Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ziarani nchini Iraq

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akutana na Waziri Mkuu wa Iraq mjini Baghdad
UNAMI/Sarmad al-Safy
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akutana na Waziri Mkuu wa Iraq mjini Baghdad

Guterres ziarani nchini Iraq

Wahamiaji na Wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amefanya ziara nchini Iraq lengo likiwa ni kusisitiza mshikamano na kuunga mkono juhudu za nchi za kuleta amani ,haki za binadamu na maendeleo endelevu.

Ziara ya mwisho ya Katibu Mkuu Guterres nchini Iraq ilikuwa miaka sita iliyopita, na alipofika Baghdad alipokelewa na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya nje Fued Hussein ambapo walifanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Katika hotuba yake Katibu Mkuu Guterres aliipongeza serikali ya Iraq kwa kuwaruhusu wananchi wa Iraq walio nje ya nchi hiyo kurejea na kusema Umoja wa Mataifa unaunga mkono kikamilifu juhudi zote za kuhakikisha nchi hiyo inakuwa na mustakabali wa amani na ustawi na taasisi zake zinaunganishwa na demokrasia.

Katika mkutano huo pia alizungumzumzia changamoto zinazowakabili wananchi wa nchi hiyo ikiwemo uhaba wa maji na athari za mabadiliko ya tabianchi na kusema “Moyo wangu unavunjika nikiona wakulima wanaacha ardhi zao na mazao ambayo wamekuwa wakilima kwa milenia. Uhaba wa maji nchini Iraq umechangiwa na kupungua kwa uingiaji kutoka nje, usimamizi usio endelevu wa maji, na sasa athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni tishio linalohitaji umakini wa kimataifa.”

Katika kupata suluhu kwenye changamoto hiyo amesema mkutano Umoja wa Mataifa wa Maji utakaofanyika baadae mwezi huu jijini New York, Marekani utajadili mengi kuhusu changamoto ya maji huku akidhibitisha kuelewa ni kwa namna gani suala ya uhakika wa maji ni muhimu kwa nchi hiyo.

Katika ziara yake hiyo, Katibu Mkuu atakutana na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Waziri Mkuu Mohammed Shia’ Al Sudani.

Akiwa katika mji mkuu, Katibu Mkuu pia atakutana na kuwasikiliza wawakilishi wa vikundi vya haki za vijana na wanawake na kufanya mkutano na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Hapo kesho Katibu Mkuu Guterres atatembelea kambi ya Wakimbizi wa Ndani na Kituo cha Urekebishaji kilichoko kaskazini mwa nchi hiyo na kufanya mazungumzo na wakazi wa kituoni hapo.

Kisha ataenda Erbil na kukutana na maafisa wa Serikali ya Mkoa wa Kurdistan.