Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malengo yetu yako palepale kukomesha machafuko na ukaliaji wa ardhi ya Palestina: Guterres

Shule ambayo watoto wa Kipalestina wanahudhuria huko Jerusalem Mashariki.
Reem Arouri
Shule ambayo watoto wa Kipalestina wanahudhuria huko Jerusalem Mashariki.

Malengo yetu yako palepale kukomesha machafuko na ukaliaji wa ardhi ya Palestina: Guterres

Amani na Usalama

"Hadhi ya Jerusalem haiwezi kubadilishwa kwa vitendo vya upande mmoja. Malengo yetu yanabaki palepale kukomesha uvamizi huo na kufikia suluhu ya kuwa na serikali mbili ya Israel na Palestina," huu ni msimamo wa Umoja wa Mataifa, ambao Katibu Mkuu wake amesisitiza leo, akionya dhidi ya kuongezeka kwa mvutano na machafuko, na kusisitiza kujitolea kwake kufanya kazi kwa ajili ya haki ya amani. 

Katika hotuba yake kwa kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki zisizoweza kuepukika za watu wa Palestina, António Guterres amezungumzia hali tete katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, kuongezeka kwa mivutano, kushika kasi kwa mzunguko wa machafuko na kukwama kwa mchakato wa amani. 

Ameelezea wasiwasi wake kuhusu habari iliyopokelewa leo ya operesheni iliyofanywa na vikosi vya usalama vya Israel na mapigano yaliyofuata, ambayo yamesababisha mauaji ya Wapalestina 10 na kujeruhi wengine zaidi ya 80. 

Katibu Mkuu ameongeza kuwa "Mwaka wa 2022 ulikuwa mbaya zaidi kwa Wapalestina tangu ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu ilipoanza mwaka 2005 kufuatilia kwa utaratibu idadi ya vifo. Katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka huu, ghasia zinapamba moto bila kukoma. Katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Gaza, kukata tamaa kumekithiri na hii inaendelea kuchochea hasira na taharuki."  

Guterres amesisitiza kwamba hadhi ya Jerusalem haiwezi kubadilishwa kwa hatua za upande mmoja, na kuhimiza haja ya kuhifadji maeneo ya watu, sifa ya kihistoria ya mji huo, na hadhi ya sasa ya maeneo matakatifu ndani yake, kulingana na jukumu maalum la ufalme wa Hashemite wa Jordan. 

Makazi ya Walowezi ni kikwazo na ugaidi hautakiwi 

Katibu mkuu ameendelea kusema kuwa kila suluhu mpya ni kikwazo kingine katika njia ya amani.  

"Shughuli zote za makazi mapya ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa na lazima zikome. Wakati huo huo, uchochezi wa ghasia ni mwisho. Hakuna kinachohalalisha ugaidi, ambao unapaswa kukataliwa na watu wote." 

Antonio Guterres amesema vipaumbele vya haraka zaidi kwa sasa lazima viwe kuzuia kuongezeka zaidi kwa machafuko, kupunguza hali ya wasiwasi, na kurejesha usalama. 

Hatua za adhabu 

Guterres ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu hatua za hivi karibuni za adhabu zilizochukuliwa na Israel dhidi ya mamlaka ya ndani ya Palestina baada ya azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la kutafuta ushauri wa mahakama ya kimataifa kuhusu uvamizi huo.  

"Hatua hizi zinahatarisha kuyumbisha mamlaka ya Palestina wakati inapambana na mzozo mgumu wa kifedha ambao unadhoofisha uwezo wake wa kutoa huduma kwa watu wake," amesema. 

Moja ya majengo ambayo UNRWA ilijenga upya katika kambi ya Jajalia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Ziad Taleb
Moja ya majengo ambayo UNRWA ilijenga upya katika kambi ya Jajalia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

UNRWA ni njia ya kuokoa maisha 

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), ambalo ni mhimili mwingine wa maisha kwa Wapalestina, linakabiliwa na kazi ngumu ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kwa kuzingatia ufadhili hafifu, amesema Katibu Mkuu. 

Amebainisha kuwa shirika hilo, hata hivyo, ulisalia imara, kwa utendakazi wa hali ya juu na wa gharama nafuu.  

Amewataka wafadhili wote kutimiza ahadi zao na kuhakikisha kuwa UNRWA inapata msaada endelevu na unaotabirika ambao unahitajika ili kutimiza wajibu wake muhimu. 

Katika muktadha huo, Guterres amesisitiza umuhimu wa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu kwenda na kutoka Ukanda wa Gaza.  

Amerejea upya wito wake wa kuchukua hatua kuondoa vikwazo, kulingana na azimio la Baraza la Usalama nambari 1860 la mwaka 2009. 

Suluhu ya mataifa mawili 

Lengo la malengo ya Umoja wa Mataifa bado ni kukomesha uvamizi na ukaliwaji wa maeneo ya Wapalestina na kufikia suluhu ya mataifa mawili, kama Katibu Mkuu alivyosema, lakini akasema kwamba mwelekeo uliopo katika ardhi unamaanisha kuwa muda unatutupa mkono kadiri siku zinavyosonga mbele bila mazungumzo ya maana ya kisiasa, malengo haya yanakuwa mbali zaidi kufikiwa . 

Katibu Mkuu amesisitiza haja ya washirika wa kikanda na kimataifa kufanya kazi kwa pamoja, kwa uvumilivu na udharura zaidi, ili kuwasaidia Wapalestina na Waisraeli kurejesha upeo wa kuaminika wa kisiasa. 

Amesema, mifumo ya suluhu iko wazi na imefafanuliwa katika maazimio ya Baraza la Usalama, sheria za kimataifa na makubaliano ya pande mbili, na kinachotakiwa kwa sasa ni dhamira ya kijasiri ya kisiasa ya kuchukua maamuzi magumu kwa ajili ya amani. 

Katibu Mkuu amehitimisha hotuba yake kwa kuthibitisha ahadi yake ya kuendelea kufanya kazi ili kuunga mkono kufikiwa kwa lengo la amani ya haki, pana na ya kudumu ambayo inamaliza ukaliwaji na kufikia suluhisho la serikali mbili, Israeli na Palestina huru wakishi bega kwa bega ndani ya mipaka salama, na Jerusalem kama mji mkuu wao.