Tumejizatiti kumwinua mwanamke kiteknolojia- Zanzibar
Tumejizatiti kumwinua mwanamke kiteknolojia- Zanzibar
Mkutano wa 67 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW67 ukikaribia kufunga pazia kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, viongozi waandamizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto huko Zanzibar Tanzania wamezungumzia ni kwa vipi serikali yao inachagiza matumizi ya teknolojia kama njia mojawapo ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs au Ajenda 2030.
Viongozi hao ni Waziri Riziki Pembe Juma na Katibu Mkuu wake, Abeida Rashid Abdallah wamesema hayo wakihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kandoni mwa mkutano huo wa CSW67 ambao maudhui yake ni kwa jinsi gani teknolojia na uvumbuzi vinaweza kumwinua na kumkomboa mwanamke wakati wa zama za sasa za kidijitali.
Tunatumia teknolojia kutoa huduma za afya na elimu
Mathalani Waziri Juma amesema hivi sasa “katika hospitali zilizoko katika kila wilaya 11 za Zanzibar kuna mashine ambazo zimefungwa na mgonjwa anapofanyiwa kipimo majibu yanatumwa kimtandao kwa madaktari wataalamu walioko India. Madaktari hao wakishasoma vipimo wanatoa ushauri aina ya tiba kwa mgonjwa.”
Ameongeza kuwa kwa njia hiyo, badala ya kumpeleka mgonjwa kumpeleka India, anapata matibabu hapo hapo na hivyo kupunguza gharama.
Kwa upande wa elimu, amesema katika Vyuo Vikuu na shule za sekondari masomo yanatolewa kwa kidijitali.
“Lakini si katika shule zote, hasa zile za kibinafsi ndiko inafanyika na katika shule za umma pia miundombinu inaanza kufungwa taratibu,” amefafanua Waziri huyo.
Amegusia pia jinsi shule zinatumia vishwambi kuwezesha watoto kupata nyaraka za masomo hata akiwa nyumbani ili aweze kujisomea.
Makundi sogozi kupitia WhatsApp pia
Waziri Juma amesema shule za msingi pia kuna makundi sogozi ya wazazi na walimu yanayowezesha wazazi sio tu kufuatilia mwenendo wa masomo ya watoto wao bali pia kupokea maelekezo kutoka kwa mwalimu.
“Zaidi haya makundi ni wazazi wanawake ndio wanahusika zaidi na hivyo unaweza kufuatilia maendeleo ya mtoto kupitia simu ya kiganjani badala ya Kwenda shuleni, hivyo unaokoa muda.”
Ujumuishaji wasichana na wanawake kwenye teknolojia
Akifafanua hoja hii, Katibu Mkuu Abeida Rashid Abdallah amesema kuna shule maalum zimeanzishwa kuhakikisha watoto wa kike wanaingia kwenye masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM.
Na zaidi ya yote kuna wanawake ambao wamepatiwa mafunzo nchini India ya kufunga nishati ya sola kwenye maeneo ya vijijini kupitia shirika liitwalo Barefoot. Shirika hili la Barefoot hutoa mafunzo hayo kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN Women nchini Tanzania
“Hii ni program ambayo inasaidia wanawake ambao hawana taaluma, hawajui kusoma na kuandika. Wanapewa teknolojia jinsi ya kutumia nishati ya jua. Hao wanawake wamefundishwa India na sasa wako Zanzibar na wanawake hao sasa wanaunganisha umeme vijijini,” amesema Katibu Mkuu Abeida.
Hivi sasa wanawake wanafundishwa wabadili fikra ya kwamba teknolojia itumike kuwainua kiuchumi badala ya kujifurahisha tu.
Je kuna changamoto?
Zipo mfano jinsi ya kutumia vifurushi kwa mfano walioko vijijini. Kwa hiyo kuna umuhimu wa kuweka miundombinu rafiki ya kufikisha mitandao hadi vijijini na itumike kwa makundi yote ya wanawake, wa mjini na vijiini.
Ujumuishaji wanawake wa makundi yote
Tunaamini kuwa ujumuishaji ni kila mtu mwanamke wa mjini na vijijini, awe na ulemavu au la. “Tuna kanzi data ya watu wenye ulemavu kufahamu waliko na wanafanya nini. Kwa wanawake wasioona, kuna programu maalum shuleni ili wasienguliwe kwenye kujifuza.”