Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde jumuiya ya kimataifa tuinusuru Myanmar: Hayzer

Mtoto akimtunza ndugu mdogo wake nchini Myanmar.
World Bank/Tom Cheatham
Mtoto akimtunza ndugu mdogo wake nchini Myanmar.

Chonde chonde jumuiya ya kimataifa tuinusuru Myanmar: Hayzer

Amani na Usalama

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar Noeleen Hayzer ametoa wito wa mshikamano wa kimataifa kuinusuru Myanmar kwa msaada wa kibinadamu, msimamo kuhusu uchaguzi na ulinzi wa raia.

Katika taarifa yake iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswis na Bankok Thailand Bi. Hayzer amesema “Wakati mgogoro wa Myanmar ukiingia mwaka wa tatu kuna hatua muhimu na Madhubuti ambazo zinahitaji mshikamano wa kikanda na kimataifa ukiongozwa na Myanmar ili kumaliza machafuko na madhila na pia kuisaidia Myanmar kurejea katika njia ya demokrasia inayoongozwa na matakwa ya wananchi.”

Katika wito wake wa dharura, mjumbe huyo maalum ameangazia misaada ya kibinadamu bila ubaguzi na kupitia njia zote zinazopatikana, msimamo wa pamoja juu ya mipango ya kijeshi ya uchaguzi, na ulinzi wa raia wakiwemo watu wote ndani ya Myanmar na wakimbizi.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, uvurugaji wa jeshi  wa demokrasia ya mpito ya Myanmar umesababisha uharibifu mkubwa kwa nchi na watu, na kusababisha mzozo wa pande nyingi unaosababisha athari mbaya za kibinadamu, uvunjifu wa haki za binadamu, masuala ya kijamii na kiuchumi na athari kubwa za kikanda.

Ameongeza kuwa “Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, watu milioni 15.2 walikuwa na uhaba wa chakula, zaidi yawatu milioni 1.5 wamekuwa wakimbizi wa ndani na wastani wa majengo 34,000 ya kiraia yalikuwa yameharibiwa tangu jeshi kuchukua hatamu.”

IOM likitoa msaada wa matibabu kwa wakimbizi wapya wa Rohingya waliowasili.
IOM
IOM likitoa msaada wa matibabu kwa wakimbizi wapya wa Rohingya waliowasili.

Hatari kwa wakimbizi na wakimbizi wa ndani

Kwa mujibu wa Bi. Hayzer wakimbizi wa Rohingya walioa katika kambi za wakimbizi na wale waliosalia nchini, pamoja na jamii zingine zilizotengwa, wako kwenye hatari kubwa huku mwaka 2022 ikiwa ni moja ya miaka mibaya zaidi kwa watu kulazimika kufanya safari hatari za baharini.

Mjumbe huyo maalum amerejelea wito wa Umoja wa Mataifa wa mshikamano wa na watu wa Myanmar na hitaji la ulinzi wa jamii zote, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza katika taarifa yake ya hivi karibuni.

Amenukuu wasiwasi wa Katibu Mkuu kuhusu nia iliyotajwa ya jeshi ya kufanya uchaguzi, ambayo inatishia kuzidisha ghasia na ukosefu wa utulivu kwa kukosekana kwa mazungumzo jumuishi ya kisiasa na masharti ambayo yanaruhusu raia kutumia haki zao za kisiasa kwa uhuru bila woga au vitisho.

Masuala matatu muhimu ya kuzingatia

Mjumbe huyo wa Umoja wa Martaifa ametoa wito wa haraka wa mshikamano kwa jumuiya ya kimataifa katika masuala matatu muhimu ambayo ni

Mosi: jumuiya ya kimataifa, na hasa wafadhili na majirani wa Myanmar, lazima waje pamoja na wahudumu wa kibinadamu ikiwa ni pamoja na mitandao ya ndani ya kibinadamu ili kuongeza msaada unaohitajika haraka kwa wale wote wanaohitaji bila ubaguzi na kupitia njia zote zilizopo.

Ahadi ya kuongeza viwango vya usaidizi wa kuvuka mpaka, pamoja na sheria rahisi zaidi za benki na utoaji wa taarifa, vitawezesha usaidizi wa kibinadamu kwa watu wanaouhitaji zaidi.

Pili: Jumuiya ya kimataifa lazima ijenge msimamo thabiti zaidi kuhusu uchaguzi uliopangwa na jeshi ambao utachochea ghasia zaidi, kurefusha mzozo na kufanya kurejea kwa demokrasia na utulivu kuwa vigumu zaidi.

Tatu: Jumuiya ya kimataifa lazima itekeleze hatua za kuongeza ulinzi kwa raia ndani ya Myanmar na pia kwa wakimbizi wa Myanmar katika eneo kubwa zaidi. Hatua kama hizo zinaweza kujumuisha utaratibu wa ufuatiliaji wa chinichini kama sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ASEAN ya mambo matano na dhamira yake ya kukomesha ghasia nchini Myanmar, na mifumo ya kikanda ya ulinzi wa wakimbizi na watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao.

"Haiwezekani kuwa na aina yoyote ya kipindi cha mpito cha amani na kidemokrasia kinachoweza kuletwa na wale wanaosababisha madhara kwa raia wao," Mjumbe maalum Heyzer amesema na kuongeza kuwa "Vurugu hizo zinapaswa kukomeshwa, ikiwa ni pamoja na milipuko ya mabomu ya angani na uchomaji moto wa miundombinu ya kiraia pamoja na wanajeshi wanaoendelea kuwakamata viongozi wa kisiasa, watendaji wa mashirika ya kiraia na waandishi wa habari."