Nchi za Bangladesh, Ethiopia, DR Congo na Nigeria ni maskani ya ndoa nyingi za utotoni: UNICEF

Mwandishi wa UNICEF-Reporter Rifa mwenye umri wa miaka kumi na nane anatumia iPad kuhamasisha jamii kuhusu ndoa za utotoni huko Cox's Bazar, Bangladesh.
©UNICEF/UN0581091/Sujan
Mwandishi wa UNICEF-Reporter Rifa mwenye umri wa miaka kumi na nane anatumia iPad kuhamasisha jamii kuhusu ndoa za utotoni huko Cox's Bazar, Bangladesh.

Nchi za Bangladesh, Ethiopia, DR Congo na Nigeria ni maskani ya ndoa nyingi za utotoni: UNICEF

Wanawake

Zaidi ya wanawake na wasichana nusu bilioni walio hai hii leo waliolewa wakati wa utoto hata hivyo mzigo huu haubebwi kwa usawa, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirika la umoja wa Mataifa kuhudumia watoto UNICEF.

UNICEF inasema asilimia kubwa zaidi ya mabibi harusi hao wa utotoni imejikita katika idadi ndogo ya nchi, na hatari ya kuolewa katika umri mdogo inatofautiana sana kulingana na mahali ambapo msichana anaishi. 

Takwimu za shirika hilo la Watoto zinaonyesha kuwa nusu ya watoto wote walioolewa duniani kote wanaishi katika nchi tano tu ambazo ni India, Bangladesh, Nigeria, Indonesia na Brazil nan chi 10 duniani ndio zinazoshikilia asilimia 60 ya ndoa zote za utotoni. 

Hii ikiashiria kwamba nchi zilizo na changamoto kubwa ya ndoa za utotoni ziko katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara 

Kwa mujibu wa UNICEF “Msichana anapoolewa, utoto wake kawaida huisha. Ushahidi mwingi unaonyesha kwamba watoto wanaoolewa wanaweza kuacha shule, kupata mimba za utotoni na kutengwa na jamii, na kuwa na matarajio machache ya kuajiriwa. Huu ndio ukweli mzito unaokabiliwa na msichana mmoja kati ya watano kote ulimwenguni.” 

Lilian Phiri, mjumbe wa kamati ya kijamii ya usaidizi kwenye jamii ya Kagoro nchini Zambia (kushoto) akizungumza na Susan Banda, mnufaika wa mradi wa UNFPA na UNICEF wa kutokomeza ndoa na mimba za utotoni nchini humo.
UNICEF Zambia
Lilian Phiri, mjumbe wa kamati ya kijamii ya usaidizi kwenye jamii ya Kagoro nchini Zambia (kushoto) akizungumza na Susan Banda, mnufaika wa mradi wa UNFPA na UNICEF wa kutokomeza ndoa na mimba za utotoni nchini humo.

Ndoa za utotoni ni ukiukaji wa haki za binadamu 

Shirika hilo la kuhudumia watoto duniani linasema “Ndoa za utotoni zinatambuliwa kama ukiuaji mkubwa wa haki za binadamu lakini bado zinaendelea.” 

UNICEF imeongeza kuwa vitendo hivyo sio tuu vinawaathiri wasichana wadogo wanaoolewa bali pia familia zao, jamii nan chi kwa ujumla. 

Pia limesema ndoa hizo za utotoni zinaendelea mzunguko wa umasikini , zinaathiri usawa wa kijinsia na kuwa kikwazo cha mchakato wa kuelekea dunia bora zaidi yenye maono ya ajenda yam waka 2030 ya maendeleo endelevu SDGs. 

Ahadi ya kutokomeza ndoa za utotoni ifikapo 2030 

Ili kukabiliana na tatizo hilo la ndoa za utotoni, hatua za pamoja zaidi za kimataifa zinahitajika haraka limesema shirika la UNICEF iwapo dunia inataka kusonga mbele kuelekea lengo la Maendeleo Endelevu (SDG) la kutokomeza ndoa za utotoni ifikapo 2030, mageuzi ya haraka katika nchi zenye mzigo mkubwa ni muhimu. 

