Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 1.2 zasakwa kusaidia wakimbizi wa Sudan Kusini na wenyeji wao

Wanawake wawili wa Sudan Kusini waliotembea kwa siku mbili mfululizo wakiwa wameketi, wakiwa wamechoka, katika kituo cha njia ya Biringi katika Mkoa wa Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNHCR/Carlinda Lopes
Wanawake wawili wa Sudan Kusini waliotembea kwa siku mbili mfululizo wakiwa wameketi, wakiwa wamechoka, katika kituo cha njia ya Biringi katika Mkoa wa Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Dola bilioni 1.2 zasakwa kusaidia wakimbizi wa Sudan Kusini na wenyeji wao

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR pamoja na mashirika 108 ya utoaji wa misaada ya kiutu wametoa ombi la dola bilioni 1.3 ili kusaidia wakimbizi kutoka Sudan Kusini na jamii zinazowahifadhi nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda.

Vichocheo havionekani kutoweka 

Msemaji wa UNHCR jijini Geneva, Uswisi Shabia Mantoo amewaeleza waandishi wa habari hii leo ya kwamba ombi hilo la fedha linatolewa wakati mwelekeo wa uchumi katika ukanda mzima wa eneo hilo ukiwa na kizawa wakati madhara ya muda mrefu ya janga la coronavirus">COVID-19 yakizidi kuibuka bila kusahau changamoto zitokanazo na vita ya Ukraine na ongezeko la bei za vyakula na ukosefu wa ajira.  

“Nchi zilizokaribisha kwa ukarimu wakimbizi kutoka Sudan Kusini zinabeba mzigo mkubwa wa janga la mzozo wakati ambapo ufadhili nao unasuasua, ukame wa muda mrefu na uhaba mkubwa wa chakula ikiwemo makato ya mgao wa chakula kwa wakimbizi,” amesema Bi. Mantoo. 

Wakati uzinduzi wa ombi hilo, UNHCR imesihi jamii ya kimataifa iongeze usaidizi wake kwa wakimbizi ambao hawawezi kurejea nyumbani kutokana na hali ya usalama kuwa tete pamoja na kuweko kwa madhara ya janga la tabianchi. 

Katika jimbo la Unity nchini Sudan Kusini, mji mkuu wa Bentiu, umekuwa kisiwa kilichozungukwa na maji ya mafuriko.
© UNHCR/Charlotte Hallqvist
Katika jimbo la Unity nchini Sudan Kusini, mji mkuu wa Bentiu, umekuwa kisiwa kilichozungukwa na maji ya mafuriko.

Mafuriko yametwamisha theluthi moja ya nchi 

Miaka minne ya mafuriko yasiyokwisha yametwamisha theluthi mbili ya Sudan Kusini, yakiharibu makumi ya maelfu ya makazi ya watu, mashamba na mifugo. 

Bi. Mantoo amesema usaidizi huu utakuwa muhimu ili kukidhi mahitaji ya haraka ya wakimbizi kwenye nchi walimosaka hifadhi, mahitaji kama vile makazi, elimu, afya na msaada wa chakula. 

“Wanawake na watoto wakiwa ni asilimia 80 ya wakimbizi wa Sudan Kusini kwenye ukanda huu, ufadhili wa miradi ya kuzuia na kuchukua hatua kuzuia ukatili wa kijinsia lazima upatiwe kipaumbele.” 

Ombi hilo pia linalenga kupatia wakimbizi msaada wa fedha taslimu na mipango mingine ya kujenga mnepo kama vile kupata fedha na mafunzo ya kusaidia wakimbizi na jamii za wenyeji kuwa na miradi ya kujipatia kipato na kukimu mahitaji yao waishi kwa utu. 

Wakimbizi wa Sudan Kusini wanaoishi katika makazi ya wakimbizi katika mkoa wa Haut Uele, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNHCR/Jean-Jacques Soha
Wakimbizi wa Sudan Kusini wanaoishi katika makazi ya wakimbizi katika mkoa wa Haut Uele, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Serikali zitawezeshwa kuimarisha huduma za msingi 

Kwa upande wake, serikali wenyeji zitasaidia pia kuimarisha maeneo ya hifadhi ya wasaka hifadhi na kulinga haki za wakimbizi na wasaka hifadhi na wakati huo huo kuchagiza majawabu ya kudumu kwa makundi hayo. 

Mathalani kuboresha huduma za usajili kwa wakimbizi na wasaka hifadhi, utunzaji wa nyaraka na ujumuishaji wa wakimbizi katika mifumo ya kitaifa ya hifadhi ya jamii na vile vile kuwawezesha kupata huduma muhimu kwa wakimbizi. 

Hatua za kuongeza matumizi ya nishati safi na endelevu kwa jamii zinazohifadhi wakimbizi zitaimarishwa pia halikadhalika kupunguza madhara kwa mazingira. 

Ikiwa tu ni theluthi moja ya mahitaji ya fedha kwa Sudan Kusini ndio ilipatikana mwaka jana pekee, nchi tano ambazo ni kimbilio kwa wasaka hifadhi Afrika, DRC, Ethiopia, Sudan, Ethiopia na Uganda zilipokea kiwango kidogo cha fedha, 

“Tunatoa wito kwa wafadhili kuonesha upendo na kutekeleza ahazi zao kusaidia wakimbizi wa Sudan Kusini na wengineo waliofurushwa makwao duniani kote. Fedha kupatikana kwa wakati ni jambo muhimu ili kuhakikisha msaada na ulinzi unapatikana kwa wale walio hatarini zaidi,” ametamatisha Bi. Mantoo.