Bima ya tabianchi kulipwa kwa waathirika nchini Burkina Faso, Mali na Gambia- WFP
Bima ya tabianchi kulipwa kwa waathirika nchini Burkina Faso, Mali na Gambia- WFP
Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP limepata dola milioni 15.4 zitakazotumika kuwalipa bima watu 490,000 katika nchi za Burkina Faso, Gambia na Mali walioathiriwa na ukame mwaka 2022.
Taarifa ya WFP iliyotolewa jijini Roma, Italia hii leo imesema fedha hizo zitalipwa kutoka shirika la African Risk Capacity, ARC kuanzia mwezi ujao wa Machi hadi Mei mwaka huu wa 2023, ili hatimaye wanufaika waweze kununua chakula au wawe na kipato na hivyo kuepuka kuuza mali zao za uzalishaji.
ARC ni shirika la Muungano wa Afrika sasa linashirikiana na WFP
ARC, ni shirika mahsusi la Muungano wa Afrika linalosaidia nchi wanachama kuhimili tabianchi na madhara ya majanga.
“Jami nchini Mali zina mchango mdogo sana kwenye janga la tabianchi duniani, lakini ndio zinatumbukizwa kwenye janga la chakula,” amesema Eric Perdison, Mwakilishi Mkazi wa WFP nchini Mali akiongeza “hizi fedha zitawezesha WFP kufikia mamia ya maelfu ya watu wasio na uhakika wa chakula na walioathiriwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Tutawapatia fedha taslimu na msaada wa chakula.”
Wakulima huko Afrika Magharibi walipata hasara na uharibifu kwenye mazao yao na njia za za kujipatia kipato kutokana na ukame mkali uliokumba eneo hilo wakati wa msimu wa kilimo mwaka 2022.
WFP inasema hali hiyo imekuwa na athari hasi kwenye upatikanaji wa chakula kwenye ukanda huo wa Afrika huku bei za vyakula zikiongezeka kila uchao.
Faida za bima ya tabianchi
Shirika hilo linasema bima ya tabianchi itawezesha jamii kujikwamua kutoka katika hasara na uharibifu na hivyo kuepusha wasitumbukie kwenye baa la njaa.
Mgao wa dola hizo milioni 15.4 ni kama ifuatavyo: WFP itapatia Burkina Faso milioni 7.2, Gambia dola milioni 187,600 na Mali dola milioni 8.
Msaada utahusisha pia usaidizi wa lishe kwa watoto wenye umri wa kati ya miezi 6 hadi 23, bila kusahau wajawazito na wanawake wanaonyonyesha watoto.
“Tunashukuru msaada wa Ujerumani, Marekani na Uingereza ambao umewezesha WFP kununua sera za bima ambazo zinatuwezesha kufanya kazi na serikali za mitaa ili kupunguza hasara na uharibifu uliosababishwa na madhara ya tabianchi,” amesema Mathieu Dubreuil, mkuu wa dawati la bima ya athari za tabianchi katika WFP.
Mpango huu wa bima kwa tabianchi upanuliwe
Ametaka mpango kama huo upatiwe msisitizo zaidi ili kulinda watu wengi zaidi walio hatarini kuathiriwa na janga la tabianchi.
Tangu mwaka 2019, WFP kupitia ARC imefikia watu milioni 4.8 katika nchi 6 za Afrika kwa kuwapatia malipo ya bima.
Hadi leo hii, WFP imepokea malipo yenye thamani ya dola milioni 25.4 kwa nchi 5 ambazo zinatumika kulipwa fedha taslimu, msaada wa chakula na na kulinda mali za zaidi ya watu 790,000.
Aissé, ambaye ni mjane kutoka Mali alipokea fedha kutoka mpango huo kufuatia ukame wa mwaka 2021 na anasema “fedha taslimu niliyopata wakati nikiwa napitia magumu nilinunua chakula. Naishi peke yangu na watoto wangu na tunahitaij chakula. Kwa hiyo nilinunua mchele na mtama.”