Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa UN wakunja jamvi Doha kwa ahadi ya mshikamano  kwa nchi za LDC

Mwanamke akiandaa chakula jikoni kwake katika moja ya vijiji nchini Chad
© WFP/Evelyn Fey
Mwanamke akiandaa chakula jikoni kwake katika moja ya vijiji nchini Chad

Mkutano wa UN wakunja jamvi Doha kwa ahadi ya mshikamano  kwa nchi za LDC

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkutano wa tano wa Umoja wa Mataifa kuhusu nchi zenye maendeleo duni duniani LDC5 uliokuwa ukifanyika Doha Qatar leo umekunja jamvi kwa nchi wanachama kuahidi kutekeleza mpango wa Doha wa kuchukua hatua(DPoA).

Mpango huo wa miaka 10 unalenga kuzirejesha kwenye msitari wa kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs, nchi 46 zenye maendeleo dunia zaidi kwa kufanya upya na kuimarisha ahadi kati ya nchi za LDC na washirika wao wa maendeleo kuashiria hatua ya mageuzi kwa nchi zilizo hatarini zaidi duniani.

Azimio la kisiasa la Doha lilipitishwa na kupigiwa makofi katika ukumbi wa mkutano wa kituo cha kitaifa cha Qatar, ambapo LDC5 imekuwa ikiendelea tangu tarehe 5 Machi.

Ikiwa ni ishara ya enzi mpya ya mshikamano, na manufaa makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa nchi 46 zenye maendeleo duni zaidi duniani, hatua ya leo inakuja karibu mwaka mmoja baada ya DPoA kupitishwa katika sehemu ya kwanza ya mkutano wa tarehe 17 Machi 2022 huko New York.

Azimio linaainisha hatua za kuchagiza mabadiliko na kufungua uwezo wa  mataifa ya LDC, likijumuisha uundaji wa mfumo wa akiba au njia mbadala, kuanzia uhamishaji fedha hadi kukabiliana na majanga mbalimbali na hatua za kujenga mnepo kwa nchi zenye maendeleo duni.

“Ahadi na majukumu hayaishi na kuanza kwa kusainiwa kwa hati au kuhudhuria mikutano. Ni lazima ziwe kitovu katika juhudi zetu kuelekea mwaka 2030 na ziendelezwe kwa muongo mzima,” amesema Amina Mohammed, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati wa kufunga mjada wa mkutano huo.

Naibu Katibu Mkuu wa Un Amina J. Mohammed akihutubia wakati wa kufungwa kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa LDC5 mjini Doha Qatar
UN Photo/Evan Schneider
Naibu Katibu Mkuu wa Un Amina J. Mohammed akihutubia wakati wa kufungwa kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa LDC5 mjini Doha Qatar

Lazima tusonge mbele zaidi

Bi. Mohammed amebainisha kuwa mambo matano muhimu kutoka kwa DPoA ambayo ni chuo kikuu cha mtandaoni, mfuko wa usaidizi wa kuhitimu kutoka LDC, suluhu ya uhifadhi wa chakula, kituo cha usaidizi cha uwekezaji, na mbinu ya kukabiliana na mgogoro na kujenga mnepo "itakuwa jibu la changamoto kuu zinazokabili mataifa ya LDC, na kuweka mwongozo  kwa ajili ya mustakabali wenye mafanikio na wenye usawa zaidi”.

Ameendelea kusema kwamba "Lakini mafanikio si ya moja kwa moja. Lazima tusonge mbele zaidi ili kufikia malengo haya, nchi za LDC zitahitaji ufadhili mkubwa na wa kwa kiwango kikubwa, na wa kuelekezwa ambapo ni muhimu zaidi."

Alibainisha kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hapo awali alipendekeza mageuzi ya usanifu wa fedha wa kimataifa, pamoja na kichocheo cha SDG cha angalau dola bilioni 500 kwa mwaka, ili kuelekeza rasilimali kuelekea maendeleo endelevu ya muda mrefu na mabadiliko ya haki. Ufadhili huu unaweza kuzisaidia nchi za LDC kushughulikia masuala ambayo yanawazuia kufikia uwezo wao.

"Ikiwa tunataka kuwa na matumaini yoyote ya kufikia SDGs, ni lazima tuwaweke mbele kwanza wale ambao wako nyuma zaidi katika safari zao za maendeleo," amesema naibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Akiwa Doha, Bi. Mohammed pia, amekutana na na maafisa wa serikali, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na waratibu wakazi wa Umoja wa Mataifa kutoka duniani kote.

Katika mikutano yake, amesisitiza umuhimu wa kupunguza majanga na kuongeza mnepo kwa LDCs, na DPoA kama mwongozo wa kuinua nchi zilizo hatarini zaidi.

Mkutano wa tano wa Umoja wa Mataifa kuhusu nchi zenye maendeleo duni (LDC5) unafanyika jijini Doha, Qatar.
UN Photo/Evan Schneider
Mkutano wa tano wa Umoja wa Mataifa kuhusu nchi zenye maendeleo duni (LDC5) unafanyika jijini Doha, Qatar.

