Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na mashirika yake wahaha kuwasaidia waathirika wa matetemeko Uturuki and Syria

Juhudi za kuwatafuta manusura kufuatia tetemeko la ardhi zinaendelea katika kitongoji cha Al-Aziziyeh mjini Aleppo nchini Syria.
© UNHCR/Hameed Maarouf
Juhudi za kuwatafuta manusura kufuatia tetemeko la ardhi zinaendelea katika kitongoji cha Al-Aziziyeh mjini Aleppo nchini Syria.

UN na mashirika yake wahaha kuwasaidia waathirika wa matetemeko Uturuki and Syria

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa leo yameendelea na harakati za kufanya kila liwezekanalo ili kuwasaidia maelfu ya watu walioathirika na matetemeko makubwa ya ardhi yaliyoikumba Uturuki na Syria jana na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 4,000 na wengine kwa maelfu kujeruhiwa.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO leo akizungumza katika kikao cha bodi ya watendaji wa shirika hilo mjini Geneva Uswis amesema yeye pamoja na mkuu wa masuala ya dharura wa shirika hilo wanatathimini hali nchini Uturuki na Syria.

Ameongeza kusema kuwa “Sote tumeshtushwa na kuhuzunishwa na picha na ripoti zinazotoka Uturuki na Jamhuri ya Kiarabu ya Syria. Sote tunatoa salam za masikitiko yetu makubwa na pole kwa wawakilishi wa nchi zote mbili hapa, na kwa watu wao. Ningependa kuwaalika ninyi nyote kusimama pamoja nami kukaa kimya kwa dakika moja, kuwaheshimu na kuwakumbuka wale ambao wamepoteza maisha, na kukumbuka wale ambao tunapozungumza wanaendelea kuwasaka manusura.”

Ameongeza kuwa kufikia sasa, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 4 000 wamepoteza maisha katika matetemeko hayo na wengine zaidi ya 18 700 wamejeruhiwa,” lakini sote tunajua kwamba idadi hii itaendelea kuongezeka kadri hali inavyoendelea. Bila shaka, kile ambacho idadi hii haituambii ni huzuni na hasara inayopatikana kwa familia hivi sasa ambazo zimepoteza mama, baba, binti, mwana walionasa chini ya vifusi au ambazo hazijui kama wapendwa wao. wako hai au wamekufa. Namba hazituambii juu ya hali ya hatari ambayo familia nyingi sasa zinakabiliwa nayo, baada ya kupoteza kila kitu, kulazimishwa kulala nje katikati ya majira ya baridi.”

Mkuu huyo wa Who Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesisitiza kwamba “Sasa ni mbio dhidi ya wakati. Kila dakika, kila saa inayopita, nafasi za kupata manusura hai hupungua. Mitetemeko inayoendelea, hali mbaya ya msimu wa baridi, uharibifu wa barabara, vifaa vya umeme, mawasiliano na miundombinu mingine inaendelea kutatiza ufikiaji wa waathirika na juhudi zingine za utafutaji na uokozi.”

Hali halisi ya athari za matetemeko

Kwa mujibu wa Serikali ya Uturuki, takriban watu 3,381 wamekufa na zaidi ya 20,000 wamejeruhiwa baada ya tetemeko la nguvu la kipimo cha rishta 7.8 kupiga karibu na mji wa kusini wa Gaziantep mapema Jumatatu, na kufuatiwa na tetemeko kingine la ardhi la ukubwa wa kipimo cha rishta 7.5 saa kadhaa baadaye.

Takriban majengo 6,000 yameripotiwa kubomoka nchini humo pia, amesema Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu (OCHA).

Athari kwa Syria

Mahitaji ya Syria ni makubwa, msemaji huyo wa OCHA ameendelea kusema , alipokuwa akitoa taarifa kutoka kwa mamlaka ya afya ya nchi hiyo ambayo imeripoti vifo 769 na majeruhi 1,448 kutokana na tetemeko la ardhi, katika mji wa Aleppo, Latakia, Hama, Idlib mashambani na Tartus.

Baada ya kustahimili matetemeko makubwa ya ardhi ya awali, jamii zilizopatwa na kiwewe nchini Syria kisha zimekabiliwa na zaidi ya mitetemeko mingine 200 ya baadaye.

"Zahma hii bila shaka imekuja wakati mbaya zaidi kwa watoto wengi, wengi walio katika mazingira magumu katika maeneo hayo ambao tayari walikuwa wanahitaji msaada wa kibinadamu," amesema James Elder, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

"Walilala kama kawaida, waliamshwa na mayowe ya majirani zao, kwa kuvunjika vioo na sauti ya kutisha ya nyumba zilizokuwa zikiporomoka."

Zahma juu ya zahma kwa watu wengi

Ingawa Syria iko katika mgogoro baada ya miaka 13 ya vita, kuna wasiwasi hasa kwa wale wote walioathiriwa na maafa ya Jumatatu ambao wanaishi katika maeneo yanayoshikiliwa na upinzani kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, mara baada ya kulazimishwa kukimbia makazi yao mara nyingi kwa sababu ya mapigano makali. .

