Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatiwa na wasiwasi hali ya amani Peru; yataka utulivu Peru

Anga la Chorrillos, moja ya vitongoji vya mji mkuu wa Peru, Lima
© Roberto Villanueva
Anga la Chorrillos, moja ya vitongoji vya mji mkuu wa Peru, Lima

UN yatiwa na wasiwasi hali ya amani Peru; yataka utulivu Peru

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama inavyoendelea kuzorota nchini Peru, hususan ripoti zaidi za vifo kufuatia makabiliano kati ya vikosi vya usalama na watu  wanaoandamana kupinga serikali wakitaka rais Dina Boluarte ajiuzulu.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani imemnukuu Katibu Mkuu akisihi mamlaka kufanya uchunguzi wa haraka na huru wa vifo hivyo na kuepusha unyanyapaa dhidi ya manusura.

Chanzo cha mzozo

Vyombo vya  habari vinasema hadi sasa watu wapatao 50 wameuawa kwenye maandamano hayo ambapo waandamanaji wanapinga kitendo cha Rais Boluarte kuapishwa kuchukua nafasi ya mtangulizi wake Pedro Castillo ambaye bunge lilipiga kura ya kumuondoa madarakani kutokana na kutokuwa na imani naye tarehe 7 mwezi uliopita wa Desemba baada ya jitihada zake za kuvunja Baraza la Kongresi kugonga mwamba.

Maandamano yameendelea licha ya Rais Boluarte ambaye alikuwa Makamu Rais kutaka maridhiano ya kitaifa wakati huu ambapo uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Aprili 2024.

Pande husika jizuieni ili kuepusha ghasia zaidi

Wakati huu maandamano yanaendelea, Katibu Mkuu ametaka pande zote kujizuia na kuepusha ghasia zaidi huku akitoa wito kwa mamlaka kuzingatia sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Amesisitiza kuwa maandamano lazima yafanyike kwa amani, yaheshimu haki ya uhai na mali za watu.

“Hata wakati wa dharura ya umma, mikakati ya kumomonyoa haki ya kukusanyika kwa amani lazima iwekwe tu kwa kuzingatia hali ilivyo na kwa mujibu wa sheria za kimataifa,” amesema Katibu Mkuu.

Bwana Guterres amesema ni muhimu kuweka mazingira yanayoweza kuchochea mashauriano ya dhati na jumuishi ili kutatua janga la sasa.