Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliouawa Laas Canood Somalia wafikia 63 na 363 kujeruhiwa UN yalaani vikali 

Kutoka Maktaba: Isha Dyfan akizungumza na wanahabari mwishoni mwa ziara yake SOmalia mapema mwaka huu.
UN Photo / Fardosa Hussein
Kutoka Maktaba: Isha Dyfan akizungumza na wanahabari mwishoni mwa ziara yake SOmalia mapema mwaka huu.

Waliouawa Laas Canood Somalia wafikia 63 na 363 kujeruhiwa UN yalaani vikali 

Amani na Usalama

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Somalia leo ameelezea kusikitishwa kwake na idadi kubwa ya vifo vya raia nchini humo kufuatia mapigano kati ya vikosi vya usalama vya Somaliland na watu wa koo huko Laas Canood, eneo la Sool mapigano yalioanza tangu mapema Februari. 

Isha Dyfan, mtaalam huyo huru  amesema "Tunasikitishwa na mauaji ya takriban watu 63 na zaidi ya 363 kujeruhiwa," wakati akitoa ripoti za mashambulizi ya kiholela au ya makusudi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, na kuongeza kwamba “mashambulizi haya hayakubaliki kabisa na yanakiuka moja kwa moja sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kibinadamu.” 

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa ameendelea kusema "Wale waliohusika lazima wawajibishwe," akitoa wito kwa mamlaka kuhakikisha uchunguzi usio na upendeleo, unaofaa na huru kuhusu vifo na majeruhi unafanyika. 

Pande zote lazima ziheshimu na kutimiza wajibu wao 

"Ninatoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mapigano kuheshimu kikamilifu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, hasa kuhusu ulinzi wa raia," Amesema Dyfan. 

Mtaalamu huyo ameonya kwamba mapigano yanayoendelea huko Laas Canood yatazidisha hali mbaya ya kibinadamu ambayo tayari ipo katika eneo pana la Sool, na kote nchini. 

Kulingana na ripoti ya ujumbe wa tathmini ya mashirika mbalimbali uliofanywa na washirika wa kibinadamu, mapigano huko Laas Canood, yaliyoanza tarehe 6 Februari, yamewakosesha makazi zaidi ya watu 185,000  sawa na asilimia 89 ya watu wote na waathirika wakubwa miongoni mwao ni wanawake na watoto. 

"Ningependa kusisitiza wito uliotolewa na washirika wa kimataifa wa kutaka fursa ya ufikiaji wa waathirika usiozuiliwa ili kushughulikia kwa haraka mahitaji ya wale waliolazimika kukimbia na kuathiriwa na ghasia," amesisitiza Dyfan. 

Mtaalamu huyo amezitaka pande zote kukubaliana kusitishwa mara moja kwa uhasama na kutatua mizozo yao kwa njia ya mazungumzo. "Kutokufanya hivyo itakuwa sawa na kunyima haki kupata haki na kuendeleza kutojali na ukwepaji sheria".