"Tayari ilikuwa hali ya dharura kaskazini magharibi mwa Syria ambapo watu milioni nne wanapokea msaada wa kibinadamu. Jamii huko zinapambana na mlipuko wa kipindupindu, majira ya baridi kali na bila shaka mzozo unaoendelea,” ameeleza bwana Elder.

Likisisitiza wasiwasi huo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limesema kuwa hali ni ya kusikitisha katika mikoa 10 ya Uturuki iliyoathiriwa na matetemeko hayo ya ardhi.

Hali ya wakimbizi

Katika baadhi ya mikoa iliyoathiriwa huko Uturuki, asilimia 50 ya watu sasa ni wakimbizi, wakati huko Syria, msemaji wa UNHCR Matthew Saltmarsh ameelezea dharura ya tetemeko la ardhi kama pigo la nyundo kwa watu waliokimbia makazi yao ambao hawana kazi na ambao akiba yao imechoka.

“Tuko kwenye msimu mrefu wa baridi, tumekuwa tukiona dhoruba za theluji na bila shaka, unajua, vita vimekuwa vikiendelea kwa zaidi ya muongo mmoja," amesema.

Wakati timu za kimataifa za utafutaji na uokoaji zikiwasili katika eneo hilo, zinazoratibiwa na OCHA, msemaji wa shirika holo Jens Laerke amesisitiza kuwa "kuna upenyo wa takriban siku saba ambapo tutapata manusura wakiwa hai. Inaweza kutokea baadaye, lakini ni muhimu sana kwamba timu hizi zitoke huko haraka iwezekanavyo.’’

Waokoaji wakiwatafuta manusura chini ya vifusi vya mijengo katika kitongoji cha Al-Aziziyeh huko Aleppo Syria.
© UNHCR/Hameed Maarouf
Waokoaji wakiwatafuta manusura chini ya vifusi vya mijengo katika kitongoji cha Al-Aziziyeh huko Aleppo Syria.

Uhaba wa mafuta unaathiri shughuli za uokozi

Kando na uharibifu mkubwa wa barabara na miundombinu ya umma ambayo imefanya kazi ya timu za dharura kuwa ngumu zaidi, hali mbaya ya kiuchumi ya Syria pia imepunguza juhudi za misaada.

"Juhudi za utafutaji na uokozi kwa sasa zinatatizwa na ukosefu wa vifaa vya kuondoa uchafu," amesema Tommaso Della Longa, msemaji wa Shirikisho la kimataifa la vyama vya Msalaba mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC).

Ameongeza kuwa "Kuna upungufu mkubwa wa mafuta kote Syria na hii imetatiza uendeshaji wa mashine nzito, usafirishaji wa wafanyikazi na huduma za magari ya kubeba wagonjwa."

Maisha yako hatarini

Sambamba na wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi zote kuunga mkono wale wote ambao tayari wanahitaji sana misaada ya kibinadamu, Bwana Laerke ametoa ombi la dhati la msaada.

"Ni muhimu kwamba kila mtu alione hili, kwa jinsi lilivyo janga la kibinadamu ambapo maisha yako hatarini. Tafadhali, msiingize siasa yoyote kati ya haya, tupeleke misaada hiyo kwa watu ambao wanaihitaji sana.”

Hadi sasa, karibu watu 8,000 wameokolewa na timu za dharura zinazoratibiwa na mamlaka ya kudhibiti maafa na dharura ya Uturuki (AFAD), kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na washirika pia wametoa msaada wa kuokoa maisha mashinani, likiwemo shirika la Afya duniani WHO.

"Kwa kweli tumeweza kuhamisha vifaa vya kuhudumia wenye kiwewe na vifaa vya upasuaji kuvuka mpaka kutoka Gaziantep ambapo bila shaka tumeweka vifaa vingi na tumeweza kuvusambaza katika hospitali 16 nchini Syria, kwenye maeneo kufikia jana," amesema. Dkt. Margaret Harris, msemaji wa WHO.

Wapalestina wameathirika pia

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, takriban asilimia 90 ya familia za wakimbizi wa Kipalestina nchini Syria zinahitaji msaada wa kibinadamu kwa sababu ya matetemeko ya ardhi.

Wakimbizi wapatao 438,000 wa Kipalestina wanaishi katika kambi 12 za wakimbizi wa Syria na kaskazini mwa Syria ni nyumbani kwa wakimbizi 62,000 wa Kipalestina huko Latakia, Neirab, Ein-el Tal na Hama.

Akiongeza sauti yake kwa wale wanaotoa pole kwa wote walioathiriwa na maafa hayo, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria, Geir Pedersen, amesema kuwa amehuzunishwa sana na vifo vya watu na uharibifu mkubwa uliosababishwa na janga hilo la asili.