Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfungo wa Ramadhani ukianza Guterres atoa wito wa kujenga dunia yenye haki zaidi

Waleed Al-Ahdal anaishi kambi ya wakimbizi wa ndani ya Aljufainah nchini Yemen. Pichani anaandaa futari kwa ajili yake na watoto wake.
© UNICEF/ Oais Al-hamdani
Waleed Al-Ahdal anaishi kambi ya wakimbizi wa ndani ya Aljufainah nchini Yemen. Pichani anaandaa futari kwa ajili yake na watoto wake.

Mfungo wa Ramadhani ukianza Guterres atoa wito wa kujenga dunia yenye haki zaidi

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma salamu kwa Waislamu kote duniani akiwatakia kila la heri kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika ujumbe maalum kwa ajili yam fungo huo, Bwana Guterres amesisitiza kwamba Ramadhani ni mwezi wa "kutafakari na kujifunza na unawakilisha wakati wa kusanyika katika ulimwengu wa roho ya uelewa na huruma, iliyofungwa na vifungo vya ubinadamu wetu wa pamoja."

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa, ujumbe wa Umoja wa Mataifa pia unalenga kukuza majadiliano umoja na amani.

Ameongeza kuwa “Katika nyakati hizi ngumu, moyo wangu unajaa hisia za huruma na sala kwa ajili ya wale wanaopatwa na janga la migogoro, kulazimika kukimbia makwao na maumivu.  Naongeza sauti yangu kwa wale wote wanaoadhimisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, nikitoa wito wa amani, kuheshimiana na mshikamano.”

Bwana Guterres ametoa wito wa msukumo kutoka kwenye maadili ya mwezi huu uliobarikiwa ili kujenga ulimwengu wa haki na usawa kwa wote.

Mapema mwezi huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitisha mkutano wa ngazi ya juu kuadhimisha kwa mara ya kwanza siku ya kimataifa ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu.

Chuki dhidi ya Uislam ni sumu

Kwakati wa maadhimisho hayo Guterres alisema kwenye ujumbe wake kwamba chuki dhidi ya Uislam ni sumu.

Amesema “Waislamu duniani ambao ni takriban bilioni mbili ni kielelezo cha ubinadamu katika utofauti wao na kubainisha kwamba wanatoka kila kona ya dunia, lakini mara nyingi wanakabiliwa na hali ya kutovumiliana na chuki bila ya sababu nyingine isipokuwa imani yao.”

Bwana Guterres ameongeza kuwa ujumbe wa amani, huruma na kuvumiliana  ulioletwa na Uislamu, zaidi ya miaka 1,400 iliyopita, ni hamasa kwa watu duniani kote.

Amebainisha kuwa neno lenyewe Uislamu limetokana na mzizi mmoja wa neno amani.

Alisema alishuhudia mwenyewe, alipokuwa kamishna mkuu wa wakimbizi, ukarimu wa nchi za Kiislamu ambazo zilifungua milango kwa wale waliolazimika kukimbia makazi yao, wakati ambapo nchi nyingi zilifunga mipaka yao.

Ameendelea kusema kuwa ukarimu huo ni dhihirisho la zama hizi za yale yaliyotajwa ndani ya Qur’ani Tukufu katika Surat Al-Tawbah: “Na yeyote katika washirikina akikuomba hifadhi, mpe ulinzi ili asikie neno la Mwenyezi Mungu. Kisha akamjulisha usalama wake, kwa sababu wao ni watu wasiojua.”

Ulinzi haubagui wala kuchagua

Katibu Mkuu amesema kuwa ulinzi huu umehakikishwa kwa waumini na wasioamini, na ni kielelezo cha kuvutia cha kanuni ya ulinzi wa wakimbizi, karne nyingi kabla ya kupitishwa kwa mkataba wa wakimbizi wa 1951.

Katibu Mkuu pia amegusia Tamko la "Udugu  kwa  binadamu kuishi kwa amani duniani" ambalo lilitolewa na Mtakatifu Papa Francis na mwadhama wake, Imamu mkuu Ahmed Al-Tayyib, Sheikh mkuu wa Al-Azhar na kusema kwamba ni kielelezo cha huruma na mshikamano wa kibinadamu.

Amesema, "Dini na mila zote kuu zinatangaza sharti la uvumilivu, heshima na uelewa. Kimsingi tunazungumza juu ya maadili ya ulimwengu wote, maadili haya ndio nguzo ya mkataba wa Umoja wa Mataifa, na ndio kiini cha harakati zetu za kutafuta haki, haki za binadamu na amani."

Bwana Guterres ametoa wito wa kuendelea kujitahidi kutekeleza maadili haya, kulinda utakatifu na utu unaohakikishwa kwa kila maisha ya binadamu, na kushughulikia nguvu za migawanyiko kwa kuthibitisha ubinadamu wa pamoja.