Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya za Hifadhi ya mazingira na wanyamapori zinalipa

Fatuma Said Mbembati, Mwenyekiti wa Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Waga inayohusika na baadhi ya maeneo ya mikoa ya kusini mwa Tanzania ya Iringa na Mbeya.
UNDP/Sawiche Wamunza
Fatuma Said Mbembati, Mwenyekiti wa Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Waga inayohusika na baadhi ya maeneo ya mikoa ya kusini mwa Tanzania ya Iringa na Mbeya.

Jumuiya za Hifadhi ya mazingira na wanyamapori zinalipa

Tabianchi na mazingira

Mradi wa kupambana, kudhibiti Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara unaotekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo duniani nchini Tanzania kupitia Jumuiya za hifadhi ya wanyamapori huko kwenye eneo la ekolojia la Ruaha Rungwa Nyanda za juu za kusini nchini humo umeanza kuzaa matunda.

Msingi wa mradi huo ni kuhakikisha kuwa maeneo ambapo kuna mwingiliano wa wanyamapori na binadamu  yanahifadhiwa na wakati huo huo yakiwa na faida kwa binadamu na wanyama.

Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Waga

Mathalani katika  pori tengefu la Waga linalopakana na mikoa ya Iringa na Mbeya manufaa yameanza kudhihirika kwa Jumuiya ya Waga ya kuhifadhi eneo hilo.

Pori la Waga awali lilikuwa makazi ya watu lakini baada ya serikali kuona kwamba lina mwingiliano wa wanyama wengi, watu wakahamishwa kwenda vijiji jirani.

Kwa mujibu wa Katibu wa jumuiya hii, Meshaki Kisoma,  eneo hilo lina vivutio vya wanyama wengi kutoka mbuga ya wanyama ya Taifa ya Ruaha kwa sababu lina mito.

Eneo hilo pia lina mito midogo midogo isiyo maarufu sana inatokea vijiji vya Igoma, Ihazutwa na vile vile kuna mto  Lyandembele unaopita kando ya hifadhi ya wanyamapori ya Taifa, ambalo linatumika kama chanzo cha maji kwa wanyama katika hifadhi hii.

Pori tengefu la Waga

Pori la Waga ni eneo tengefu ambalo kwa mujibu wa Bwana Kisoma serikali iliona lisiwe ndani ya hifadhi ya taifa ya Ruaha na kwamba manufaa yote yatakayopatikana kwenye  hii hifadhi ni kwa ajili ya vijiji wanachama wanaozunguka eneo hilo. Na kwa maana hiyo viongozi wa maliasili walizunguka vijiji tofauti na kueleza kuwa kwa kupitia pori hili tengefu mtaweza kuboreshewa ofisi za vijiji, madarasa na huduma za afya zitaboreshwa kwa kupitia fedha hizo ambazo wawekezaji wanawekeza na fedha vijiji tofauti tofauti.”

UNDP inafanya nini sasa?

UNDP kupitia mradi wake wa kupambana, kudhibiti Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara inasaidia Tanzania kutekeleza Mkakati wake wa kitaifa wa kukabili ujangili na biashara haramu ya nyara, NSCPIWT kwa kuimarisha sheria na uwezo wa kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori katika ngazi ya kitaifa.

Halikadhalika mradi unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na nchi jirani kwa mujibu wa Mradi wa kimataifa wa wanyamapori uliozinduliwa mwaka 2015 na Fuko la kimataifa la mazingira, GEF.

Soundcloud

Je kuna faida hadi sasa za uwepo wa pori tengefu la Waga?

Bila shaka, amesema Katibu wa Jumuiya hiyo ya hifadhi ya wanyamapori ya Waga akitaja mafanikio kuwa ni pamoja na kijiji cha Igoma kina ofisi nzuri. Halikadhalika hospitali ya kijiji cha Maoninga imeweza kuboreshwa kupitia fedha za Waga.

Jumuiya za Hifadhi ya mazingira na wanyamapori zinalipa

Kwanza kabisa serikali ya kijiji inapata mapato, wawekezaji wanatoa fedha tunapata mapato .Vijiji navyo vinapata fedha na kuzigawa kwa vikundi vya wajasiriamali kwa ajili ya maendeleo.

Ametaja pia shule moja ya sekondari inatumia fedha kununulia vifaa vya shule.

Vijiij vitano vinahusika na uhifadhi wa pori la Waga

Fatuma Said Mbembati, Mwenyekiti wa  Jumuiya ya Waga akiwa na jukumu la kusimamia uendeshaji pamoja na kumulika vyanzo vya mapato anasema pori la Waga linasimamiwa na vijiji vitano ambavyo ni Maoninga, Igomaa, Ihanzutwa, Nyamakuyu na Nyakadete.

“Pori lina wanyama mbalimbali kama simba, chui, twiga, nyati, swala na zaidi ya yote lina uoto wa asili kama miti mingi na nyasi,” amesema Bi. Mbembati akieleza pia ni eneo zuri kwa utalii.

Ujumbe wa siku ya wanyamapori tarehe 3 mwezi huu wa Machi ulichagia ubia katika uhifadhi wa wanyamapori kama njia mojawapo ya kulinda sio tu bayonuai bali pia kuweka utangamano kati ya wanyamapori na binadamu hasa kwenye maeneo yenye muingilano wa wanyamapori na binadamu.