Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndio inawezekana kutokomeza kabisa TB kwa kuongeza juhudi dhidi ya ugonjwa huo

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nembo ya kutokomeza Kifua Kikuu ikiwa imewekwa.
UN News/Daniel Dickinson
Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nembo ya kutokomeza Kifua Kikuu ikiwa imewekwa.

Ndio inawezekana kutokomeza kabisa TB kwa kuongeza juhudi dhidi ya ugonjwa huo

Afya

Leo ni siku ya kifua kikuu duniani maudhui yakiwa “ndio inawezekana kuitokomeza TB.” Takwimu za shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2000 watu milioni 74 wamesalimika baada ya Kupona kifua kikuu na ni kwasababu ya harakati za ulimwengu za kupambana na ugonjwa huo hatari. Kifua kikuu husababishwa na bakteria wanaosambaa kupitia kukohoa, kucheua, kuimba na hata kucheka. Kifua kikuu ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria. Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi ambacho kinaweza kutoka na damu, kupungua uzito wa mwili, joto mwilini hasa wakati wa usiku na maumivu ya viungo.

Kulingana na WHO, watu milioni 10 waliambukizwa kifua kikuu mwaka 2021. Geoffrey Murage aliugua kifua kikuu mwaka 2015 na ishara za kikohozi kisichokwisha pamoja na kuishiwa nguvu ndivyo vilivyomsukuma kusaka vipimo.Murage anasema, "nilianza kukohoa na kusikia mwili uko na uchovu.Nilifikiria kwenda kwa madaktari kuangaliwa na nikapimwa magonjwa tofauti tofauti ndipo wakaiona TB.Baada ya hapo ndio nikapewa dawa za wiki moja na kuagizwa kwenda kwenye hospitali iliyokuwa karibu ya Kayole kuchukua nyengine.Nilipewa maagizo ya kumeza dawa na nikichelewa itabidi nirudie kwahiyo nilitii.Nilikuwa napewa za mwezi mmoja kisha narejea kuongezea hadi ikatimia miezi sita.” anasimulia.

Janga la covid 19 lilimulika matatizo yanayowakabili wakaazi wa mataifa masikini ukizingatia mifumo ya afya na utoaji huduma.Wagonjwa wa kifua kikuu ni baadhi ya wanaohitaji huduma mujarab za afya na matibabu kwani vikwazo ni vingi.Kwa Kenya, dawa za kifua kikuu hutolewa bure kwenye hospitali za umma. Hilo lilimuwezesha Geoffrey Murage kujipa moyo kwenye safari ya matibabu.Tathmini imebaini kuwa kifua kikuu kinawaathiri zaidi wanaume ikilinganishwa na wanawake kwani mienendo na tabia ina mchango mkubwa kwani, "kuepuka TB kitu cha kwanza ni usafi. Cha pili mambo ya kuombana sigara na pombe ni muhimu kuachana na hayo kwani mimi nahisi huko ndiko nilikookota TB.Hii ni kwasababu hivyo vikombe wanavyotumia havioshwi vizuri na vinatumiwa na kila mtu,”  anafafanua.

Mada kuu ya siku ya Kifua kikuu mwaka huu ni Ndio! Tunaweza kuitokomeza TB!.Dhamira ya siku hii ni kuwatia imani viongozi na kuwatia shime kuimarisha uwekezaji kwenye sekta ya afya kwenye vita dhidi ya Kifua Kikuu. Geoffrey Murage ana imani TB inaweza kutokomezwa kwani yeye ni mfano mzuri.Kwa mtazamo wake, "TB ni kama homa ukitii.Ukitii mawaidha ya daktari utapona kwani ni kama homa. Ukikosa kutii utakufa tu.Ukinywa dawa mara kadhaa mwili unazowea. Ni lazima unywe hizo dawa. Ukiacha kuzitumia utaumia.Maisha sio ya daktari, ni yako tu.”  anasisitiza.

Mwaka wa 2023 una umuhimu mkubwa katika vita dhidi ya Kifua Kikuu na Umoja wa Mataifa uko mstari wa mbele kwenye harakati hizo. Kongamano la pili la Kifua kikuu la ngazi ya juu limepangwa kufanyika tarehe 22 mwezi wa Septemba mwaka huu. Ajenda kuu ni manufaa ya sayansi, teknolojia na uwekezaji kupambana na TB. Takwimu za shirika la Afya la Umoja wa Mataifa,WHO, zinaashiria kuwa Kenya ni moja ya mataifa 22 yanayochangia 80% ya wagonjwa wa Kifua kikuu ulimwenguni.Kwa mantiki hii, Kenya ni ya 15 katika orodha hiyo ya mataifa 22 yanayozongwa naTB.

TM, UN News Nairobi (Thelma Mwadzaya)