Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Ukoma Duniani inalenga hatua za kukomesha maambukizi ya ugonjwa huo wenye umri wa zaidi ya miaka 4000

Watu walioathiriwa na ukoma bado wanaendelea kukumbwa na unyanyapaa na ubaguzi
© PAHO/Joshua Cogan
Watu walioathiriwa na ukoma bado wanaendelea kukumbwa na unyanyapaa na ubaguzi

Siku ya Ukoma Duniani inalenga hatua za kukomesha maambukizi ya ugonjwa huo wenye umri wa zaidi ya miaka 4000

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO linasema katika muongo huu linataka kuondoa maambukizi ya asili ya ukoma na kuna mazingira yanayofaa kutokomeza ugonjwa huo; matokeo yanategemea hatua za haraka na jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa wagonjwa ambao bado hawajafikiwa. 

Katika Siku ya Ukoma Duniani, iliyoadhimishwa Jumapili hii, WHO, inasisitiza lengo la kuwa na nchi 120 bila mgonjwa wa asili wa ukoma ifikapo 2030. Siku hii ya ukoma huadhimishwa kila Jumapili ya mwisho ya Januari, na kwa mwaka huu ina kauli mbiu “Chukua sasa. Komesha ukoma”. 

Rekodi za ugonjwa huo wa ukoma zinaonesha kushuka kwa 30%, ikilinganishwa na maambukizi 200,000 ya kila mwaka yaliyogunduliwa kabla ya janga la Covid-19. “Kupungua huku kumechangiwa na kukatizwa kwa programu za afya katika kipindi hicho.” Inasema WHO. 

Unyanyapaa na Ubaguzi 

WHO inaamini kuwa bado inawezekana katika kizazi hiki kusitisha maambukizi ya ugonjwa huo, ambao una zaidi ya miaka 4,000. 

Mamilioni ya watu wanaishi na ulemavu unaohusiana na ukoma, hasa katika Asia, Afrika na Amerika Kusini. Ukosefu wa matibabu inaweza kusababisha matatizo makubwa. 

WHO inatoa wito wa kutumia vyema fursa ya kusherehekea watu ambao wamepona ukoma, kuongeza ufahamu kuhusu ugonjwa huo na kutetea kukomeshwa kwa unyanyapaa na ubaguzi. 

Uwezekano wa kuutokomeza ukoma 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia afya katika ulimwengu mzima linasema kuwa kaulimbiu ya mwaka huu pia inaonesha uwezekano wa kutokomeza ugonjwa huo kwa sababu kuna uwezo na zana zinazopatikana za kukatiza maambukizi. 

WHO pia inaomba tarehe hii iwe tafakari ya kuchukua hatua mara moja, kukusanya rasilimali na kuongeza dhamira ya kutanguliza uondoaji wa ukoma. 

Mwisho WHO inasisitiza haja ya kuwafikia watu ambao hawana matibabu ya ugonjwa huu wa ukoma unaozuilika na unaotibika.