Uharibifu wa makusudi wa utamaduni wa Ukraine lazima ukome: Wataalam wa haki za binadamu.

Takriban mwaka mmoja baada ya vita kamili kuzuka nchini Ukraine na huku kukiwa na mashambulizi mapya ya makombora yanayolenga mji wa Mashariki wa Kharkiv siku ya Jumatano wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kukomeshwa mara moja uharibifu wa makusudi wa hazina za kitamaduni za nchi hiyo unaofanywa na vikosi vya Urusi.
Kulingana na wafanyikazi wa misaada ya kibinadamu, takriban watu sita wameuawa siku ya Jumanne baada ya makombora ya Urusi kugonga kwenye barabara yenye shughuli nyingi katika mji wa Kherson.
Wengi wa waathirika walikuwa wamesimama kwenye kituo cha basi, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York siku.
Wataalamu hao huru wa haki za binadamu walioteuliwa na Umoja wa Mataifa pia wameonyesha wasiwasi wao kwa "kuendelea kudharauliwa kwa historia na utambulisho wa watu wa Ukraine kama uhalali wa vita na chuki".
Wataalamu hao, ambao wanaripoti kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kama wawakilishi maalum, wametoa ripoti kwamba maeneo muhimu ya kitamaduni nchini Ukraine yanalengwa kwa makusudi, wakati yanapaswa kulindwa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, hasa mkataba wa The Hague wa 1954 wa ulinzi wa mali za kitamaduni katika wakati wa tukio la migogoro ya silaha.
Maeneo muhimu ya kitamaduni ya Ukraine ambayo yameguswa ni pamoja na majengo "yaliyowekwa alama kama makazi ya wakaazi, yakiwemo ya watoto, na vile vile makumbusho, maktaba na makanisa. Mashambulizi ya kiholela na yasiyo na uwiano kwenye maeneo yenye wakazi wengi, na uharibifu uliosababishwa kwa miundombinu ya kiraia katika mchakato huo, ni wa kiwango cha juu kiasi cha kudhihirisha ni kampeni ya makusudi ya uharibifu," wamesema wataalam hao katika taarifa yao.
Zaidi ya maeneo 240 ya urithi wa Ukraine yanakadiriwa kuharibiwa tangu uvamizi wa Urusi tarehe 24 Februari mwaka jana, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la utamaduni, elimu, sayansi na utmaraduni UNESCO.
Lakini idadi halisi ya mashambulizi inaweza kuwa zaidi ya 1,000, wataalam wa haki za binadamu wamesema.
"Hazina za fasihi za Kiukraine, makumbusho, na kumbukumbu za kihistoria zinaharibiwa, na kuna simulizi iliyoenea ya unyanyasaji na udhalilishaji wa utamaduni na utambulisho wa Kiukraine unaokuzwa na maafisa wa Urusi, pamoja na wito wa ukandamizaji wa kiitikadi na udhibiti mkali katika siasa, utamaduni na nyanja za elimu. Hebu tuwe wazi watu wa Ukraine wana haki ya utambulisho wao. Hakuna mtu anayeweza kukiuka haki hii." Limeongeza shirika hilo
Katika eneo la Mashariki mwa Ukraine na Crimea, yanayodhibitiwa na Urusi tangu Machi 2014, wataalamu hao wamesisitiza kwamba jitihada zimekuwa zikifanywa “kufuta utamaduni, historia na lugha ya wenyeji katika taasisi za kitamaduni na za elimu.”
Badala yake, jamii zilikabiliwa na kuziona tamaduni zao zikibadilishwa na lugha ya Kirusi na historia na utamaduni wa Kirusi na Soviet.
"Vitabu vya historia ya Ukraine na fasihi zinazochukuliwa kuwa za itikadi kali vimekamatwa kutoka kwenye maktaba za umma katika miji na vitongoji katika eneo linalokaliwa la Luhansk, Donetsk, Chernihiv na Sumy Oblasts na kuharibiwa na mamlaka inayokalia maeneo hayo" wwameripoti wataalam hao na kuongeza kuwa "Hali hiyo limeripotiwa pia kuhusu vitabu vya historia vya shule katika miji fulani."
Wawakilishi maalum na wataalam huru wa haki za binadamu wanateuliwa na Baraza la Haki za Kibinadamu lenye makao yake makuu jijini Geneva Uswis ili kuchunguza na kutoa ripoti kuhusu mada maalum ya haki za binadamu au hali ya haki za binadamu katika nchi fulani.
Nafasi hizo ni za heshima na wataalam si wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wala hawalipwi kutokana na kazi zao.