Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya ICC yatoa waranti ya kukamatwa kwa Rais Putin wa Urusi

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague Uholanzi
UN Photo/Rick Bajornas
Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague Uholanzi

Mahakama ya ICC yatoa waranti ya kukamatwa kwa Rais Putin wa Urusi

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu inayoungwa mkono na Umoja wa Msataifa ICC leo imetoa hati au waranti ya kukamatwa kwa Rais Vladimir Putin wa Urusi kuhusiana na madai ya uhalifu wa kivita kuhusu kurejeshwa kwa lazima na uhamishaji haramu wa watoto kutoka eneo linalokaliwa la Ukraine amesema mkuu wa ICC.

Piotr Hofmański ambaye ni Rais wa ICC amesema "Yaliyomo kwenye hati ni siri kwa ajili ya kuwalinda waathirika. Hata hivyo, majaji waliamua kuweka wazi kuwepo kwa hati hizo, kwa maslahi ya haki na kuzuia uhalifu katika siku zijazo."

Pia mahakama hiyo ya ICC imetoa hati ya kukamatwa kwa kamishna wa haki za watoto wa Urusi Maria Alekseevna Lvova-Belova.

Mahakama hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imesema wakati wa kutangaza vibali hivyo kwamba “Amri hizo zinasema kwamba kila mmoja "anadaiwa kuhusika na uhalifu wa kivita wa kuwahamisha watoto kinyume cha sheria kutoka maeneo yanayokaliwa kwa mabavu nchini Ukraine hadi Urusi.”

Jukumu la makosa ya jinai

ICC imeeleza kuwa "Uhalifu huo unadaiwa kufanywa katika eneo linalokaliwa la Ukraine kuanzia tarehe 24 Februari 2022. Kuna sababu za kuridhisha za kuamini kwamba Bwana Putin na Bi. Lvova-Belova wanawajibika kwa uhalifu binafsi."

Mahakama hiyo inasema imebaini sababu za kuridhisha kwamba Bwana Putin anawajibika kwa kufanya vitendo hivyo moja kwa moja, kwa kushirikiana na wengine na, au kupitia kwa wengine, na kwa kushindwa kwake kudhibiti ipasavyo wasaidizi wa chini wa kiraia na kijeshi waliofanya vitendo hivyo, au kuruhusu tume kufanya vitendo hivyo na ambao walikuwa chini ya mamlaka na udhibiti wake madhubutiwakitekeleza wajibu wa amri ya juu zaidi”.

Madai yote yanaambatana na mkataba wa Roma. Ambapo Urusi na wala Ukraine wote sio washirika wa sheria ya mkataba huo, ambayo iliunda chombo cha mahakama ya ICC mwaka 1998.

Tweet URL

Kulinda waathirika

Mwendesha Mashtaka wa ICC, Karim A. A. Khan amesema wale waliohusika na madai ya uhalifu lazima wawajibishwe na kwamba watoto lazima warudishwe kwa familia na jamii zao.

"Hatuwezi kuruhusu watoto kutendewa kana kwamba wao ni nyara za vita. Matukio yaliyobainiwa na ofisi yangu ni pamoja na kufukuzwa kwa angalau mamia ya watoto waliochukuliwa kutoka katika vituo vya kulelea watoto yatima na kulea watoto. Wengi wa watoto hawa, tunadai, tangu wakati huo wametolewa ili wakalelewe katika Shirikisho la Urusi.”

Kupitia amri za rais zilizotolewa na Rais Putin, sheria ilibadilishwa nchini Urusi ili kuharakisha kukabidhiwa uraia wa Urusi, na hivyo kurahisisha kupitishwa kwao kulelewa na kuasiliwa na familia za Urusi.

Ameongeza kuwa "Ofisi yangu inadai kuwa vitendo hivi, miongoni mwa vingine, vinaonyesha nia ya kuwaondoa kabisa watoto hawa kutoka katika nchi yao. Wakati wa kufukuzwa huko, watoto wa Ukraine walikuwa watu waliolindwa chini ya Mkataba wa nne wa Geneva."

Hapo awali mahakama ilikuwa imeamua kwamba hati hizo zisichapishwe ili kuwalinda wathiriwa na mashahidi na pia kulinda uchunguzi, amesema Bwana Hofmański.

Hata hivyo, kwa kuzingatia kwamba mwenendo ulioshughulikiwa katika hali ya sasa unadaiwa kuwa unaendelea, na kwamba ufahamu wa umma juu ya hati hizo za kukamtwa unaweza kuchangia kuzuia utekelezaji zaidi wa uhalifu, mahakama iliona kuwa ni kwa maslahi ya haki kuidhinisha masjala kufichua hadharani kuwepo kwa hati hizo, jina la washukiwa, uhalifu ambao vibali vimetolewa, na njia za dhima kama ilivyoanzishwa na mahakama.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kutoa maoni yao juu ya hati za kukamatwa kwenye mkutano wa kawaida wa mchana mjini New York leo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, amesisitiza kwamba “ICC na Umoja wa Mataifa ni taasisi tofauti, zenye mamlaka tofauti."

Kuhusu ICC

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ni chombo huru na cha kudumu cha mahakama. Ilianzishwa kwa mujibu wa mkataba wa Roma, uliotiwa saini tarehe 17 Julai 1998 katika mkutano kwenye mji mkuu wa Italia.

Uwezo wake unaenda mbali hadi kwenye uhalifu mkubwa zaidi wa kimataifa uliofanywa baada ya tarehe 1 Julai 2002, tarehe ambayo mkataba wa Roma ulianza kutumika.

Mamlaka ya mahakama hiyo ni ni kwa ajili ya uhalifu wa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita, na uhalifu wa uchokozi.

Katika kipindi cha miaka 20 ya kwanza ya operesheni, ICC imejaribu na kutatua kesi zenye umuhimu kwa haki ya kimataifa, ikitoa mwanga juu ya uhalifu uliofanywa kwa matumizi ya askari watoto, uharibifu wa urithi wa kitamaduni, unyanyasaji wa kijinsia, au mashambulizi dhidi ya raia wasio na hatia.