuawa kwa ndugu zetu – Mkazi Beni, DRC

Mkazi huyu wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC aitwaye Joel Methya Ndeku alipoteza ndugu zake katika mauaji ya mwaka 2018 na hadi leo hafahamu chochote kuhusu wauaji.
UN News/George Musubao
Mkazi huyu wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC aitwaye Joel Methya Ndeku alipoteza ndugu zake katika mauaji ya mwaka 2018 na hadi leo hafahamu chochote kuhusu wauaji.

UN itusaidie tupate ukweli na haki kwa kuuawa kwa ndugu zetu – Mkazi Beni, DRC

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC mashambulizi yanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo kwenye jimbo la Kivu Kaskazini yanasababisha sio tu vifo bali machungu yasiyoisha kwa familia za waliouawa kwa kushindwa kufahamu ukweli wa nini kiliwafika jamaa zao, nani aliwaua, na haki gani imetendeka na sheria dhidi ya waliohusika. 

Hii leo  ikiwa ni siku ya kimataifa ya haki ya kupata ukweli kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na utu kwa waathirika mwandishi wetu nchini DRC, George Musubao amefunga safari hadi kwenye makazi ya mmoja wa waliopoteza jamaa zao na kufahamu hali iko vipi na zaidi ya yote Umoja wa Mataifa unafanya nini. 

Ndugu 4 wa Bwana Ndeku wameuawa na hafahamu ukweli wowote

Miongoni mwa aliokutana nao mjini Beni ni Joel Methya Ndeku. Yeye amepoteza watu wanne wa familia yake akiwemo kaka yake mkubwa. Kisa hiki kilitokea wakati waasi wa ADF waliposhambulia eneo lao mwaka 2018.

Bwana Ndeku anasema, “kuna ndugu yangu mmoja anaitwa Poroto aliuawa hapa Alungupa. Tulikuwa tuko naye sasa akatoka tu Tukasikia tu wamemuua. Sasa hawa waasi wa ADF walituita kwa simu ‘mje mje.’ Tuna huzuni kubwa sana. Mpaka sasa hatujui ukweli kuhusu haya mauaji. Hatujui nani anachinja watu hapa mjini Beni.

Bado anavumilia machungu na hakuwahi kufahamu ukweli kuhusu mazingira ya kifo akisema,

Ombi langu ni kwa UN itusaidie wakamatwe wafikishwe mahakamani

Hivyo anaomba Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi ili wapate kujua ukweli wa mauaji hayo na waliofanya vitendo hivyo wafikishwe mahakamani. 

“Umoja wa Mataifa utusaidie tujue kwanza ukweli nani anachinja watu hapa kwetu Beni. Na zaidi ya kujua ukweli, hawa watu wakamatwe waende mahakamani na waadhibiwe kabisa kwa sababu haiko kawaida watu wachinjwe hivi kama wanyama, wanakata shingo. Naomba hawa watu wajulikane na wafikishwe mahakamani,” amesema Bwana Ndeku

MONUSCO inafanya nini?

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO moja ya jukumu lake ni ulinzi wa raia na pia hushirikiana na Ofisi ya pamoja ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu. Jean-Tobi Okala ni Mkuu wa Kitengo cha Habari kwa Umma anasema wanaunga mkono serikali ya DRC katika kufuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu.   

Yeye anasema “ndani ya MONUSCO tuna ofisi inayoitwa ofisi ya pamoja ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu na katika suala la mamlaka yake katika mapambano dhidi ya utovu wa nidhamu . Hii  inaunga mkono serikali ya Kongo, hasa taasisi za mahakama, kwa njia kadhaa.  mojawapo ya njia hizo ni ile inayoitwa ufuatiliaji wa ukiukwaji wa haki za binadamu na kesi zote zilizoandikwa. Ni  kutokana na kesi hizi ambazo tunashirikiana na serikali, na viongozi wa Kongo  kwa misingi ya ushahidi huu, ya kesi hizi zilizorekodiwa ambazo tunasaka haki, iwe ya kiraia au ya kijeshi, kwa kuanzisha uchunguzi na kesi.” 

Na kisha anatoa wito kwa waathiriwa wa vitendo vya ukatili. Anasema washiriki katika majaribio ili kufahamu ni kwa jinsi gani haki inatendeka.

Jean-Tobi Okala - Mkuu wa kitengo cha Habari kwa Umma, MONUSCO .
MONUSCO/George Musubao
Jean-Tobi Okala - Mkuu wa kitengo cha Habari kwa Umma, MONUSCO .

Bwana Okala anasematunawahimiza waathiriwa wa vitendo vya uaktili na ukiukwaji wa haki za binadamu kushiriki katika kesi hizi, ni muhimu sana waone jinsi haki inavyotendeka.  na hapa kinachopaswa kukumbukwa ni kwamba utaratibu wa kuficha na wakati mwingine upotoshaji wa sauti unawekwa ili kuwahakikishia waathirika na mashahidi ulinzi wa kutosha dhidi ya vitisho vinavyoweza kutokea. 

Siku hii inaadhimishwa wakati taratibu za pamoja za ulipaji fidia manusura na waathirika wa vitendo vya ukatili mkubwa kwa waathirika na manusura zimeanzishwa na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa katika matukio kadhaa.  

 

Taarifa hii imendaliwa na GEORGE MUSUBAO wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Beni, DRC