Bidhaa rafiki kwa mazingira ziliinua uchumi wa dunia 2022- UNCTAD

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Biashara, UNCTAD imetoa ripoti yake hii leo kuhusu mwelekeo wa biashara ulimwenguni kwa mwaka 2022 ikitaja mambo chanya na hasi.
Ripoti hiyo imetolewa jijini Geneva, Uswisi ambapo inasema licha ya mivutano ya kijiografia na kisiasa duniani, mienendo ya biashara duniani ilikuwa na mnepo hadi thamani ya biashara ilivunja rekodi na kufikia dola trilioni 32.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo biashara iliyoweka chachu zaidi kwenye ukuaji wa biashara ni bidhaa rafiki kwa mazingira ambazo kwa mwaka mzima mwelekeo ulikuwa juu.
Bidhaa hizo ni pamoja na magari yanayotumia nishati safi pamoja na umeme, bila kusahau mapangaboi ya kuzalisha umeme kwa njia ya upepo.
“Thamani ya jumla ya bidhaa hizo ilifikia dola trilioni 1.9 mwaka 2022 ikiwa ni nyongeza ya dola bilioni 100 ikilinganishwa na mwaka 2021,” imesema ripoti hiyo ya UNCTAD huku ikisema matarajio ni kwamba mwelekeo utakuwa juu zaidi kwa kuwa nchi nyingi zinajielekeza kwenye kuzalisha bidhaa zisizochafua mazingira.
UNCTAD inasema kupitia taarifa yake kuwa “habari hizo ni njema kwa kuwa bidhaa hizo ni nyenzo muhimu katika kuchochea uchumi usioharibu mazingira au uchumi wa kijani.”
Hata hivyo UNCTAD inasema mwenendo wa biashara ulibadilika na kuwa hasi katika robo ya mwisho wa mwaka ambayo ni kuanzia mwezi Septemba hasa kwa nchi zinazoendelea kwani kiwango cha biashara kiliporomoka.
Ripoti inataja sababu kuwa ni pamoja na ongezeko la bei za vyakula, nishati bila kusahau kuzidiwa madeni.
Makadirio ya UNCTAD ni kwamba hata robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2023 yaani Januari hadi Aprili, biashara itaendelea kuwa dhaifu, lakini kuna nuru nusu ya pili ya mwaka.