Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto ya homa ya uti wa mgongo inaendelea Niger: WHO

Wahudumu wa afya katika harakati za kukabiliana na homa ya uti wa mgongo.
WHO Africa
Wahudumu wa afya katika harakati za kukabiliana na homa ya uti wa mgongo.

Changamoto ya homa ya uti wa mgongo inaendelea Niger: WHO

Afya

Homa ya uti wa mgongo au meningitis imeendelea kuiathiri Niger kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO ambapo hadi kufikia tarehe 27 Januari 2023 kulikuwa na wagonjwa 559 huku 111 wakithibitishwa na vipimo vya maabara na idadi ya waliokufa kufa ni 18. 

Eneo liliyoathirika zaidi kutokana na taarifa ya WHO ni jimbo la Zinder lililoko Kusini Mashariki mwa Niger na hivi sasa kampeni kubwa ya chanjo dhidi ya homa hiyo inaendelea. 

Niger kwa sehemu kubwa iko katika ukanda wa uti wa mgongo wa Afrika na milipuko ya msimu hujirudia kila mwaka.  

Lakini, mlipuko unaoendelea unaonyesha idadi iliyoongezeka ya wagonjwa na kiwango cha ukuaji ikilinganishwa na misimu iliyopita. 

WHO inasema mkoa wa Zinder unashiriki mpaka wa kimataifa na jimbo la Jigawa nchini Nigeria ambapo mlipuko wa homa ya uti wa mgongo NmC pia unaendelea, na hivyo kuthibitisha hatari ya kuenea kimataifa.  

Zaidi ya hayo, kutokea kwa wakati mmoja kwa magonjwa mengine ya mlipuko, ukosefu wa usalama na kuhamishwa kwa idadi ya watu, yote katika muktadha wa mgogoro wa muda mrefu wa kibinadamu, kuna uwezekano wa kuchangia kuenea kwa mlipuko katika nchi nyingine za eneo ndogo la Afrika Magharibi. 

WHO inatathmini hatari inayoletwa na mlipuko wa sasa wa homa ya uti wa mgongo nchini Niger kuwa ya juu katika ngazi ya kitaifa, ya wastani katika ngazi ya kanda, na ya chini katika ngazi ya kimataifa. 

Hali halisi Niger 

Ikiwa iko katika ukanda wa uti wa mgongo wa Afrika, Niger imeathiriwa na milipuko kadhaa ya homa ya uti wa mgongo na kusababisha wagonjwa 20,789 na vifo 1369 sawa na asilimia  6.6 vilivyoripotiwa tangu 2015. 

Kuanzia tarehe 1 Novemba 2022 hadi 27 Januari 2023, jumla ya kesi 559 za homa ya uti wa mgongo zimeripotiwa ambapo 111 zimethibitishwa kimaabara, zikijumuisha vifo 18 vimeripotiwa kutoka eneo la Zinder, Kusini Mashariki mwa Niger, ikilinganishwa na kesi 231 zilizoripotiwa kuanzia tarehe 1 Novemba 2021 hadi 31 Januari 2022. 

Mlipuko wa mwisho wa homa ya uti wa mgongo katika eneo la Zinder, ulitokea katika msimu wa mwaka 2021/2022, na jumla ya wagonjwa 372, ikiwa ni pamoja na vifo 12 viliripotiwa. 

Mwitikio wa afya ya umma 

• Kamati ya kiufundi imeanzishwa katika eneo la Zinder ili kuratibu mwitikio wa janga hili.  

Mpango wa kukabiliana na homa ya uti wa mgongo umekamilika na kutekelezwa. Timu ya kimataifa kutoka WHO na washirika wengine ikiwa ni pamoja na madaktari  wasio na mipaka MSF na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF imetumwa kusaidia hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.. 

• Shughuli za mfumo wa ufuatiliaji zimeimarishwa katika mkoa wa Zinder hasa katika wilaya ya Dungass, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa wagonjwa.  

Shughuli za kimaabara zinaendelea, ikijumuisha ukusanyaji wa sampuli na uthibitisho kutoka kwa visa vinavyoshukiwa vya uti wa mgongo. 

• Shughuli za usimamizi wa wagonjwa zimeimarishwa, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ceftriaxone ya viuavijasumu au antibiotocs, kutengwa kwa kesi, kupeleka wahudumu wa afya kwa ajili ya usimamizi wa kesi, usambazaji wa miongozo ya usimamizi wa kesi na utoaji wa matibabu bure kwa wagonjwa. 

• Ombi la dozi 608 960 za chanjo ya polisaccharide ya ACW liliidhinishwa na kuwasilishwa na kikundi cha kimataifa cha kuratibu (ICG) kuhusu utoaji wa chanjo katika makundi mawili ya takriban dozi 300,000 kila moja tarehe 31 Desemba 2022 na 9 Januari 2023. 

• Kampeni za chanjo yenye ndogo ya ACW ya meningococcal polysaccharide zimetekelezwa na wizara ya afya kwa usaidizi wa WHO na muungano wa chanjo duniani (GAVI) katika wilaya za Dungass, Gouré, Mirriah na Matamèye, zikilenga rika la miaka 2 hadi 29 na kiwango cha jumla cha chanjo kilichofikiwa ni asilimia 99.8. 

• Mawasiliano kuhusu hatari na shughuli za ushirikishwaji wa jamii yanaendelea kwa ushirikiano wa karibu na watendaji na viongozi wa jamii katika wilaya zilizoathiriwa, kutoa ushauri wa afya na maambukizi, mapendekezo ya kuzuia na kudhibiti kupitia redio za jamii na njia nyingine, ikiwa ni pamoja na uhamasishaji wa nyumba kwa nyumba juu ya haja ya mara moja ya kutafuta usaidizi wa kimatibabu iwapo dalili zitatokea ili kuanza matibabu mara moja. 

Tathmini ya WHO kuhusu hatari iliyopo 

WHO inasema mlipuko unaoendelea unaonyesha idadi iliyoongezeka ya wagonjwa na kasi ya ongezeko ikilinganishwa na misimu iliyopita. 

Zaidi ya hayo, msimu wa janga la uti wa mgongo kawaida huanzia Januari hadi Juni, unaambatana na joto la juu na upepo mkavu pamoja na vumbi zito, kipindi kinachojulikana kama harmattan, mchanganyiko wa idadi ya watu, kutokea kwa magonjwa mengine ya mlipuko katika eneo hilohilo kama surua, diphtheria na COVID-19, ukosefu wa usalama na uhamishaji wa watu, yote katika muktadha wa janga la kibinadamu la muda mrefu, huenda vikachangia kuenea kwa mlipuko huo. 

WHO haipendekezi vikwazo vyovyote vya usafiri na biashara kwenda Niger kwa misingi ya taarifa inayopatikana kuhusumlipuko wa sasa.