Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Inditex yajiunga na mtandao wa ILO wa biashara na mtandao wa wenye ulemavu

Changamoto nyingi zinawakabili watu wenye ulemavu ikilinganishwa na watu wasio na ulemavu linapokuja suala la ulimwengu wa kazi
ILO
Changamoto nyingi zinawakabili watu wenye ulemavu ikilinganishwa na watu wasio na ulemavu linapokuja suala la ulimwengu wa kazi

Inditex yajiunga na mtandao wa ILO wa biashara na mtandao wa wenye ulemavu

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kampuni ya Inditex  ambayo ni muuzaji mkubwa wa nguo duniani ni kampuni ya hivi karibuni kabisa kujiunga na mtandao wa kimataifa wa biashara na ulemavu GBDN wa shirika la kazi la Umoja wa Mataifa duniani ILO. 

Mtandao wa biashara na ulemavu wa shirika la ILO unalenga kuongeza kutambuliwa na makampuni, kama vile Inditex  muuzaji mkuu wa nguo duniani na kufahamisha manufaa ya kujumuishwa kwa ulemavu. 

Mkurugenzi mtendaji wa kundi hilo, la Inditex Óscar García Maceiras, ametangaza hatua hiyo wakati wa mkutano huko Geneva Uswis na mkurugenzi mkuu wa ILO, Gilbert F. Houngbo.  

Wote wawili walitia saini mkataba wa GBDN, ambao huwapa watia saini wa kampuni fursa ya kuunga mkono kanuni kumi za ujumuishaji wa wenye ulemavu. Kanuni kumi za mkataba huu ni pamoja na usawa wa matibabu na fursa, upatikanaji na uhamasishaji, utoaji wa malazi yanayofaa mahali pa kazi na ushirikiano na mashirika ya watu wenye ulemavu. 

Tunaipongeza hatua ya Inditex 

Mkurugenzi mkuu wa ILO Houngbo amekaribisha hatua ya Inditex akisema  “Makampuni yanazidi kutambua kuwa utofauti wao, usawa na juhudi za ujumuishi lazima zishughulikie ujumuishaji wa watu wenye ulemavu ili kuleta mabadiliko chanya na endelevu ya biashara. Mtandao wa ILO wa biashara na wenye ulemavu duniani unatoa nafasi ya kipekee kwa makampuni ya biashara kujifunza na kusaidiana katika safari yao ya kujumuisha wenye ulemavu,”  

García Maceiras amersisitiza kuwa "Ushirikishwaji wa wenye ulemavu mahali pa kazi ni sehemu ya msingi ya kujitolea kwetu kwa watu. Utofauti, usawa na ujumuishi ni maadili ambayo sote tunakumbatia, maadili tunayofuata siku hadi siku, ili kuwa na athari chanya ndani ya Inditex, na pia watu wote wanaotuzunguka, ahadi yetu ni kubuni fursa kwa kila mtu."  

Ili kuonyesha kujitolea kwake kwa GBDN, Inditex inatarajia kuajiri watu 1,500 wenye ulemavu duniani kote katika mitandao yake ya maduka, vifaa vya usafirishaji, maghala na ofisi zake kote ulimwenguni.  

“Katika masoko ambapo hakuna viwango maalum vinavyohitajika, lengo la kampuni ni kwamba angalau asilimia 2 ya wafanyikazi wake wa ndani wanapaswa kuwa watu wenye ulemavu.” Amesema mkuu wa Inditex 

Kuhusu mtandao wa GBDN 

Mtandao wa kimataifa wa ILO wa biashara na wenye ulemavu GBDN ulianzishwa mwaka wa 2010,  na ni mtandao wa kipekee unaoongozwa na waajiri duniani kote wa makampuni 36 ya kimataifa, biashara 34 za kitaifa na mitandao ya watu wenye ulemavu, ukijumuisha kutoka katika nchi zinazoendelea, pamoja na wanachama wanane wasio wa biashara yaani taasisi za kitaaluma na mashirika yasiyo ya kiserikali ya masuala ya ulemavu na maendeleo, yakifanya kazi kwa ushirikiano ili kukuza ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika sekta binafsi, kwa faida ya sekta zote.