Hebu tujenge ushirika wa amani, asema Katibu Mkuu wa UN
Hebu tujenge ushirika wa amani, asema Katibu Mkuu wa UN
Hebu na tuazimie tena kujenga ushirika wa amani, ni sehemu ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliotoa hii leo ambao ni siku ya kimataifa ya udugu wa kibinadamu duniani, akisema wito wake huo unazingatia ongezeko la kauli za chuki, mizozo na misimamo mikali kwa misingi ya kiitikadi za kidini na makundi mbalimbali.
“Siku ya kimataifa ya udugu wa kibinadamu huadhimishwa kusherehekea maadili ambayo yanashikanisha jamii ya kibinadamu pamoja, upendo, uelewa wa kidini na kuheshimiana,” amesema Katibu Mkuu.
Zuia chuki, ondoa misimamo mikali
Katibu Mkuu amesema maadili hayo yanapatia msisitizo amani, lakini duniani kote yanamomonyolewa na kushamiri kwa migawanyiko, ukosefu wa usawa na ongezeko la watu kukata tamaa, sambamba na kushamiri kwa kauli za chuki, misimamo mikali na mizozo.
Amesema mifano ya misimamo mikali ya kidini na ukosefu wa stahmala kwenye jamii zote na zaidi ya yote imani, akiongeza kuwa “ni wajibu wa viongozi wa kidini kokote kule kuepusha kushamiri kwa chuki na waondoe misimamo mikali miongoni mwa wafuasi wao.”
Muundo wa maelewano baina ya imani mbalimbali za dini
Katibu Mkuu ametaja muundo wa maelewano baina ya imani mbalimbali za dini akitaja azimio la mshikamano baina ya makundi hayo ambalo ni, “Udugu wa kibinadamu kwa dunia ya amani na inayoishi pamoja,” lililoandikwa kwa pamoja na kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis na Imam Mkuu wa Al-Azhar, Sheikh Ahmed El Tayeb mwaka 2019.
“Hebu na sote tuhamasishwe na kurejelea tena ahadi yetu ya kusimama pamoja kama familia moja ya kibinadamu,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “na hebu tujenge ushirika wa amani, uliosheheni utofauti, usawa katika utu na haki na mshikamano.”
Hofu kuhusu chuki za kidini
Mwaka 2021, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kutenga tarehe 4 mwezi Februari kuwa siku ya Kimataifa ya Udugu wa kibinadamu.
Rasimu ya azimio hilo iliwalishwa kwa pamoja na Misri na Falme za Kiarabu ikielezea hofu kubwa ya vitendo vinavyochochea chuki, hasa wakati dunia ilipokabiliwa na janga la coronavirus">COVID-19 na majanga mengine yahusianayo.
Katika kupitisha azimio hilo, nchi wanachama walitambua mchango bora wa watu wa imáni za dini zote au imani za kibinadamu na mchango wa mashauriano baina ya makundi yote ya kidini kuelekea kuimarisha uelewa bora zaidi wa maadili ya pamoja ya kibinadamu.
Wiki ya utangamano wa kidini
Katika kuadhimisha wiki ya utangamano wa kidini, ambayo huadhimishwa kila wiki ya kwanza ya mwezi Februari, ofisi ya Uwakilishi wa Sierra Leone kwenye Umoja wa Mataifa na wadau wake waliendesha mkutano kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani ambapo washiriki walijadili mada ya utangamano katika dunia yenye majanga.