Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 3.7 walioathirika na tetemeko Syria wanakabiliwa na zahma kubwa: UNICEF

Watoto milioni 3.7 walioathirika na tetemeko Syria wanakabiliwa na zahma kubwa
UN News
Watoto milioni 3.7 walioathirika na tetemeko Syria wanakabiliwa na zahma kubwa

Watoto milioni 3.7 walioathirika na tetemeko Syria wanakabiliwa na zahma kubwa: UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Watoto milioni 3.7 ambao walinusurika na matetemeko ya ardhi ya tarehe 6 Februari mwaka huu katika maeneo yaliyoathirika nchini Syria wanakabiliwa na ongezeko la vitisho kadhaa vya zahma kubwa, ameonya leo Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF, Catherine Russell akihitimisha ziara yake ya siku mbili nchini humo. 

Ameongeza kuwa athari za kihisia na kisaikolojia za matetemeko hayo kwa Watoto ni tishio kubwa la magonjwa ya kuambukiza na yanayotokana na  maji kwa familia zilizolazimika kuhama makwao, na ukosefu wa huduma za msingi kwa familia zilizoachwa hatarini kwa sababu ya takriban miaka 12 ya vita vinaleta hatari inayoendelea na kuzidisha majanga kwa watoto walioathirika. 

Bi. Russell amesema "Watoto wa Syria tayari wamevumilia mshtuko usioelezeka na madhila makubwa .Sasa, matetemeko haya ya ardhini hayakuharibu tu nyumba, shule na mahali kwa watoto kucheza, pia yamebadili kabisa hali ya usalama kwa usalama kwa watoto wengi na familia zilizo hatarini zaidi. " 

Amekutana na kuzungumza na watoto 

Huko Aleppo, Bi. Russell amekutana na watoto katika makazi ya muda ya kujifunza, ambapo zaidi ya watoto 250 wanaoishi katika makao hayo ya pamoja wanaweza kupata elimu, huduma za afya, burudani, na shughuli za kifiziolojia za huduma ya kwanza. 

Katika msikiti mmoja huko Al Masharqa, Russell amezungumza na mama wa watoto wawili anayeitwa Esraa, ambaye mume wake alitoweka wakati wa vita. Sasa analea binti zake wa umri wa miaka 10 na 11 peke yake.  

Esraa ni mmoja wa maelfu ya watu waliopoteza makazi yao kutokana na tetemeko la ardhi.  

Yeye na binti zake  walikaa kwa siku mbili kwenye baridi na mvua kabla ya kupata hifadhi msikitini.  

Sasa wanapata msaada wa pesa taslimu kutoka UNICEF. "Wakati wa tetemeko la pili la ardhi lililotokea wiki moja iliyopita, binti yangu aliogopa sana na kupata kiwewe hadi alizimia," Esraa amemwambia Russell.  

Mmoja wa wasichana hao, Jana, alimwambia Russell alipoulizwa anachotumainia, kwamba “Nataka kitanda na nyumba.” 

Mvulana wa miaka mitano anachunguzwa utapiamlo na mfanyakazi wa timu ya afya ya simu inayoungwa mkono na UNICEF katika kitongoji cha Alsalheen, mji wa Aleppo, kaskazini mwa Syria.
© UNICEF/Muhannad Al-Asadi
Mvulana wa miaka mitano anachunguzwa utapiamlo na mfanyakazi wa timu ya afya ya simu inayoungwa mkono na UNICEF katika kitongoji cha Alsalheen, mji wa Aleppo, kaskazini mwa Syria.

UNICEF inaendelea kutoa msaada 

Russell pia alitembelea kituo cha kusukuma maji kinachoungwa mkono na UNICEF ambacho kinatoa maji salama kwa takriban theluthi mbili ya vitongoji vya Aleppo.  

Huku familia nyingi zaidi sasa zimehama na kuishi katika hali duni katika makazi ya muda, kuendelea kupata maji salama na usafi wa mazingira ni muhimu katika kuzuia milipuko ya magonjwa kama vile vipele, chawa, kipindupindu na kuhara kutokana na maji machafu yasiyo salama ameongeza Bi. Russell. 

Kaskazini-magharibi mwa Syria, UNICEF imewafikia zaidi ya watu 400,000 walioathirika na aidha huduma za lishe au maji, usafi wa mazingira na usafi na vifaa vingine mbalimbali ambavyo ni muhimu.  

Kabla ya tetemeko la ardhi, UNICEF ilikuwa imetuma utangulizi wa vifaa muhimu vya kibinadamu, ambavyo vilianza kufikia watoto na familia katika saa 48 za kwanza baada ya tetemeko la ardhi la kwanza. Hadi sasa, malori ya UNICEF yanayobeba misaada ya kibinadamu kwa zaidi ya watu milioni 1.8 yametumwa kusaidia jamii na watoto kaskazini magharibi mwa Syria. 

Msaada wa dharura pekee hautoshi 

Mkurugenzi huyo wa UNICEF amesema "Haitoshi tu kutoa ahueni ya haraka kwa waathirika, lazima tujitolee kusimama na familia hizi kwa muda mrefu, kuzisaidia kurejesha hali ya utulivu na matumaini. Kwa ufikishaji wa huduma muhimu, kama maji salama, huduma za afya, na usaidizi wa kisaikolojia, tunaweza kusaidia watoto na familia kujikwamua kutoka kwenye jinamizi ambalo wamelivumilia ili waanze kujenga upya maisha yao." 

Nchini Syria, UNICEF inahitaji dola milioni 172.7 ili kutoa msaada wa haraka wa kuokoa maisha kwa watu milioni 5.4, wakiwemo watoto milioni 2.6, walioathiriwa na tetemeko la ardhi.  

Usaidizi utatolewa kwa maeneo yaliyoathiriwa sana kwa kutumia mbinu zote zinazowezekana, ikiwa ni pamoja na ndani ya Syria na kupitia operesheni za mipakani na njia nyingine.  

Ni muhimu kwamba usaidizi uwe rahisi maalum kwa ajili ya UNICEF na washirika wake ili kukabiliana na mahitaji ya msingi na popote ambapo watoto wameathiriwa.