Mratibu wa Misaada wa UN nchini Syria: Hatupati msaada wa kutosha

Maelfu ya watoto na familia wako hatarini baada ya matetemeko mawili mabaya ya ardhi kupiga kusini mashariki mwa Türkiye na Syria mnamo Februari 6, 2023.
© UNICEF/Can Erok
Maelfu ya watoto na familia wako hatarini baada ya matetemeko mawili mabaya ya ardhi kupiga kusini mashariki mwa Türkiye na Syria mnamo Februari 6, 2023.

Mratibu wa Misaada wa UN nchini Syria: Hatupati msaada wa kutosha

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mratibu wa muda wa Misaada ya Kibinadamu nchini Syria El- Mostafa Benlamlih amesema ingawa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa misaada wanafanya kila juhudi kusaidia wananchi walioathiriwa na matetemeko ya ardhi lakini hali ni mbaya kwani hawapati msaada ya kutosha.

Katika mahojiano maalum aliyofanya na Idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani El- Mostafa akiwa nchini Syria ameeleza mpaka sasa ingawa wanafahamu athari ni kubwa lakini bado hakuna ripoti kamili ya makadirio ya waathiriwa wa matetemeko ya ardhi hata hivyo kuna timu zinazofanya tathmini katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ikiwemo Halab na Aleppo, “Majengo mengi yameanguka, watu wakiongea wanataja namba kubwa, lakini ni takriban majengo 40 yameanguka na mengine yamepiga nyufa hivyo yanaweza kuanguka muda wowote.  Kwahiyo nadhani hii inaweza kukuonesha athari.”

Na je nini mashirika ya Umoja wa Mataifa yanafanya kusaidia wananchi walioathiriwa na matetemeko? “Sawa. Sote tunajaribu kuratibu na kuhakikisha kuwa tunafanya jambo sahihi na ili kuepuka kurudia kile mwingine anafanya. WHO wanaleta ndege mbili za misaada ya matibabu kutoka katika maghala yake yaliyoko Dubai ili kushughulikia mahitaji ya haraka.  WFP wanatoa chakula, tena kile kilicho tayari kuliwa na tena kwakutumia majiko yake wanatoa chakula chamoto kwa maelfu ya watu hasa wale wanaosaka hifadhi katika makazi ya muda na shule, nadhani tuna kama shule 70 au 80 ambazo zinatumika kama makazi ya muda ya watu wenye uhitaji na tunajitahidi kuwapa msaada wowote ule tunaoweza. UNFPA nao wanasaida hapo na kutoa misaada ya utu kwa watoto. UNICEF wanafanya tathmini pamoja na kuleta umakini kwenye mahitaji ya watoto. Pia shirika la kusaidia wakimbizi UNHCR nao wanatoa yale yanayohitajika ikiwemo kuweka makazi na vifaa vinavyohitajikana na watu.”

Hata hivyo mratibu huyo wa misaada wa UN amesema changamoto kubwa yanayokabiliana nayo hivi sasa ni mafuta ya petroli ili kuweza kufikisha misaada mahali inapohitajika kwani Syria hivi sasa inakabiliwa na uhaba wa mafuta hata hivyo kwa ushirikiano wa mashirika ya UN wanatumia mafuta waliyonayo hususan ya WFP kusambaza misaada.

Mratibu huyo alihitimisha mahojiano yake akieleza kuwa wasiwasi mkubwa hivi sasa ni kupata misaada ya kutosha kuweza kuwasaidia wananchi, “Ujumbe wa mwisho ni kwamba tunahitaji msaada kutoka kwa kila mtu. Hatupati msaada wa kutosha. Tunafanya kila tuwezalo kufika katika maeneo yanayohitaji usaidizi wetu, na tunahitaji usaidizi wa kila mtu. Na hilo ni jambo ambalo ni la haraka sana. Hatuwezi kusubiri hadi iwe tumechelewa sana.”