Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada sio jibu kwa nchi zenye maendeleo duni

Wachuuzi wakiuza mboga katika soko la Antananarivo, mji mkuu wa Madagascar.
ILO Photo/E. Raboanaly
Wachuuzi wakiuza mboga katika soko la Antananarivo, mji mkuu wa Madagascar.

Misaada sio jibu kwa nchi zenye maendeleo duni

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kuanzia siku ya jumapili tarehe 5 mpaka 9 ya mwezi huu wa Machi, huko Doha nchini Qatar viongozi kutoka kila pembe ya dunia watakutana katika mkutano wa tano wa Umoja wa Mataifa wa nchi zenye maendeleo duni- LDC5 ili kukubaliana na kuangalia namna ya kuzisaidia nchi hizo ziweze kustawi wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na changamoto lukuki.

Kimsingi mkutano huo wa LDC5 unazileta pamoja nchi 46 zenye maendeleo duni zaidi duniani, na kuzikutanisha na nchi nyingine duniani pamoja na wadau wa maendeleo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani kuelekea mkutano huo, Bi. Rabab Fatima, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa nchi zenye maendeleo duni, zisizo na bahari na visiwa vidogo amesema dunia inapaswa kujali masuala ya nchi hizo kwani zimeachwa nyuma zaidi.

Bi. Rabab anasema “Ni muhimu sana kwa dunia nzima kusaidia LDCs kuwa endelevu zaidi na zisiwe tegemezi kwa misaada. Na ni muhimu sana tuwasaidie kupata nafuu, kuwajengea uwezo wa kustahimili, ili waweze kupunguza utegemezi wao kwa dunia nzima.”

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa kwa nchi hizo duni amesema kwa miaka mingi zimekuwa zikitegea misaada zaidi, na imedhihirika misaada sio jibu la maendeleo.

“Bila shaka jibu ni, kujenga uwezo wa LDCs wenyewe kuwa wanazalisha mapato yao wenyewe. Mapato ya ndani, mapato yote. Biashara ni jibu linalofuata. Uwekezaji ni jibu linalofuata. Nchi hizo nyingi zimejaliwa kuwa na wingi wa maliasili pamoja na rasilimali watu, idadi kubwa ya vijana duniani wako katika nchi hizo zenye maendeleo duni.”

Wakati mkutano huo ukianza hapo kesho kutwa Bi. Rabab Fatima ametoa wito kwa nchi zenye maendeleo duni sio tu kuhudhuria mkutano huo bali kushika usukani wa kuendesha mijadala na kushughulikia ahazi zao za kusonga mbele pamoja na kuhakikisha wadau wao na jumuiya ya kimataifa nazo zinashiriki kikamilifu na kuweka ahadi za kuwasaidia kusonga mbele.

Nchi zenye maendeleo duni duniani ni zipi?

Nchi hizo ni Afghanistan; Angola; Bangladesh; Benin; Bhutan; Burkina Faso; Burundi; Kambodia; Jamhuri ya Afrika ya Kati- CAR; Chad; Comoro; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo -DRC; Djibouti; Eritrea; Ethiopia; Gambia; Guinea; Guinea-Bissau.

Nyingine ni Haiti; Kiribati; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Lao; Lesotho; Liberia; Madagascar; Malawi; Mali; Mauritania; Msumbiji; Myanmar; Nepal; Niger; Rwanda; Sao Tome na Principe; Senegal; Sierra Leone; Visiwa vya Solomon; Somalia; Sudan Kusini; Sudan; Timor-Leste; Togo; Tuvalu; Uganda; Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Yemen na Zambia.

Vanuatu ilikuwa nchi ya hivi karibuni kutoka katika orodha ya nchi hizo na iliondolewa mwishoni mwa mwaka 2020.