Tupunguze uchafuzi wa mazingira ili kuondokana na vijidudu sugu-UNEP

Usugu wa dawa kwa viua vijiumbe maradhi hutokea pale vijiumbe maradhi kama vile bakteria au vimelea, virusi na wengineo wanapokuwa wamebadilika katika kipindi fulani na hivyo hawawezi tena kutibika kwa kutumia dawa zilizoko
© WHO/Etinosa Yvonne
Usugu wa dawa kwa viua vijiumbe maradhi hutokea pale vijiumbe maradhi kama vile bakteria au vimelea, virusi na wengineo wanapokuwa wamebadilika katika kipindi fulani na hivyo hawawezi tena kutibika kwa kutumia dawa zilizoko

Tupunguze uchafuzi wa mazingira ili kuondokana na vijidudu sugu-UNEP

Tabianchi na mazingira

Hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira duniani, UNEP limetoa ripoti yake inayozitaka nchi duniani kupunguza uchafuzi wa mazingira kama njia mojawapo ya kupunguza vijidudu au vijiumbe maradhi vyenye usugu kwa dawa za viua vijiumbe maradhi, au AMR.

Ripoti hiyo ikipatiwa jina Kuibuka kwa vijidudu sugu: Kuimarisha hatua za mazingira ili kufanikisha hatua za kiafya dhidi ya usugu wa viua vijiumbe maradhi, imezinduliwa leo huko nchini Barbados wakati wa mkutano wa sita wa kundi la viongozi wa dunia kuhusu AMR.

Watu milioni 10 kufa kila mwaka hadi 2050 kutokana na AMR

Takribani watu milioni 10 wanaweza kufariki dunia kila mwaka hadi mwaka 2050 kutokana na usugu wa dawa dhidi ya vijiumbe maradhi, kiwango ambacho ni sawa na idadi ya watu waliokufa kutokana na saratani duniani mwaka 2020, imeonya ripoti hiyo.

Uchafuzi utokanao na shughuli za kiuchumi kwenye sekta kuu za maendeleo unatajwa kuwa sababu kuu ya maambukizi na kuenea kwa vijiumbe maradhi sugu duniani, imesema ripoti hiyo ya UNEP

Kama hiyo haitoshi gharama za kiuchumi za usugu wa vijidudu kwa viua vijiumbe maradhi unaweza kusababisha paot la taifa kwa mwaka kupungua kwa dola trilioni 3.4 kila mwaka na hivyo kutumbukiza zaidi ya watu milioni 24 kwenye linda la umaskini.

Vijidudu sugu au viua vijiumbe maradhi sugu ni nini ?

Taarifa iliyotolewa leo na UNEP jijini  Nairobi, Kenya inanukuu ripoti ikisema kuwa kampuni za dawa, sekta ya afya ni muhimu katika kupunguza kuibuka, maambukizi na kusambaa kwa vijidudu sugu, ambavyo ni aina ya vimelea au bakteria wasiotibika kwa viua vijasumu vinavyotambulika kwa sasa duniani.

UNEP inasema uwepo wa vijidudu hivyo tayari umesababisha madhara kwa afya ya binadamu, wanyama na mimea, halikadhalika uchumi.

Hatua za kimtambuka ndio muarobaini

Ripoti inasema changamoto hii ni mtambuka na hivyo inahitaji kutatuliwa kimtambuka, “na hatua hizi za kimtambuka zinaunga mkono usharikiwa pande nne unaojumuisha mashirika manne ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la mazingira, UNEP, la chakula na kilimo, FAO, la afya, WHO na la afya ya wanyama, WOAH.”

UNEP inasema kuibuka na kusambaa kwa usugu wa viua vijiumbe maradhi kuna maana ya kwamba dawa za kuua vijiumbe maradhi ambazo zimezoeleka kuzuia na kutibu maambukizi kwa binadamu, wanyama na mimea zitakuwa hazina ufanisi na hivyo dawa hizo za kisasa kutokuwa na uwezo wa kujibu hata maambukizi ya kawaida.

Fahamu janga la utatu kwenye sayari dunia

Viwango vya juu vya joto na mienendo isiyo ya kawaida ya hali ya hewa, mabadiliko ya matumizi ya ardhi yanayochochea mabadiliko ya anuwai ya vijiumbe maradhi pamoja na uchafuzi wa mazingira kibailojia na kikemikali vimetajwa kuwa janga la utatu kwenye sayari ya dunia. Vyote hivi vinachangia kuibuka na kusambaa kwa AMR.

Takribani watu milioni 10 watakuwa wanakufa kila mwaka hadi ifikapo mwaka 2050 kutokana na usugu wa dawa za viua vijiumbe maradhi, AMR
© Unsplash/Volodymyr Hryshchenko
Takribani watu milioni 10 watakuwa wanakufa kila mwaka hadi ifikapo mwaka 2050 kutokana na usugu wa dawa za viua vijiumbe maradhi, AMR

Kauli ya Mkuu wa UNEP

Uchafuzi wa hewa, udongo na maji unadumaza haki ya binadamu ya kuwa na mazingira safi na yenye afya. Vichocheo hivyo hivyo vinavyoharibu mazingira vinazidi kufanya usugu wa viua vijiumbe maradhi kwa dawa kuwa mbayá zaidi,” amesema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, akitoa maoni kuhusu ripoti hiyo.

Amesema athari hasi za usugu kwa viua vijiumbe maradhi unaweza kusambaratisha afya ya binadamu na mifumo ya chakula.

Kupunguza uchafuzi ni sharti la kuwa na karne nyingine ya kupunguza njaa na kuwa na afya njema,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNEP.

Nini kifanyike sasa?

  • Mosi: Kuweka mifumo katika ngazi ya kitaifa ya usimamizi, mipango, udhibiti na uratibu
  • Pili:Kuongeza juhudi za kimataifa za kuboresha mifumo ya usimamizi wa maji, matumizi ya maji, huduma za kujisafi na usafi ili kupunguza uendelezaji na kusambaa kwa usugu wa dawa kwenye mazingira pamoja na kupunguza maambukizi na mahitaji ya viua vijiumbe maradhi
  • Tatu: Kuongeza ujumuishaji wa masuala ya mazingira kwenye mipango ya kitaifa ya kudhibiti usugu wa viua vijiumbe maradhi ikiwemo usimamizi wa taka.

Mapendekezo kamili soma hapa