Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa mashirika ya Umoja wa Mataifa watembelea walioathirika na tetemeko nchini Syria

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasafirisha misaada kibinadamu kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi kutoka Türkiye kwenda kaskazini magharibi mwa Syria.
© UNOCHA/Madevi Sun Suon
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasafirisha misaada kibinadamu kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi kutoka Türkiye kwenda kaskazini magharibi mwa Syria.

Ujumbe wa mashirika ya Umoja wa Mataifa watembelea walioathirika na tetemeko nchini Syria

Msaada wa Kibinadamu

Ujumbe wa mashirika saba ya Umoja wa Mataifa umetembelea hospitali na kliniki zinazoungwa mkono na shirika lisilo la kiserikali la Misaada na Maendeleo la Syria au SRD, Kaskazini Magharibi mwa Syria na kujionea athari za tetemeko la Ardhi lililoikumba nchi hiyo wiki mbili zilizopita pamoja na kujionea usambazaji wa misaada iliyotolewa na Umoja wa Mataifa.

Lengo la ziara hiyo iloyohusisha mashirika saba ya Umoja wa Mataifa ni kufanya tathmini ya mahitaji na kusambaza misaada.

Mashirika ya UN katika ziara hiyo maalum ni lile la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu -OCHA, la Uhamiaji IOM, la Idadi ya watu duniani na Afya ya Uzazi- UNFPA, la Kuhudumia Watoto UNICEF, la Afya duniani -WHO, la Kuhudumia Wakimbizi -UNHCR pamoja na Idara ya Usalama na ulinzi ya Umoja wa Mataifa UNDSS.

Wakiwa Kaskazini – Magharibi mwa Syria ujumbe huo ulizungumza na wananchi walionusurika kwenye tetemeko. Akijitambulisha kwa jina moja tu, Muhammed aliwaeleza hali ilivyokuwa.

"Watoto wangu walikuwa wamelala kwenye ghorofa ya pili. Nilihisi mtikisiko na harufu ya vumbi. Nilikuwa na uhakika kwamba gorofa ya juu ingetuangukia, kisha nikashukuru nilipoona watoto wangu wakikimbia. Jengo lililokuwa mbele yetu liliporomoka. Tulitoka nje na kulikuwa na mvua na radi. Ilikuwa baridi. Umeme ulikatika.”

Kisha wakatembelea hospitali na zahanati zinazoungwa mkono shirika lisilo la kiserikali la SRD. Wakiwa katika hospital ya Al-Refah, Daktari Ahmad Jumaa aliwaeleza hali ilivyo.

“Tangu mwanzo wa tetemeko la ardhi, tulijaribu kuwapokea watu wote waliojeruhiwa. Ndiyo hospitali pekee inayofanya kazi hapa Jandairis. Tulijaribu kusaidia kila mtu kwa uwezo wetu mdogo na mpaka sasa tunaendelea kujaribu kusaidia majeruhi wote wanakuja hapa wakiwa wamefungwa bandeji na majeraha yaliyoshonwa.”

Mbali na kutembelea hospitali nyingine ya Muhammad Wassim Maazi, wajumbe wa ziara hiyo walitembelea bohari inayofanya usambazaji wa misaada iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani WHO, misaada ambayo inajumuisha vifaa vya dharura vya majeraha na upasuaji pamoja na dawa mbalimbali za kusaidia waaathirika wa tetemeko.