Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

YouthWave inatumia teknolojia kumuinua mtoto wa kike

John Nyirenda, kijana Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la kusongesha ustawi wa vijana nchini Malawi, YouthWAVE Malawi akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa..
UN News
John Nyirenda, kijana Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la kusongesha ustawi wa vijana nchini Malawi, YouthWAVE Malawi akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa..

YouthWave inatumia teknolojia kumuinua mtoto wa kike

Wanawake

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mkutano wa 67 wa hali ya wanawake duniani, CSW67 ukiendelea maudhui yakiwa nafasi ya teknolojia na ugunduzi katika kumsongesha mwanamke tunapata mgeni studio ambaye ni John Nyirenda, kijana huyu, Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la kusongesha ustawi wa vijana nchini Malawi, YouthWAVE Malawi.  

Shirika hili kwa ushirikiano na wadau linatekeleza malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ikiwemo kuhakikisha afya kwa vijana kupitia matumizi ya teknolojia na ubunifu. 

YouthWave Malawi na maudhui ya teknolojia ya kidijitali kuna uhusiano gani? 

Sisi ni shirika la vijana ikimaanisha kwamba idadi kubwa ya timu yetu ni vijana na kama vijana tumebaini kuwa njia za kizamani za kufanya kazi haziwezi kufanya kazi, na teknolojia ndio njia yenyewe na kusonga mbele. Kwa hiyo ugunduzi na uvumbuzi ndio lugha ya sisi vijana kutumia. Sasa Youthwave inajikita katika elimu, afya na ushiriki wa vijana kwenye masuala ya kiraia. Jambo muhimu zaidi kwenye program zetu ni kwamba tunajumuisha teknolojia kuhakikisha vijana wanapata taarifa, ufahamu, stadi na mbinu zinazotakiwa kwa mujibu wa matumizi ya teknolojia. 

Ujumuishaji wa teknolojia ili kuongeza ufahamu kwa vijana una maana gani? 

Tumetumia njia iliyorahisishwa zaidi ya kutumia teknolojia. Idadi kubwa ya vijana tunaohudumia wako kwenye jamii za vijijini. Kwa hiyo tunatumia majukwaa kama WhatsApp ambapo tuliweza kuwaleta pamoja vijana ambao tayari wako kwenye vilabu vya vijana. Tunatumia majukwaa haya kualika wataalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya kuna na kufanya mijadala na vijana katika njia salama. Majukwaa haya yanasaidia kusambaza taarifa sahihi na za kweli kuhusu afya ya uzazi na kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia. Tunajadili pia ni vipi wasichana na wavulana wanaweza kushirikiana ili kusongesha usawa wa jinsia. 

Majukwaa yamekuwa jawabu la kukabili taarifa potofu na za uongo 

Wakati COVID-19 ilipokuja, kulikuwa na taarifa za uongo kwenye mitandao na vijana hawakupata taarifa za ukweli. Na kutokana na kuvurugwa kwa utoaji huduma kwenye vituo vya afya ilikuwa vigumu sana kwao kupata huduma  hivyo tukaona ni vema kuwaleta kwenye jukwaa moja ili wapate taarifa sahihi na washirikishane mambo muhimu. Nchini Malawi tuna vijana walio kwenye vilabu vilivyo chini ya mfumo wa serikali, na wengi wa vijana hawa wako kwenye Whatsapp. Sasa kilichokuwa kinakosekana ni taarifa sahihi na watu sahihi wa kuwaongoza. Kwa hiyo tumefanya kazi na Wizara ya afya kuleta watalaamu kujiunga na majukwaa hayo na kujadili na vijana. Vijana wanatoa mawazo yao na wanauliza  maswali. Vile vile majukwaa yameweza kuunganisha vijana na vituo vya afya ambako huko wanakwenda na kupata huduma za kupima VVU, magonjwa na zinaa na hii kweli imeweka mazingira salama kwa vijana kuweza kupata huduma katika vituo vya afya vilivyo karibu nao. 

YouthWave inatumia namna gani teknolojia kumsongesha mwanamke? 

Tuna mradi huko Machinga, wilaya iliyoko mashariki mwa Malawi na kwa msaada wa mdau wetu tunatumia miundombinu iliyoko ya kijamii. Nchini Malawi tuna mamlaka ya usimamizi wa mawasiliano na wamekuwa na vituo vya mawasiliano kwenye jamii nyingi. Hili ni jengo limewekewa kompyuta, lakini nyingi hazifanyi kazi. Kwa  hiyo shirika letu linaenda kwenye majengo hayo na kurekebisha na kuweka kompyuta hizo. Na kwa ushirikiano na wabia wetu wametuwezesha sisi kupata kompyuta nyingi zaidi na kutoa mafunzo ya elimu ya kidijitali. Kwa hiyo tuna mkufunzi kutoka Wizara ya Elimu ambaye anawapatia mafunzo ya msingi ya teknoloji kwa wasichana. Mfano matumizi ya kompyuta na infanyaje kazi. 

Soundcloud

Na je mradi huu umekuwa na mafanikio? 

Kupitia hii tumesaidia wasichana wengi kupata hamasa kujifunza sayansi na teknolojia kupitia mtazamo wa STEM. Na hii imeruhusu wasichana kutamani Kwenda shule kwa kuwa katika wilaya hii wasichana wengi wanaacha masomo, na kuna ndoa nyingi za utotoni. Lakini kupitia kituo hiki, wasichana wengi wanaweza Kwenda na kujifunza. Tunawaambia pia wale walio elimu ya msingi na sekondari wanaweza kufika na kujifunza bila gharama yoyote. Imesaidia sana ongezeko la wasichana kujiunga na masomo na kiwango cha kuacha shule miongoni mwa wasichana kimepungua. Na hii sasa ndio nguvu ya teknolojia. 

CSW si pahala pa maneno matupu bali vitendo 

Ni kuona viongozi wakichukua hatua. Tumeona wajumbe kutoka maeneo mbalimbali, mawaziri, wakuu wa taasisi, watendaji wakuu wa mashirika! Huu ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo. CSW si jukwaa la kuzungumza tu, bali  ni jukwaa la kuchokoza viongozi wetu wachukue hatua.Kama vijana tutaendelea kuwajibisha viongozi wetu na wasimamizi wa haki kuwaambia wanatakiwa kuwekeza kwenye teknolojia na wahakikishe wasichana na wanawake wana fursa ya kupata mafunzo ya Sayansi na Teknolojia,  Sayansi lazima ianze kutambulishwa kwa wasichana katika umri mdogo na kwa njia hiyo tutaweza kufikia lengo letu la kusongesha usawa wa kijinsia.