Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani watu bilioni 2.4 hawatakuwa na maji mijini ifikapo mwaka 2050: UN

Mvulana akikusanya maji kutoka kwenye bonde la ukamataji lililokarabatiwa katika jimbo la kusini mwa Sudan la White Nile.
UNEP/Lisa Murray
Mvulana akikusanya maji kutoka kwenye bonde la ukamataji lililokarabatiwa katika jimbo la kusini mwa Sudan la White Nile.

Takribani watu bilioni 2.4 hawatakuwa na maji mijini ifikapo mwaka 2050: UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa maji wa Umoja wa Mataifa unaanza leo  ukibeba maudhui “kushikamana kwa ajili ya maji kwa wote” ikiwa pia ni siku ya maji duniani  na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti sasa ili kuhakikisa rasilimali hiyo adhimu inalindwa, kudhibitiwa ipasavyo na kupatikana kwa kila mtu.

Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema maji ni kama damu ya Maisha ya dunia, kwani kuanzia katika suala la afya na lishe, hadi elimu na miundombinu maji ni muhimu katika kila nyanja ya mwanadamu kuishi na ustawi wake lakini pia yanachangia pakubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kushamiri kwa kila taifa.

Pamoja na umuhimu wake wote huo amesema lakini “Tone kwa tone rasilimali hii muhimu inaharibiwa na uchaguzi wa mazingira na kukaushwa kwa kutumiwa kupita kiasi, huku mahitaji yam aji yakitarajiwa kupita uwezo wa rasilimali hiyo kwa asilimia 40 ifikapo mwisho wa muongo huu.”

Wakati huo huo, Katibu Mkuu amesema mabadiliko ya tabianchi yanaharibu mzunguko wa asili wa maji.

Uchafuzi wa gesi ya viwandani unaendelea kuongezeka hadi viwango vya kuvunja rekodi ya wakati wote ule , ongezeko la joto duniani likifurutu ada  kwa viwango vya hatari.

“Hii inazidisha majanga yanayohusiana na maji, milipuko ya magonjwa, uhaba wa maji na ukame, huku ikisababisha uharibifu wa miundombinu, uzalishaji wa chakula, na minyororo ya usambazaji.”

Guterres ameongeza kuwa kati ya kila watu 100 duniani, 25 huchota maji yao yote kutoka kwenye vijito vya wazi na madimbwi au hulipa bei ya juu kununua maji yenye usalama wa kutiliwa shaka. Watu 22 kujisaidia nje au kutumia vyoo vichafu, vilivyo hatari au vilivyobomoka. Na 44 wanaona maji yao machafu yakitiririka kurudi kwenye vyavyo vya maji vya asili bila kutibiwa, na kusababisha matokeo mabaya ya kiafya na kimazingira.”

Umoja wa Mataifa unasema “watu wanaoishi mijini wanaotarajiwa kuwa kwenye mgogoro wa kukosa maji itaongezeka mara mbili kutoka watu milioni 930 mwaka 2016 hadi kufikia watu kati ya bilioni 1.7 na bilioni 2.4 mwaka 2050.”

Kwa kifipu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema “Dunia yetu inakwenda kombo  katika kufikia lengo letu la maji yanayodhibitiwa kwa usalama na usafi wa mazingira kwa wote ifikapo 2030 na hii ni hatari sana.”

Amesisitiza kuwa hakuna mud awa kupoteza akimtaka kila mmoja kuchukua hatua Madhubuti ili kuleta mabadiliko mwaka huu na kuwekeza katika brasilimali hii ambayo uhai wa waytu na dunia unaitegemea.

Amehitimisha kwa kusema kwamba “Maudhui ya siku ya maji mwaka huu yanatukumbusha gharama ya kushindwa huku kuchukua hatua kwa mabilioni ya watu ambao wanakosa maji safi na salama.”