Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msako dhidi ya watetezi wa haki Burundi watia hofu UN

Marta Hurtado, Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu
UN /Elma Okic
Marta Hurtado, Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu

Msako dhidi ya watetezi wa haki Burundi watia hofu UN

Haki za binadamu

Ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa hii leo imesema ina hofu kubwa juu ya ongezeko la msako dhidi ya watetezi wa haki nchini Burundi kufuatia kuswekwa korokoroni hivi karibuni kwa watetezi watano wa haki za binadamu na kufungwa jele kwa mwandishi wa Habari. 

Msemaji wa ofisi hiyo Martha Hurtado akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva, Uswisi hii leo ametaja watetezi hao walioko rumande kuwa ni Sonia Ndikumasabo, Marie Emerusabe, Audace Havyarimana, Sylvana Inamahoro na Prosper Runyange  ambao walikamatwa tarehe 14 mwezi uliopita kutokana na kazi yao.

Mahakama ya Rufaa tarehe 15 mwezi huu ilikazia hukumu ya Mahakama Kuu ya watetezi hao kuendelea kusalia rumande wakisubiri kesi yao. 

Mashtaka dhidi ya watano hao ni yapi?

Kwa mujibu wa Bi. Hurtado, mashtaka dhidi ya watano hao ni uasi, kudhoofisha usalama wa ndani ya nchi halikadhalika utendaji kazi wa sekta ya fedha ya umma.

“Mashtaka hayo yanaonekana kuhusishwa moja kwa moja na uhusiano wao na shirika la kimataifa la haki za binadamu, ‘Avocats sans Frontières’ au watetezi bila mipaka,” amesema Bi. Hurtado.

Amefafanua kuwa kufanya kazi na shirika lisilo la kiserikali hata kama halijasajiliwa nchini Burundi, sio na haipaswi kukatazwa chini ya sheria ya Burundi.

Wanahabari nao hali zao mashakani

Ameongeza kuwa msako dhidi ya mashirika ya kiraia unafanyika huku wakishuhudia pia mashambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari Burundi.

“Mfano ni kisa cha Floriane Irangabiye, mwanahabari ambaye aliswekwa gerezani kwa zaidi ya miezi 6 kwa sababu ya kufanya kazi yake,” ametolea mfano msemaji huyo wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa akiongeza kuwa Floriane alikamatwa mwezi Agosti mwaka jana akiwa ziarani nchini Rwanda kuhusu mahoaji ya redio aliyofanya na warundi wawili waoishi nje ya nchi. Watu hao ni mwanahabari mwenzake na mtetezi wa haki za binadamu.

Tarehe 2 mwezi Januari mwaka huu alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na faini ya dola 500 kwa madai ya kudhoofisha eneo la mamlaka ya nchi.

Msemaji huyo amekumbusha kuwa ukandamizaji wa mashirika ya kiraia kwa misingi kinyume na wajibu wa kitaifa wa Burundi umekuwa unashamiri tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hali ambayo imesababisha watetezi wa haki za binadamu na wanahabari kukimbilia ughaibuni.

“Tunasihi serikali ya Burundi izingatie kwa kina viwango vya haki za binadamu hususan kujielezea, kukusanyika na kuachia huru wote wale wote walioko ndani na mashtaka dhidi yao yafutwe,” amesema Bi. Hurtado.