Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi waliorejea nyumbani Burundi wasonga mbele na maisha

Filippo Grandi, Kamishna Mkuu UNHCR , akimkabidhi mwanamke mkimbizi aliyerejea katika kituo cha usafiri huko Cibitoke, Burundi, zinki iliyotengenezwa kwa bati.
© UNHCR/Samuel Otieno Burundi. Grandi wa UNHCR asifu maendeleo katika kurejea kwa wakimbizi Burundi, ahimiza msaada zaidi

Wakimbizi waliorejea nyumbani Burundi wasonga mbele na maisha

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linaendelea na hatua zake za kuhakikisha wakimbizi waliorejea nyumbani wanaishi maisha ya utu na ustawi, ambapo pamoja na kuwapatia wakimbizi hao huduma bora pia linazidi kuomba wahisani waoneshe ukarimu zaidi.  

Video ya UNHCR inatupeleka mkoa wa Cibitoke, ambako huko wakimbizi waliorejea tayari wameanza kuishi na kujitafutia kipato. 

Anaoenakana Odette Bikorimana, akitembea kuelekea nyumbani kwake, nyumba imeezekwa kwa nyasi na paa limedhoofika. 

“Paa la nyumba yangu ninamoishi sasa ni la nyasi,” anasema Odette akiongeza kuwa mvua ikinyesha linavuja, Jirani yangu ambaye ndiye aliniuzia hii nyumba, hivi sasa anahifadhi watoto wangu kwa sababu yangu inavuja na ni ndogo. Nina watoto watano. Jumla tuko sita kwenye familia yetu.” 

Odette anajipatia kipato kwa kuuza mkaa na baada ya kupata mteja anafunguka zaidi madhila yanayomsibu kama vile, “ni vigumu sana kupata mkaa kwa sababu unatoka mbali milimani. Wafanyabiashara ndio wanatuletea na gunia moja ni dola 20. Nikipata wateja wengi, fedha ninayopata natumia kununua chakula sokoni, kama vile viazi vitamu. Siwezi kusema kwamba biashara hii hainisaidii, la hasha! Faida ndogo nipatayo natumia kusaidia familia yangu.” 

Wafanyakazi wa UNHCR na Filippo Grandi wanakutana na waomba hifadhi wa Kongo katika kituo cha mapokezi huko Cibitoke, Burundi.
© UNHCR/Samuel Otieno Burundi. Grandi wa UNHCR asifu maendeleo katika kurejea kwa wakimbizi Burundi, ahimiza msaada zaidi

Mgeni njoo mwenyeji apone 

Punde Odette anapata ugeni ukiongozwa na Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi akiambatana na viongozi wengine wa serikali ya Burundi na mwakilishi wa Muungano wa Ulaya, EU.   

Baada ya mazungumzo kati ya ugeni huo na Odette, Bwana Grandi anasema“ni muhimu sana katika mazingira ya wakimbizi sio tu kuwapatia msaada wanapokimbia bali pia kusaidia wanaporejea nyumbani. Kurejea nyumbani kwa hiari, salama na kwa utu ndio mpango bora zaidi kwa mkimbizi yeyote. Lakini inahitaji msaada, msaada wa jamii ya kimataifa.” 

Amesema UNHCR inahitaji msaada kwa sababu wao wanatoa msaada kidogo wa fedha na kwamba “WFP inatoa mgao wa chakula kwa miezi michache hasa kwa walio hatarini. Mathalani kwa familia hii ya Odette itapokea msaada wa vifaa waweze kukarabati paa.” 

Halikadhalika amesema mambo mawili muhimu ni mosi, watu wajumuishwe kwenye huduma za kitaifa na miradi ya maendeleo ya kitaifa na pili ni kwa wadau wa maendeleo kupeleka rasilimali kwani watu wanahitaji misaada ya kimkakati na ya muda mrefu kuepusha mvutano wa rasilimali kati ya waliorejea na wenyeji.