Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW imekuwa ikisongesha haki za wanawake tangu mwaka 1946

Wanawake katika moja ya vijiji vya jimbo la Bihar India wakiwa wamekutana katika mkutano wa kijamii
UN Women
Wanawake katika moja ya vijiji vya jimbo la Bihar India wakiwa wamekutana katika mkutano wa kijamii

CSW imekuwa ikisongesha haki za wanawake tangu mwaka 1946

Wanawake

Mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa wa kamisheni ya hali ya wanawake (CSW) hukutana mwezi Machi kushughulikia ukosefu wa usawa ulioenea, unyanyasaji na ubaguzi ambao wanawake wanaendelea kukumbana nao duniani kote.

Huu ni mwongozo mfupi wa mambo matano muhimu ya mkutano huo wa ngazi ya wa Umoja wa Mataifa.

Kwa viwango vya sasa, itachukua karibu karne nyingine tatu kuleta usawa kwa wanawake na wasichana.

Wakikabiliwa na ukosefu wa usawa unaoendelea, takriban wanawake na wasichana milioni 383 wanaishi katika umaskini uliokithiri, na kila baada ya dakika 11, mwanamke au msichana anauawa na mtu fulani katika familia yake.

Hizi ni baadhi ya sababu ambazo CSW inaendelea kuwa muhimu na imekuwa safu muhimu sana kwenye kalenda ya Umoja wa Mataifa tangu ilipoitishwa mara ya kwanza, muda mfupi baada ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa wenyewe.

1: Kusukuma hatua kwa miongo minane

 

Mwenyekiti wa kamati ya haki za binadamu Bi. Eleanor Roosevelt (Kulia) akiwa na Bi.Hansa Mehta wa India
UN Photo/Marvin Bolotsky
Mwenyekiti wa kamati ya haki za binadamu Bi. Eleanor Roosevelt (Kulia) akiwa na Bi.Hansa Mehta wa India

(PHOTO)

Kazi ya kamisheni hiyo ilianza mwaka wa 1946, siku chache baada ya mikutano ya uzinduzi ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kumsikia Mama wa Rais wa zamani wa Marekani Eleanor Roosevelt na sehemu ya ujumbe wa nchi hiyo, akisoma barua ya wazi iliyoelekezwa kwa "wanawake wa dunia".

Bi. Roosevelt alikuwa ametoa wito kwa “Serikali za dunia kuhimiza wanawake kila mahali kushiriki kikamilifu katika masuala ya kitaifa na kimataifa, na kwa wanawake wanaotambua fursa zao kujitokeza na kushiriki katika kazi ya amani na ujenzi mpya walivyofanya katika vita na upinzani”.

Tume ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kiuchumi na kijamii (ECOSOC) ilianzisha tume ndogo mara moja.

Wanachama wake sita kutoka Uchina, Denmark, Jamhuri ya Dominika, Ufaransa, India, Lebanon, na Poland  walipewa jukumu la kutathmini "matatizo yanayohusiana na hali ya wanawake" ili kuishauri tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, mtangulizi wa Baraza la haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.

Katika ripoti yake ya kwanza, "wajumbe walizingatia kwamba kazi ya tume ndogo inapaswa kudumu hadi wanawake wafikie kiwango cha kuwa katika usawa na wanaume katika nyanja zote za masuala ya binadamu".

Tangu mwanzo kulikuwa na wito wa kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na kuweka kipaumbele kwa haki za kisiasa, "kwani maendeleo madogo yasingeweza kupatikana bila wao", pamoja na mapendekezo ya maboresho katika nyanja za elimu ya kiraia, kijamii na kiuchumi, ambapo "matatizo yanapaswa kushughulikiwa kwa wakati mmoja", ilisema ripoti.

Aidha, ripoti hiyo ilitoa wito wa kuwa na "Kongamano la Umoja wa Mataifa la wanawake ili kuendeleza mpango huo."

Kufikia Juni 1946, ikawa rasmi “Kamisheni ya Hali ya Wanawake”, kama moja ya mashirika tanzu ya ECOSOC.

 Kuanzia 1947 hadi 1962, kamisheni ilizingatia kuweka viwango na kuunda mikataba ya kimataifa ya kubadilisha sheria za kibaguzi na kukuza ufahamu wa kimataifa wa masuala ya wanawake.

2: Mikataba ya kihistoria iliyofikiwa

Mkulima Biresaw, kutoka Ethiopia.
© World Bank/Dana Smillie
Mkulima Biresaw, kutoka Ethiopia.

Kuanzia siku za awali za kamisheni hiyo, kuongezeka kwa wanachama wake kulichangia baadhi ya mikataba ya kimataifa iliyokubaliwa zaidi katika historia ya Umoja wa Mataifa. Hapa ni michache tu.

Ikimsaidia Bi. Roosevelt, mwenyekiti wa kamati ya kuandaa Tamko la Kimataifa la Haki za Kibinadamu, kamisheni ilifanikiwa kupinga dhidi ya marejeleo ya "wanaume" kama kisawe cha ubinadamu.

Pia ilianzisha lugha mpya, katika tamko hilo ambayo ni jumuishi zaidi katika toleo la mwisho lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1948.

