FAO yaandaa mbinu ya kuwezesha wajasiriamali wadogo vijijini kuvutia wawekezaji
FAO yaandaa mbinu ya kuwezesha wajasiriamali wadogo vijijini kuvutia wawekezaji
Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO limekamilisha mwongozo mpya zaidi ulioboreshwa wenye lengo la kuleta mapinduzi kwa wajasiriamali wadogo na wa kati vijijini mwongozo ambao unapatikana mtandaoni.
Taarifa ya FAO iliyotolewa leo huko Roma, Italia inasema mwongozo huo uitwao RURALINVEST umesheheni mbinu za kumwelekeza mtumiaji nadharia na vitendo za kuanzisha na kutekeleza mipango ya biashara endelevu.
Kichocheo cha kuanzisha mwongozo huu
“Katika mazingira ya kutokuweko kwa miundo fanisi ya biashara, wakulima na wajasiriamali vijijini hukumbwa na changamoto za kushawishi taasisi za fedha au benki kuwekeza katika biashara zao na mara nyingi kwa kuzingatia kuwa kilimo huonekana kuwa eneo hatari la uwekezaji,” imefafanua taarifa hiyo ikiongeza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya chakulia kinacholiwa duniani kinazalishwa na kilimo cha kaya, lakini ni chini ya asilimia 10 tu ya wakulima wadogo ndio wana uwezo wa kupata mikopo kutoka Benki au ufadhili.
Hii ina maana kwamba RuralInvest itawezesha wajasiriamali wa kati na wadogo kuchanua kwani itawajengea uwezo kupitia mafunzo kutoka kwa wakufunzi mahsusi na hatimaye kutafsiri mawazo yao ya kibiashara kuwa mipango mahususi na kisha kuvutia wawekezaji.
Kituo cha Uwekezaji cha FAO
Mwongozo umeandaliwa na kituo cha uwekezaji cha FAO na kwa kuzingatia uzoefu wa timu hiyo katika Nyanja za uwekezaji vijijiji, mbinu zilizotumika na tayari zimewekwa katika mazingira ya kuwa na matokeo chanya.
Katika kipindi cha miaka mitano, RuralInvest imesaidia ukuaji wa kilimo biashara zaidi ya 1,000 katika nchi zaidi ya 15 na kuchochea uwekezaji wa takribani dola million 34 za uwekezaji na kusaidia kuanzishwa kwa kampuni za za ujasiriamali vijijini duniani kote.
Teknolojia iliyotumika kwenye mwongozo wa sasa ni rafiki zaidi ikiwa ina lugha zaidi ya moja na inaweza kutumiwa na watu wengi zaidi.
Teknolojia inafanyaje kazi?
Mwongozo huo wa mtandaoni unapatikana kupitia wavuti wa RuralInvest na unawezesha watumiaji kuandaa mipango ya biashara yenye ueledi. Maafisa ugaji wanaelezwa dira ya mkulima, na hivyo anajifunza ni vipi na aina gani ya takwimu zinapaswa kukusanywa na kuingizwa kwenye wavuti ambayo yenyewe sasa inachakata na kumpatia mhusika mpango wa biashara autakao.
Nani atumie RuralInvest?
Mbinu hii imebuniwa kwa ajili ya maafisa ugani na washauri wa kuandaa mipango ya biashara.
Halikadhalika ina ubi ana Vyuo Vikuu au vituo vya wajasiriamali ambako wanaweza kutoa mafunzo kwa njia mtandao ili kujenga ueledi wa matumizi ya mbinu hii.