Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi wa rangi ni kama gari, kila mwaka muundo hubadili- UN

Umoja wa Mataifa umeazimia kung'oa mizizi yote ya ubaguzi wa rangi na kuheshimu haki za binadamu na utu wa kila mtu kokote aliko.
Unsplash/Jay Chen
Umoja wa Mataifa umeazimia kung'oa mizizi yote ya ubaguzi wa rangi na kuheshimu haki za binadamu na utu wa kila mtu kokote aliko.

Ubaguzi wa rangi ni kama gari, kila mwaka muundo hubadili- UN

Haki za binadamu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi wa rangi, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kila mtu aazimie kutokomeza ubaguzi huu ambao unaendelea kuathiri kila nchi dunia

Katika ujumbe wake Guterres amesema ubaguzi wa rangi unaomomonyoa na kukiuka haki za binadamu na utu wa binadamu ni moja ya shinikizo linalogawanya jamii, linasababisha vifo na machungu kwa kiwango kikubwa katika historia.

“Leo hii, ubaguzi wa rangi na mchango wa ukoloni na utumwa vinaendelea kuharibu maisha na kufuta fursa huku vikizuia mabilioni ya watu kufurahia uhuru na haki zao za binadamu,: amesema Katibu Mkuu.

Amesema ubaguzi wa rangi si kitu mtu anazaliwa nacho bali anajifunza katika makuzi yake na pindi anapojifunza kinaweza kuwa na nguvu kubwa haribifu isiyozuilika.

Hali inakuwa mbaya serikali na mamlaka zikitumia ubaguzi wa rangi

Katibu Mkuu amesema pindi serikali na mamlaka wanapotumia ubaguzi wa rangi kwa manufaa ya kisiasa, wanachochea mvutano na kuchangai katika mazingira ambayo yanaweza kugeuka kuwa ghasia, ikiwemo uhalifu na ukatili.

Chuki dhidi ya wageni, misimamo ya kibaguzi, kauli za chuki na aina nyingine za ubaguzi vinashamiri kila mahali, amesema Katibu Mkuu.

“Viongozi wa kisiasa wanalenga makundi madogo na wahamiaji. Wenye ushawishi katika mitandao ya kijamii wanajifaisha kwa fedha kupitia ubaguzi wa rangi. Akili bandia nayo inatengeneza jukwaa la kiditali lenye ubaguzi,”  amefafanua Guterres.

Nini kifanyike?

Katibu Mkuu amesema tunahitaji kujizuia na kubadili mwelekeo huu, tulaani na tutokomeze ubaguzi wa rangi katika ain azote zile na kuchukua hatua wakati wowote na popote pale unapoibuka.

“Viongozi wa aina yote katika sekta ya umma na binafsi, lazima wachukue hatua, wazungumze, wapaze sauti kumaliza janga hili.”

Amekumbusha kuwa kwa kuwa mwaka huu wa 2023 ni miaka 75 tangu kupitishwa kwa tamko la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu, UNDHR, “hebu tuahidi kung’oa ubaguzi wa rangi na kuzingatia utu na haki za kila mtu kokote aliko.”

 

Maisha ya weusi ni muhimu, (BLM) ni kampeni ya mtandaoni inayolenga kukabilianana ubaguzi wa rangi unaotekelezwa na polisi dhidi ya watu weusi.
© Unsplash/Clay Banks
Maisha ya weusi ni muhimu, (BLM) ni kampeni ya mtandaoni inayolenga kukabilianana ubaguzi wa rangi unaotekelezwa na polisi dhidi ya watu weusi.

Rais wa Baraza Kuu akazia hoja ya Guterres

Mapema hii leo katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Rais wa Baraza hilo Csaba Kőrösi aliwaeleza washiriki wa tukio la kuadhimishi siku hiyo ya kwamba kusanyiko lao ni kusherehekea wale waliotangulia na kufanya kazi kubwa na ambao wanaendelea kutokomeza aina zote za ubaguzi wa rangi na ubaguzi.

“Katika harakati hizi tunahitaji juhudi bila ukomo,” amesema Kőrösi akiongeza kuwa miaka 75 tangu kupitishwa kwa Tamko la Kimataifa la haki za binadamu, UDHR mchango wa mifumo ya ubaguzi wa rangi, utumwa bado inaendelea kuonekana kwenye jaii, taasisi na fikra.

Ubaguzi wa rangi ni kama gari kila mwaka kuna muundo mpya

“Kama virusi, ubaguzi unanyumbulika na kujibadilisha na mazingira katika nyakati na mazingira tofauti na yaelezwa kuwa ubaguzi wa rangi ni kama gari aina ya Cadillac ambalo kila mwaka kuna muundo mpya.”

Bwana Kőrösi  amesema mwenendo na dalili zake unaweza kubadili lakini madhara na wigo wake vinasalia vile vile.

Mathalani teknolojia inaweza kutumika kuongeza ufuatiliaji wa watu au jamii kinyume cha sheria na wakati huo huo kuimarisha mifumo ya kibaguzi.

Na bila usimamizi makini, mitandao ya kijamii inaweza kuibua na  kuchochea kampeni za ukatili wa misimamo mikali inayoweza kupanuka na kuzalisha mauaji ya kimbari.

Hatua za pamoja ni muhimu

Ametoa wito kwa serikali na mashirika ya teknolojia kufanya kazi pamoja kuweka kanuni za kusimamia majukwaa ya mtandaoni na kudhibiti kauli za chuki kokote zinakoibuka na katika lugha yoyote ile.

Maudhui ya siku ya leo na historia yake

Maudhui ya siku ya kupinga ubaguzi wa rangi duniani mwaka huu ni  udharura wa kutokomeza ubaguzi wa rangi, miaka 75 tangu kupitishwa kwa Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za binadamu.

Siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi wa rangi huadhimishwa kila mwaka tarehe 21 mwezi Machi ikiwa ni siku ambayo polisi nchini Afrika Kusini mwaka 1960 walishashambulia wanafunzi na kuwaua kwenye kitongoji cha Sharpeville. Waandamanaji 69 waliuawa wakati wakiandamana kwa amani dhidi ya utawala wa kibaguzi .