Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana tujengewe uwezo wa teknoljia na tupatiwe haki yetu ya elimu bora – Elionora CSW67

Elionora Emiel Wilfred, mwanafunzi wa kidato cha 4 katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Thereza wa Avila mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania akihojiwa na UN News Kiswahili service kandoni mwa mkutano wa CSW67 jijini New York Marekani.
UN News
Elionora Emiel Wilfred, mwanafunzi wa kidato cha 4 katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Thereza wa Avila mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania akihojiwa na UN News Kiswahili service kandoni mwa mkutano wa CSW67 jijini New York Marekani.

Wasichana tujengewe uwezo wa teknoljia na tupatiwe haki yetu ya elimu bora – Elionora CSW67

Wanawake

Mkutano wa 67 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW67 ukielekea tamati mwaka huu 2023 kikiwa kimebeba mada uvumbuzi, mabadiliko ya kiteknolojia, na elimu katika zama hizi za kidigitali kwa ajili ya kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote, mijadala mingi ilijikita katika kuwawezesha na kuhakikisha watoto wa kike wanaingia kwenye masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM ili hapo baadaye waweze kuchangia katika ubunifu wa teknolojia katika enzi hizi za dunia ya kidijitali.  

Soundcloud

Mashirika ya kimataifa na serikali  walihakikisha wasichana wenyewe wanapata fursa ya ushiriki na miogoni mwao ni Elionora Emiel Wilfred, mwanafunzi wa kidato cha 4 katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Thereza wa Avila mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania. 

Elionora alizungumza na Selina Jerobon wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa mataifa katika mahojiano kandoni mwa mkutano huo na kumuelezea changamoto na matarajio yake katika ulimwengu huu wa kidijitali. 

Elionora Emiel Wilfred(akitumia kompyuta yake), mwanafunzi wa kidato cha 4 katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Thereza wa Avila mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania akiwa na mwalimu wake Sara Mduma katika chumba cha mikutano cha Umoja wa Mataifa jijini …
UN News
Elionora Emiel Wilfred(akitumia kompyuta yake), mwanafunzi wa kidato cha 4 katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Thereza wa Avila mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania akiwa na mwalimu wake Sara Mduma katika chumba cha mikutano cha Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Je nini kimekuleta hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa? 

Mimi nimekuja hapa kudai haki za wanawake na wasichana hasa wale wanaotoka jamii yangu na wale wanaotoka katika nchi ambazo kidogo hazijaendelea, kwa sababu tunafaa kupatiwa elimu bora na kujengewa uwezo wa technolojia. 

Mnatumiaje teknolojia katika shule yako? 

Katika shule yangu hatujafikia uwezo wa kutumia teknolojia. Tunakumbwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa vifaa vya teknolojia kama vile kompyuta au vishkwambi, na mara nyingi unakuta kwamba walimu wanutumia kompyuta moja kuwafundisha wanafunzi 10 ama 15, na hivyo kusababisha wanafunzi wengi wakose kupata maarifa wa kutosha katika masomo ya teknolojia kwa sababu kawaida inafaa kuwa mwanafunzi mmoja na kompyuta yake. Tunakumbwa pia na ukosefu wa nishati na mtandao wa intaneti.  

Umejifunza nini katika mkutano huu wa CSW? 

Nimejifunza mengi sana; mosi ni kwamba ubunifu wa teknolojia unaanza na sisi wasichana, tukiamini tunaweza na kuongeza vitendo. Pili, nimejifunza kwamba tunaweza kuendeleza yale tumejiifunza hapa tukirejea nyumbani. Kwa mfano mimi nitaenda kuwatia moyo wasichana katika shule yangu, ambayo ni shule ya sekondari ya wasichana, kwamba sisi tunaweza kuleta mabadiliko katika nchi yetu kupitia masomo ya sayansi na teknolojia. Pia nimekuja na mikakati ambayo tumeanza kuifuata, na nikipatiwa nafasi nitahamasisha wasichana katika shule nyingine kwa sababu ninapenda nchi yangu sana na ningependa sote kama wasichana wa Tanzania tuweze kuchangia katika ujenzi wa taifa letu hasa kidijitali ambapo ulimwengu wa sasa unaelekea. Na mwisho kabisa ni kusihi shule zetu ziweze kuwekeza kiuchumi katika teknolojia. 

Umekuja pia kuwakilisha tamko, hilo tamko linahusu nini? 

Nimekuja hapa kuwakilisha wasichana na wanawake 80 kutoka nchi 13, nyingi zikiwa ni nchi zenye maendeleo duni. Tuliketi chini, tukayafikia na kuandika makubaliano kwa pamoja, na hapa nimekuja kueleza kikao hiki cha viongozi mbalimbali wa kiserikali na wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwamba tunataka wazazi walete wasichana wote shuleni, watupilie mbali ndoa za utotoni na mila potofu kama za ukeketaji wa wasichana na wanawake kwa lengo la kuwatayarisha kuolewa mapema. Tunataka wasichana wapatiwe elimu bora, watengenezwe kuwa viongozi wa kesho, tuweze kuchangia katika ubunifu na maendeleo ya nchi zetu kiuchumi kwa sababu sisi wasichana tunaweza! 

Elionora Emiel Wilfred (akitumia kompyuta yake ikiwa imegeuzwa vishkwambi au tablet), mwanafunzi wa kidato cha 4 katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Thereza wa Avila mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania katika chumba cha mikutano cha Umoja wa Mataifa ji…
UN News
Elionora Emiel Wilfred (akitumia kompyuta yake ikiwa imegeuzwa vishkwambi au tablet), mwanafunzi wa kidato cha 4 katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Thereza wa Avila mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania katika chumba cha mikutano cha Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.
Tweet URL

Ujumbe wako kwa wasichana wenzako ni nini? 

Ujumbe wangu si tu kwa ajili ya wasichana pekee, ni kwa wanawake na watu wote na ni kwamba, tujengee uwezo wa teknolojia na mazingira mazuri ya masomo wasichana kote ulimwenguni, kwa sababu wasichana na wanawake wanaweza nyanyua  jamii zao, ni nguzo wa taifa lao, na wanachangia kiuchumi katika nchi zao. Wasichana wasikatishwe tamaa yao ya kutaka kushiriki kwenye masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM kwa sababu wanaweza kuchangia kiasi kikubwa katika ubunifu wa teknolojia mpya na kuendeza nchi zao katika nyanja hizi na kukuza maendeleao ya kidijitali. Tunataka haki zetu kama tulivyodai. Tunataka usawa wa kijinsia. Wasichana tunaweza tukipatiwa nafasi stahiki, mfano mimi, ninapenda hesabu sana na nimeweza kuja hapa na kukutana na wakubwa wengi sana ambao sikutarajia kuketi kwa meza moja nao, na nikawaeleza yale yote nilikuwa nimepanga kusema, nimejifunza mengi kutokana na mazumgumzo hayo na nitapeleka shuhuda huo. Kwa hivyo sisi wasichana tunaweza!