Ndiyo maana UNICEF inaunga mkono ahadi mpya iliyotolewa na serikali za Bangladesh, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Ethiopia na Nigeria  ambako ni nyumbani kwa asilimia kubwa ya watoto wa kike duniani wanaoolewa utotoni ili kuweza kukomesha ndoa hizo za utotoni. 

Kupitia ahadi hii, nchi hizo zimeahidi kuchukua hatua katika maeneo matano yenye ushahidi wa kuingilia kati: 

1. Hakikisha kwamba ukuaji wa uchumi unafikia sehemu zisizo na uwezo zaidi za jamii na kuweka mipango ya ulinzi wa kijamii inayozingatia jinsia ili kusaidia familia zenye uhitaji mkubwa. 

2. Kuimarisha sera za soko la ajira zinazohimiza kazi zenye staha kwa wanawake ili wazazi waone thamani ya kuwaweka watoto wao wa kike shuleni, na kukuza sera zinazoshughulikia mzigo wa kazi za malezi bila malipo, ambayo huwaangukia wasichana na wanawake kwa njia isiyo sawa. 

3. Kuwekeza katika elimu bora ya sekondari inayowawezesha wasichana kupata maarifa, kujifunza ujuzi na kuboresha matarajio yao ya ajira ya baadaye. 

4. Kuwawezeshe wasichana ambao tayari wameolewa, walioachwa au wajane kwa kusaidia kuendelea kwao au kurudi shuleni, na kuboresha upatikanaji wao wa huduma za afya. 

5. Kukabiliana na kanuni hatari za kijinsia na mienendo ya nguvu katika juhudi zote ili kuhakikisha kwamba wasichana wanawezeshwa kuzungumza na kufanya maamuzi yao wenyewe kuhusu kama, lini na nani wataolewa nao. 

Watoto wa kike wanakuwa hatarini kuozeshwa mapema na wengi wao ni wale wanaotoka familia maskini na makundi ya pembezoni
©UNFPA-UNICEF Nepal/KPanday
Watoto wa kike wanakuwa hatarini kuozeshwa mapema na wengi wao ni wale wanaotoka familia maskini na makundi ya pembezoni

Kutumia takwimu ili kuchochea hatua 

UNICEF imesisitiza kuwa hakuna wakati wa kupoteza kwani licha ya maendeleo katika nyanja nyingi kwa miaka, matukio ya hivi karibuni yamerudisha nyuma maendeleo.  

Kabla ya janga la COVID-19, kulingana na makadirio ya UNICEF, wasichana milioni 100 walikadiriwa kuwa wachumba katika muongo mmoja ujao.  

Wasichana wengine milioni 10 sasa wako katika hatari ya ndoa za utotoni ifikapo mwaka 2030 kutokana na janga hili.  

Mchanganyiko wa mambo unachangia hatari hii kubwa, ikiwa ni pamoja na majanga ya kiuchumi, kufungwa kwa shule na kukatizwa kwa huduma.  

Katika maeneo mengi ya dunia, hatari ya ndoa za utotoni inachangiwa zaidi na ukosefu wa usalama na vitisho vinavyoletwa na migogoro na mabadiliko ya tabianchi. 

Ili kusaidia kukabiliana na tatizo hilo, UNICEF inajivunia kuongoza mpango wa ufuatiliaji wa ndoa za utotoni (CMMM), mpango unaoangazia suala la ndoa za utotoni kwa kuhimiza matumizi ya takwimu ili kuibua muonekano wake, kuboresha mikabala ya sera na kudumisha dhamira na ufadhili.  

Utaratibu huu wa ufuatiliaji unalenga kuweka takwimu mikononi mwa wadau mbalimbali, kwa kuelewa kwamba kukomesha ndoa za utotoni kunahitaji juhudi shirikishi za aina nyingi za watumiaji wa takwimu.  

Kwa kuzingatia jukumu lake kama shirika mlezi wa lengo la Maendeleo Endelevu namba 5.3.1, UNICEF inatumika kama kiongozi wa kiufundi wa CMMM. 

“Kupitia utaratibu wa kufuatilia ndoa za utotoni, tunasimama na serikali na washirika kuongeza uwekezaji ili kukomesha ndoa za utotoni leo, na kupanga mustakabali mwema kwa wasichana wote, kila mahali duniani.”