Mwaka 1963, juhudi za kujumuisha viwango vya haki za wanawake zilisababisha Baraza Kuu kuomba kamisheni kuandaa azimio la kutokomeza ubaguzi dhidi ya wanawake, ambalo Umoja wa Mataifa ulilipitisha mwaka 1967.

CSW ilikuwa na mchango muhimu katika kupitishwa kwa Azimio la Beijing na mfumo wa utekelezaji wake la mwaka 1995, ambalo ni waraka muhimu wa sera ya kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia.

3: Nchi nyingi mahitaji mengi zaidi

Mwanamke akichuuza chakula katika soko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
UN Women/Carlos Ngeleka
Mwanamke akichuuza chakula katika soko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanachama wa Umoja wa Mataifa na ushahidi ulioongezeka katika miaka ya 1960 kwamba wanawake waliathiriwa kwa kiasi kikubwa na umaskini, CSW ilizingatia mahitaji ya wanawake katika maendeleo ya jamii na vijijini, kazi za kilimo, uzazi wa mpango, na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Pia ilihimiza mfumo wa Umoja wa Mataifa kupanua wigo wa usaidizi wa kiufundi ili kuendeleza maendeleo ya wanawake, hasa katika nchi zinazoendelea.

Katika kusongesha kazi katika suala hili, CSW pia ilitayarisha mkataba unaofunga kisheria wa “Kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW) mwaka wa 1979.”

Katika muongo huu, Umoja wa Mataifa ulitangaza mwaka 1975 kuwa mwaka wa kimataifa wa wanawake na kuitisha kongamano la kwanza la dunia kuhusu wanawake, lililofanyika Mexico.

Mwaka 1977, Umoja wa Mataifa ulitambua rasmi “Siku ya Kimataifa ya Wanawake, inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka”.

Mwaka wa 2010, baada ya majadiliano ya miaka mingi, Baraza Kuu lilipitisha azimio la kuunganisha sehemu na idara zinazohusiana na wanawake za shirika kuwa “Shirika la Umoja wa Mataifa la usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake (UN Women), ambalo linaendelea kushirikiana kwa karibu na kamisjeni ya hali ya wanawake duniani CSW.

4: Kushughulikia dharura zinazoibuka

Mabadiliko ya tabianchi yamefanya maisha ya wanawake wengi kuwa magumu zaidi katika miaka ya karibuni
Jose Manuel Moya
Mabadiliko ya tabianchi yamefanya maisha ya wanawake wengi kuwa magumu zaidi katika miaka ya karibuni

Vikao vya kila mwaka vinashughulikia na kutathmini masuala yanayojitokeza pamoja na maendeleo na mapungufu katika utekelezaji wa jukwaa la utendaji la Beijing.

Nchi wanachama zinakubaliana juu ya hatua zaidi za kuharakisha maendeleo. Tangu mwaka 2018, CSW imeshughulikia changamoto kama vile mabadiliko ya tabianchi, unyanyasaji wa kijinsia, na kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi na katika mikakati ya maendeleo endelevu.

Ikipitisha programu za kazi za miaka mingi ili kutathmini maendeleo na kutoa mapendekezo zaidi ili kuharakisha utekelezaji wa jukwaa la utekelezaji, CSW inatuma mahitimisho yake yaliyokubaliwa kwa ECOSOC kwa ajili ha hatua kuchukuliwa.

Kwa nia ya kuwafikia wanawake wote na kutomwacha mtu yeyeto nyuma, kamisheni pia inachangia katika ufuatiliaji wa ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu ili kuharakisha utekelezaji wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.

5: Kukabiliana na changamoto za karne ya 21

Wanafunzi wasichana katika chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Missouri wakitengeneza roboti
© Missouri S&T/Michael Pierce
Wanafunzi wasichana katika chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Missouri wakitengeneza roboti

Inazidi kudhihirika kwamba ubaguzi unaoendelea, unyanyasaji, na unyanyasaji wa kijinsia ambao wanawake wanakabiliana nao katika ulimwengu wa kimwili unaakisiwa katika ulimwengu wa kidijitali.

Masuala haya ya karne ya 21 yanashughulikiwa katika kikao cha CSW cha 2023, ambacho kinalenga kusawazisha uwanja wa kidijitali ili kushughulikia, miongoni mwa mambo mengine, ufikiaji mdogo wa teknolojia, unyanyasaji usio na uwiano wa mtandaoni, uwakilishi mdogo na upendeleo wa kijinsia katika tasnia ya teknolojia.

Wanachama 45 wa kamisheni hiyo watajadili uvumbuzi na mabadiliko ya kiteknolojia, na elimu katika enzi za kidijitali ili kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote, katika mkutano wake wa kwanza wa ana kwa ana tangu kuzuka kwa janga la COVID-19 mwaka 2020.

Zaidi ya wadau 7,000 walihudhuria kikao cha awali cha ana kwa ana, CSW63, kikijumuisha karibu wajumbe 2,000 wa nchi wanachama, mawaziri 86, na wawakilishi 5,000 kutoka mashirika ya kiraia duniani kote.