Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yazungumzia shambulio dhidi ya walinda amani wake DRC

Walinda amani wa MONUSCO wakifanya doria eneo la Beni nchini DRC.
UN Photo/Sylvain Liechti
Walinda amani wa MONUSCO wakifanya doria eneo la Beni nchini DRC.

UN yazungumzia shambulio dhidi ya walinda amani wake DRC

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umezungumzia tukio la jana la kushambuliwa kwa msafara wa ujumbe wake wa kulinda amani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambapo raia watatu waliuawa na walinda amani 32 walijeruhiwa sambamba na madereva 3 wa malori. 

Msemaji wa  Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani amesema msafara huo ulishambuliwa katika barabara ya Kiwanja kwenda Munigi jimboni Kivu Kaskazini. 

Msafara ulishambuliwa baraba ya Kiwanja- Munigi 

 “Ukiwa njiani, msafara huo ndipo ulizuiwa na waandamanaji ambao walishambulia walinda amani kwa mawe, walipora vifaa na kuchoma moto magari,” amesema Dujarric. 

Akinukuu MONUSCO,  msemaji huyo ameongeza kuwa jeshi la serikali pamoja na polisi walifika na kuchukua hatua ya kutawanya waandamanaji huku ujumbe huo ukituma kikosi chake cha kuchukua hatua haraka, QRF, ambacho nacho pia baada ya kuwasili eneo la tukio, kilishambuliwa. 

Majeruhi walisafirishwa hadi hospitali ya MONUSCO iliyoko mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini ,Goma kwa matibabu zaidi. 

Ulinzi umeimarishwa katika vituo vyote vya MONUSCO  

Kwa sasa MONUSCO imeimarisha ulinzi kwenye vituo vyake vyote mashariki mwa DRC huku safari zozote ni zile za lazima na zilizoidhinishwa huko Goma, kutokana na ongezeko la vitisho dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. 

MONUSCO inaendelea kuwasiliana na mamlaka za kitaifa na majibo pamoja na viongozi wa kijamii ili kuondoa mvutano ulioko hivi sasa. 

Msemaji huyo amesema Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC ambaye pia ni Mkuu wa MONUSCO, Bintou Keita, amelaani ghasia hizo. 

Tayari mamlaka za DRC na MONUSCO wameanza uchunguzi wa pamoja ili kuweza kubaini mazingira ya shambulio hilo dhidi ya msafara wa walinda amani hao wa Umoja wa Mataifa.