Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malipo ya deni la nje ni asilimia 20 zaidi ya mapato ya ndani, yasema UNDP na kutaka hatua zichukuliwe

Wachuuzi wakiuza mboga katika soko la Antananarivo, mji mkuu wa Madagascar.
ILO Photo/E. Raboanaly
Wachuuzi wakiuza mboga katika soko la Antananarivo, mji mkuu wa Madagascar.

Malipo ya deni la nje ni asilimia 20 zaidi ya mapato ya ndani, yasema UNDP na kutaka hatua zichukuliwe

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchi zinazoendelea zinaweza kusalia na mamia ya mabilioni yad ola kwenye akiba zao iwapo dunia itaahidi kufanyia marekebisho mfumo wa sasa wa madeni na kwa siku za usoni wigo wa kupata fedha bila masharti magumu uongezwe. 

Tamko hilo limo kwenye chapisho jipya lililotolewa leo huko Paris nchini Ufaransa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP kuelekea mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu wa kundi la nchi zenye uchumi bora duniani, G20 unaoanza wiki hii huko Bangalore, India. 

Likipatiwa jina Kujenga Hatua Kutoka katika Janga, chapisho hilo linaainisha nchi 52 za kipato cha chini na kati ambazo zimetwama kwenye madeni au ziko hatarini kutwama kwenye madeni, nchi hizo zikiwa na asilimia 40 ya watu wote maskini wa kupindukia au hohehahe duniani. 

Chapisho linaonesha ni kwa vipi kupunguzwa kwa asilimia 30 ya ulipaji wa deni la nje la mwaka 2021 kunawea kusaidia malipo yad ola bilioni 148 za madeni katika kipindi cha miaka 8 ijayo. 

“Viongozi duniani wanaombwa kuchukua hatua kusaidia kuepusha nchi maskini zisitumbukie kwenye madhara ya sasa ya majanga yaliyofungamana ilhali pia wahakikishe kuwa rasilimali za fedha ziko ili kufanikisha mpito wenye uwiano na usawa kwa nchi zote,” limesema chapisho hilo. 

Mipango hiyo ya Kuchukua Hatua kutoka kwenye Janga na ambayo tayari inajadiliwa katika kundi hilo, G20 ni pamoja na marekebisho ya benki za kimataifa za maendeleo, marekebisho ya mfumo wa ulipaji madeni na uwezeshaji wa nchi kuwa na uwezo wa kifedha. 

Akinukuliwa katika taarifa hiyo kutoka Paris, Kiongozi Mkuu wa UNDP Achim Steiner anasema “huku  mwanya mkubwa kati ya nchi tajiri na maskini ukiendelea kupanuka kwa kasi kubwa, tunahitaji kuondoka kwenye maneno na tuanze kutekeleza kwa vitendo.” 

Deni la nje ni kubwa kwa asilimia 20 kuliko mapato yote ya ndani 

Leo hii, serikali za nchi 25 zinazoendelea zinatakiwa kulima deni la nje ambalo ni asilmia 20 zaidi ya jumla ya mapato ya ndani, ikiwa ni nchi nyingi zaidi kuwa na kiwango hicho katika kipindi cha miaka 20. 

Bwana Steiner anasema zikiwa zimezingirwa na ongezeko la mzigo wa madeni, nchi hizo zinashindwa kuelekeza fedha kwenye huduma muhimu kama vile hatua kwa tabianchi ni kujenga mnepo kwa janga la tabianchi. 

“Cha kusikitisha zaidi, nchi zenye mzigo mkubwa zaidi wa madeni na zisizo na uwezo wa kupata ufadhili, ndio zinakumbwa na majanga lukuki- zimeathiriwa zaidi vibaya kiuchumi na janga la coronavirus">COVID-19, umaskini na dharura ya tabianchi,” amesema Mkuu huyo wa UNDP. 

Chapisho linatoa mapendekezo ya dharura ya kisera ili kubadili mwelekeo wa sasa wa janga la madeni ikiwemo marekebisho ya mfumo wa utoaji wa madeni na kuongeza kipindi cha malipo. 

Halikadhalika kupunguza gharama za ukopaji wa fedha kwa ajili ya uwekezaji kwenye mipango iliyomo katika Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi na vile vile Ajenda 2030 au Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.