Wiki hii katika LDC5

Chini ya mada y‘Kutoka kwenye uwezekano hadi ufanisi’, mkutano wa LDC5 ulilenga kuleta mabadiliko yenye athari chanya kwa watu bilioni 1.2 wanaoishi katika nchi za LDC.

Mkutano wa LDC5 ulikaribisha washiriki takriban 9,000, wakiwemo wakuu wa nchi na serikali 46 na karibu mawaziri na makamu wa mawaziri 200, ambao walitaka msaada wa haraka kutoka kwa nchi zilizoendelea ili kusongesha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira katika nchi za LDC.

Viongozi wa makampuni ya biashara, pamoja na mashirika ya kiraia, vijana na wadau wengine, walishiriki mipango, na mapendekezo katika maeneo mbalimbali, kuanzia kwa kuimarisha ushiriki wa nchi za LDC katika biashara ya kimataifa na ushirikiano wa kikanda hadi kutumia nguvu za sayansi, teknolojia, na uvumbuzi.

Naibu Katibu Mkuu amekiri kuhusu ushiriki huo mpana, akisema “Katika wiki hii tumeshuhudia kile ambacho kinaweza kupatikana kupitia ushirikiano wa kweli na mazungumzo ya kimataifa. Kila mchango kupitia vijana, ushirikiano wa Kusini-Kusini, sekta binafsi, wabunge, na mashirika ya kiraia umechangia nishati, maono na mawazo kwa ajili ya mabadiliko ya kudumu."

Majadiliano katika LDC5 yalilenga katika utekelezaji wa DPoA. Makubaliano yaliyofikiwa wiki hii yatasaidia  nchi za LDC kushughulikia mzozo wa sasa, wa kujikwamua kutoka kwenye janga la coronavirus">COVID-19 hadi mabadiliko ya tabianchi, na kuwasaidia kurejea kwenye mstari malengo ya maendeleo endelevu SDGs na kupiga hatua za maendeleo kuelekea kuhitimu kutoka katika kundi la nchi za LDC.

Rabab Fatima mwakilishi wa UN wa OHRLLS akizungumza mjini Doha Qatar kwenye mkutano wa LDC5
UN Photo/Ruwan Dilanka
Rabab Fatima mwakilishi wa UN wa OHRLLS akizungumza mjini Doha Qatar kwenye mkutano wa LDC5

Rabab Fatima, katibu mkuu wa mkutano huo na mwakilishi mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi zenye maendeleo duni, nchi zinazoendelea zisizo na Bandari na nchi zinazoendelea visiwa vidogo (UN-OHRLLS) amesema "nchi za LDC zina uwezo mkubwa zaidi ambao haujatumiwa duniani, kuanzia kwa asili hadi rasilimali watu. Tulichowasilisha wiki hii kinaweza kutumia uwezo huu na kupanga mustakabali bora kwa watu wa nchi za LDC."

Amewataka waliohudhuria mkutano huo baada ya kuondoka Doha, kuzingatia "kile tunachoweza kuchangia katika kutekeleza mpango wa utendaji wa Doha katika muktadha na uwezo wetu".

Akisisitiza kwamba dhamira ya kisiasa ndiyo "mafuta ambayo yataendesha injini ya maendeleo", akikaribisha maneno ya umiliki wa kitaifa wa DPoA na kuwataka washirika wa maendeleo kurekebisha sera zao za ushirikiano wa kitaifa kwa njia ambayo inakidhi matamanio na matarajio ya nchi zilizoendelea.

Lazarus McCarthy Chakwera, Rais wa Malawi na mwenyekiti wa kundi la nchi zenye maendeleo duni, ameuelezea mkutano huo kama ushindi wa mtindo na dhamira.

Matarajio yalikuwa makubwa sana mkutano ulioanza amesema, akikumbusha miito mingi ya ushirikiano imara iliyotolewa katika siku tano zilizopita.

Nchi zilizoendelea zilikumbushwa juu ya ahadi zao rasmi za usaidizi wa maendeleo (ODA), akisisitiza kuwa ni wakati wa kutimiza ahadi hiyo ya kihistoria ya kutenga kati ya asilimia 0.15 na 0.20 ya pato lao la taifa. Kama hii, na ahadi nyingine katika maeneo ya biashara, uwekezaji na uhanmishaji wa teknolojia vinaweza kuzingatiwa hivyo tutaondoka na matumaini mapya kwamba mpango wa kuchukua hatua wa Doha utatekelezwa kikamilifu.

Baadhi ya washiriki kwenye mkutano wa LDC5 Doha Qatar
UN Photo/Ruwan Dilanka
Baadhi ya washiriki kwenye mkutano wa LDC5 Doha Qatar

Naye Soltan bin Saad Al-Muraikhi, waziri wa mambo ya nje wa Qatar pia ametoa hotuba ya kufunga kama Rais wa mkutano huo.

Akibainisha ahadi zilizoahidiwa katika siku tano zilizopita, alisisitiza haja ya hatua za vitendo na akakumbusha ahadi muhimu za kifedha za nchi yake. Qatar itaweka nchi zenye maendeleo duni katika kitovu cha ushirikiano wa kimataifa, amesema.