Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji wa kimkakati unahitajika ili kuboresha uhakika wa chakula na maji kwa mamilioni ya Wasomali

Wanufaika wa miradi inayotekelezwa na FAO nchini Somalia
©FAO/Arete/Ismail Taxta
Wanufaika wa miradi inayotekelezwa na FAO nchini Somalia

Uwekezaji wa kimkakati unahitajika ili kuboresha uhakika wa chakula na maji kwa mamilioni ya Wasomali

Msaada wa Kibinadamu

Wakati misaada ya kibinadamu imesaidia baadhi ya maeneo ya Somalia kutotumbukia kwenye baa la njaa, wananchi wa vijiji nchini humo bado wanaendelea kukabiliwa na ukosefu wa uhakika wa chakula limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO hii leo baada ya hivi karibuni kutangazwa matokeo ya uchunguzi wa uhakika wa chakula.

Taarifa iliyotolewa leo kutoka jijini Rome, Italia na FAO imeeleza kuwa ili wasomali hao waweze kurejesha hali ya kawaida kwa wananchi wa vijijini kujikimu inahitajika si tu kuongeza usaidizi wa kibinadamu bali pia kuja na mbinu za kuleta mabadiliko ili kuhakikisha wananchi wanapata uhakika wa chakula, maji, na mnepo katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Kwa mujibu wa mchanganua uliofanywa hivi karibuni kuangalia uhitaji wa upatikanaji wa chakula IPC hakuna tena utabiri wa kuweza kutokea kwa baa la njaa hata hivyo Somalia imebaki kuwa eneo lenye “Hatari ya njaa”.

Misaada ya kibinadamu iliyotolewa kwa ushirikiano mkubwa na mashirika mbalimbali imesaidia sana Somalia kutotangazwa kuwa na baa la njaa.

Ukame na ukosefu wa usalama nchini Somalia umemfurusha Rukia Yaarow Ali na watoto wake 9 na sasa anaishi ukimbizi nchini Kenya. Mume amemkimbia kwa sababu ya ukame na hawezi tena kutunza familia.
UNFPA Kenya
Ukame na ukosefu wa usalama nchini Somalia umemfurusha Rukia Yaarow Ali na watoto wake 9 na sasa anaishi ukimbizi nchini Kenya. Mume amemkimbia kwa sababu ya ukame na hawezi tena kutunza familia.

Hali ikoje

Ripoti hiyo inaonesha kuwa kati ya mwezi Januari na Machi 2023, karibu watu milioni 5 kote Somalia walikuwa katika ngazi ya tatu ya kutokuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula IPC ikijumuisha watu 96,000 wanaokabiliwa na janga la njaa ya janga katika ngazi ya tano IPC 5.

Njaa inatarajiwa kuongezeka, na watu milioni 6.5 ambao ni zaidi ya theluthi moja ya jumla ya idadi ya watu nchini humo wanakadiriwa kuwa wanakabiliwa na 'shida' au kutokuwa na uhakika wa chakula kwa ngazi ya tatu (IPC 3) au juu zaidi yah apo kati ya Aprili na Juni mwaka huu ikiwemo watu 223,000 wanaotabiriwa kuwa na janga la njaa kwa ngazi ya tano IPC5.

Taarifa hiyo ya FAO imeongeza kuwa idadi ya wakulima ambao pia ni wafugaji katika wilaya ya Burhakaba na wakimbizi wa ndani huko Baidoa na Mogadishu wanakabiliwa na 'hatari ya njaa' kati ya mwezi Aprili hadi Juni 2023 ikiwa mvua za msimu wa 2023 zinashindwa kunyesha na misaada ya kibinadamu haitafikia wenye uhitaji zaidi.

Fadumo Ibrahim, mkulima huyu akipalilia shamba lake la mahindi huko Marka, Somalia mwezi tarehe 22 Novemba mwaka 2021.
©FAO/Arete/Abdulkadir Zubeyr.
Fadumo Ibrahim, mkulima huyu akipalilia shamba lake la mahindi huko Marka, Somalia mwezi tarehe 22 Novemba mwaka 2021.

Nini kifanyike 

FAO imesema kuwa kuendelea kufanya biashara kama kawaida sio chaguo tena na imependekeza mifumo mipya yenye uratibu jumuishi ili kuhamisha uwekezaji wa muda mrefu wenye kuleta suluhu za muda mrefu za uhakika wa upatikaji wa maji na chakula.

"Misaada ya kuokoa maisha inayotolewa na FAO inasaidia si tu kuokoa maisha bali pia kutengeneza njia za kuwawezesha kujikwamua haraka” amesema Rein Paulsen, mkurugenzi wa Ofisi ya Dharura na Ustahimilivu wa FAO.

Hata hivyo ameeleza kuwa “Mzozo uliojitokeza sasa katika mwaka wake wa tatu umedhoofisha mikakati ya kukabiliana na walio hatarini zaidi, na familia zinaendelea kukabiliwa na kuhamahama, utapiamlo kwa watoto na hata kupoteza maisha. Uwekezaji kwenye mifumo yenye kutoa maonyo mapema, ufadhili rahisi wa hatua za zinazotarajiwa na njia zilizoratibiwa za ujenzi wa ujasiri ni muhimu ili kuvunja mzunguko wa mwaka baada ya mwaka wa hatari za ukosefu wa chakula hususan kwa jamii za vijijini.”

Wakati athari za ukame katika Pembe ya Afrika zikiendelea kushuhudiwa, njia za kiwango vya juu za kuokoa maisha na usalama wa kuishi zitabaki kuwa muhimu mnamo 2023.

Hali ya sasa inaonesha hitaji la haraka la kuongeza uwekezaji na sera za janga kupunguza hatari na ujenzi wa ujasiri, kuangazia jukumu muhimu la kilimo katika kufikia mustakabali endelevu kwa watu wa Afrika Mashariki.

Safiya Mahdi Cise, mnufaika wa mradi wa FAO wa kuboresha ufugaji akiwa amembeba ndama wa kondoo huko kijiji cha  Duudwayne, wilaya ya Baki nchini Somalia
© FAO / Isak Amin / Arete
Safiya Mahdi Cise, mnufaika wa mradi wa FAO wa kuboresha ufugaji akiwa amembeba ndama wa kondoo huko kijiji cha Duudwayne, wilaya ya Baki nchini Somalia

FAO imefanya nini

FAO imepokea msaada wa dola milioni 183 ikiwa ni sawa na 68% ya fedha zinazohitajika chini ya Mpango wa Kuzuia Njia ya FAO ya Somalia  kwa kipindi cha mwezi Mei 2022-Juni 2023.

Kwa fedha hizo, FAO imeweza kuwafikia zaidi ya watu milioni 1 au 47% ya walengwa milioni 2.4.

FAO inahitaji haraka fedha za ziada kuongeza ufikiaji wa haraka wa chakula na mahitaji ya kimsingi katika maeneo ya vijijini, maeneo yaliyo magumu kufikika na yasiyoweza kufikiwa, na pia kulinda maisha na msaada wa uzalishaji wa chakula katika maeneo ambapo bado inawezekana kufanya hivyo.