Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuboresha upatikanaji wa nishati ni muhimu ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu barani Afrika- UNCTAD

WFP na serikali ya Madagascar zaungana mikono kubadilisha jamii za vijijini kusini mwa Madagascar.
© WFP Madagascar
WFP na serikali ya Madagascar zaungana mikono kubadilisha jamii za vijijini kusini mwa Madagascar.

Kuboresha upatikanaji wa nishati ni muhimu ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu barani Afrika- UNCTAD

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Biashara na Maendeleo, UNCTAD inazitaka nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kutumia akiba yao kubwa ya nishati mbadala na kukusanya rasilimali kupitia ushirikiano wa kikanda ili kuunda mustakabali safi na usio na madhara kwa mazingira.

Taarifa iliyotolewa Geneva, Uswisi hii leo na UNCTAD inasema ingawa upatikanaji wa nishati umeongezeka katika nchi za Afŕika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara katika miaka ya hivi karibuni, bado kiwango ni kidogo kwani zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wa eneo hilo bado hawana umeme.

Upatikanaji huu mdogo wa nishati una madhara  kwa afya, elimu, kupunguza umaskini na maendeleo endelevu, inasema ripoti ya UNCTAD iliyopatiwa jina "Bidhaa kwa mtazamo: Suala maalum kuhusu upatikanaji wa nishati katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara", iliyochapishwa tarehe 21 Machi.

Kwa mfano, ukosefu wa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na teknolojia ni jambo linalosumbua sana, hasa wanawake na wasichana, ambao wameathiriwa kupita kiasi na uchafuzi wa hewa kwenye kaya, ambao ulisababisha vifo 700,000 barani Afrika mnamo mwaka 2019.

Ripoti hiyo inaonya kwamba bila juhudi za ziada, idadi ya watu katika eneo hilo wasio na mafuta safi inaweza kuongezeka kutoka watu milioni 923 mnamo 2020 hadi zaidi ya watu bilioni 1.1 mnamo 2030.

"Usambazaji wa nishati ya kutegemewa na bora ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi yoyote," ripoti hiyo inasema. "Unawezesha ukuaji wa viwanda, unakuza uzalishaji na ukuaji wa uchumi, unawezesha maendeleo ya binadamu, na ni muhimu kwa kufikia karibu Malengo yote ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs)."

UNCTAD inatoa wito kwa serikali za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kuharakisha juhudi zao za kupanua upatikanaji wa nishati ili kuepuka kutotimiza SDG 7. Lengo hilo linahitaji nchi kuhakikisha upatikanaji wa huduma za nishati nafuu, za kutegemewa na za kisasa ifikapo mwaka 2030.

Viwango vya chini vya upatikanaji wa umeme

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, upatikanaji wa nishati ya umeme katika Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahara ni wa chini zaidi kuliko katika ukanda wowote wa dunia. Hii ni kutokana na kukosekana kwa gridi zinazosambaza umeme kwa watumiaji. Na pale ambapo gridi zipo, zimepitwa na wakati na hazina miunganisho ya wateja.

Pia, ukosefu wa uwezo wa kutosha wa kuzalisha, usambazaji duni kwa watumiaji, ada kubwa za kuunganisha, mtiririko wa mapato usiotabirika na ushuru wa juu huwakatisha tamaa watumiaji kutumia huduma za kisasa za nishati.

Mahitaji ya chini pamoja na mitambo inayozeeka na ufadhili usiotosha kwa miundombinu huwakatisha tamaa wasambazaji kuvumbua na kusambaza nishati safi.

Mwanamke akiwa kwenye mtambo wa nishati ya sola nchini Mauritius
© UNDP/Stephane Bellerose
Mwanamke akiwa kwenye mtambo wa nishati ya sola nchini Mauritius

Mwelekeo katika siku zijazo safi na za kijani

Ripoti hiyo inasema Afrika inaweza kujenga mustakabali safi na wa kijani kwa kuongeza upatikanaji wa nishati safi kupitia masuluhisho endelevu na bora kwa mazingira ili kuhakikisha kanda hiyo haiachwi nyuma wakati dunia inaelekea kwenye nishati isiyotoa hewa chafu.

Hili linaweza kupunguza madhara ya kiafya yanayohusiana na matumizi ya nishati chafu, kuanzisha nishati bora katika mchanganyiko wa nishati na kujenga sekta ya nishati inayostahimili hali ya tabianchi.

Kutumia akiba kubwa ya vyanzo vya nishati mbadala katika bara kunaweza kusaidia kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme katika kanda na kusaidia mpito kwa vyanzo vya nishati vya kaboni kidogo au sifuri.

Kwa mfano, kwa kuwa Afrika ina asilimia 60 ya rasilimali bora zaidi za jua duniani, inaweza kutumia mitambo inayoendeshwa na jua kama njia ya gharama nafuu ya kutoa umeme kwa mamilioni ya watu ambao hawana umeme.

Afrika pia inaweza kuzalisha takriban tani milioni 50 za gesi ya kaboni ya chini kutoka kwa mabaki ya kilimo, samadi ya wanyama na taka ngumu za manispaa kupitia vichochezi vya kaya, ripoti hiyo inasema.

Kuzalisha gesi ya kibayolojia kupitia vichochezi vya ndani pia kunaweza kutoa nishati ya kaboni ya chini inayozalishwa nchini kwa mamilioni ya kaya katika eneo hili.

Jinsi ya kufungua nguvu ya soko la kikanda

Ripoti hiyo inataka kuunganishwa kwa rasilimali za kikanda na gridi za kitaifa ili kufungua uwezo wa soko la kawi barani Afrika. Soko kama hilo linaweza kutoa nishati ya kutegemewa huku likipunguza gharama ya umeme kwa watumiaji.

Kwa kuunganisha uwezo wa uzalishaji wa vyanzo vya nishati mbadala kuvuka mipaka, nchi zinaweza kuimarisha kutegemewa kwa vifaa vyake vya umeme na kuboresha ufikiaji wa umeme, kwani mataifa yenye nishati ya ziada yanaweza kubadilishana kawi na yale yanayokumbwa na upungufu.

Serikali zinahitaji kuchunguza upya mahitaji yao ya uwekezaji wa nishati na kuyashughulikia kupitia vyanzo vya ndani na kimataifa vya ufadhili.

Ripoti hiyo inasema kutoa ruzuku zinazolengwa katika uzalishaji wa mafuta na kawi ili kupata umeme safi kunaweza kusaidia kuzalisha nishati safi. Nchi zinapaswa pia kuchunguza chaguzi mbalimbali za ufadhili ili kutumia rasilimali za nishati mbadala.