Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majanga lukuki yasababisha ukuaji finyu wa uchumi duniani

Wajasiriamali Cape Town nchini Afrika Kusini
John Hogg/World Bank
Wajasiriamali Cape Town nchini Afrika Kusini

Majanga lukuki yasababisha ukuaji finyu wa uchumi duniani

Ukuaji wa Kiuchumi

Mchanganyiko wa majanga lukuki umechochea kiwango kidogo  zaidi cha ukuaji wa uchumi duniani kuwahi kushuhudiwa katika miongo ya hivi karibuni na mwelekeo unazidi kutia shaka, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo ikimulika ukuaji uchumi mwaka jana na makadirio kwa mwaka huu.

Ikitolewa hii leo jijini New York, Marekani na Idara ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya kiuchumi na kijamii, DESA, ripoti hiyo Hali ya Uchumi Duniani na Matarajio, WESP imetaja majanga hayo kuwa ni COVID-19, vita ya Ukraine na kuchochea kwake katika  ongezeko la bei ya nishati na vyakula, mfumuko wa bei, madeni na dharura ya tabianachi.

Ripoti inasema kinachotakiwa sasa ni mikakati thabiti ya kifedha ili kupatia uhai uchumi wa dunia na kufanikisha ajenda ya maendeleo.

Kwa hali ilivyo sasa, kasi ya ukuaji uchumi inatarajiwa kuporomoka kutoka asilimia 3.0 mwaka 2022 hadi asilimia 1.9 mwaka huu wa 2023, na hivyo kuwa ni kiwango kidogo zaidi cha ukuaji uchumi kuwahi kurekodiwa katika miongo ya karibuni,” imesema WESP.

Taswira ya uchumi ni kiza kinene

Kinachowasilishwa kwenye ripoti hiyo ni taswira ya kiza kinene na kutokuweko na uhakika wa uchumi bora katika siku za usoni.

Hata hivyo nuru inaonekana mwaka 2024 ambako yakadiriwa kiwango cha ukuaji kinakadiriwa kuongezeka na kufikia asilimia 2.7 kwa kuwa baadhi ya changamoto zitaanza kupungua.

Ripoti inasema hali hiyo ingawa hivyo itategemea ubanaji wa matumizi, mwelekeo wa vita ya Ukraine na uwezekano wa kuvurugwa tena kwa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa.

Mkazi huyu wa akiwa eneo la soko la Konyokonyo mjini Juba nchini Sudan Kusini akivalia vizuri barakoa yake kujikinga na virusi vya Corona. UNICEF ilitengeneza barakoa 6,000 na kuzisambaza kwa wanajamii.
© UNICEF/Bullen Chol
Mkazi huyu wa akiwa eneo la soko la Konyokonyo mjini Juba nchini Sudan Kusini akivalia vizuri barakoa yake kujikinga na virusi vya Corona. UNICEF ilitengeneza barakoa 6,000 na kuzisambaza kwa wanajamii.

Ukuaji vuguvugu wa uchumi watishia Ajenda 2030

Angalizo linatolewa kwenye ripoti ya kwamba makadirio ya ukuaji vuguvugu wa uchumi yanatishia mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs au Ajenda 2030 wakati huu ambapo mkutano wa viongozi wa mwezi Septemba mwaka huu unafanyika kujadili malengo hayo ikiwa “tumefikia nusu ya kipindi cha utekelezaji wa malengo hayo.”

Kauli ya Katibu Mkuu wa UN kuhusu WESP 2022

“Huu si wakati wa kuchukua hatua nusu nusu au upunguzaji matumizi ambao unachochea ukosefu wa usawa, kuongeza machungu na hata kutowesha matumaini ya kufanikisha SDGs,” anasema Katibu Mkuu wa UN António Guterres.

Badala yake anasema nyakati za sasa zisizo za kawaida zinataka hatua zisizo za kawaida. “Hatua hizo ni pamoja na marekebisho katika mipango ya kuchechemua SDGs, marekebisho ambayo yatafanyika kupitia hatua za pamoja na thabiti za wadau wote.”

Mwelekeo wa kiza wa kiuchumi kwa tajiri na maskini

Ripoti inasema mfumuko wa bei ukishika kasi, ubanaji wa fedha nao vivyo hivyo na kuna hofu kubwa wakati huu ambapo kudorora kwa ukuaji uchumi kumekwamisha harakati za kujikwamua baada ya janga la COVID-19 na hii inatishia nchi kadhaa zikiwemo zilizoendelea na zinazoendelea huku mdororo wa uchumi ukinyemelea.

Kasi ya ukuaji uchumi ilidorora kwa wazi Marekani, nchi za Muungano wa Ulaya na nchi nyingine tajiri mwaka 2022 na kuwa na madhara kwa mataifa mengine duniani kwa njia mbali mbali.

Kiwango cha madeni kimeongezeka ambapo zaidi ya asilimia 85 ya Benki Kuu duniani kote zimeongeza sera za kifedha na kuongeza viwango vya riba kuanzia mwishoni mwa mwaka 2021 kwa lengo la kukabili mfumuko wa bei na kuepusha mdororo wa kiuchumi.

Kwa sasa kiwango cha mfumuko wa bei kimevunja rekodi na kufikia cha juu zaidi takribani asilimia 9 mwaka 2022 lakini mwaka 2023 kinatarajiwa kupungua lakini bado kuwa ni cha juu ambacho ni asilimia 6.5.

UNDP inasaidia wanawake wafanyabiashara kurejea katika biashara baada ya janga la COVID-19
UNDP Tanzania
UNDP inasaidia wanawake wafanyabiashara kurejea katika biashara baada ya janga la COVID-19

Ajira nazo zimesuasua, umaskini unaongezeka

Katika nchi nyingi zinazoendelea, ukwamukaji kwenye soko la ajira mwaka 2022 ulisuasua na ajira zilisalia ndoto kwa wengi.

Kitendo cha wanawake wengi kupoteza ajira wakati wa awamu ya kwanza ya janga la COVID-19 bado hakijapata jawabu la kutosha huku nuru ikiwaelekea kupitia ajira zisizo rasmi.

Kwa muijbu wa ripoti hiyo, kasi ndogo ya ukuaji uchumi, ongezeko la mfumuko wa bei na hatari ya ongezeko la madeni vinatishia kurudisha hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa SDGs.

Mwaka 2022 idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula iliongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka 2019, na kufikia milioni 350.

Mkuu wa DESA Li Junhua anasema “majanga ya sasa yanapiga zaidi wale ambao tayari walikuwa taabani licha ya kwamba wao sio tatizo. Jamii ya kimataifa inahitajika kuimarisha juhudi za pamoja kuepusha machungu ya kibinadammu na kusaidia mustakabali jumuishi na endelevu kwa wote.”

Irene Pallangyo, (kushoto) mjasiriamali wa kitanzania ambaye wakati wa janga la COVID-19 alilazimika kuanza biashara ya bidhaa mtandaoni kwa kuwa janga hilo liliathiri biashara ya kupeleka watalii kwenye mbuga za wanyama.
UN News
Irene Pallangyo, (kushoto) mjasiriamali wa kitanzania ambaye wakati wa janga la COVID-19 alilazimika kuanza biashara ya bidhaa mtandaoni kwa kuwa janga hilo liliathiri biashara ya kupeleka watalii kwenye mbuga za wanyama.

Ushirikiano wa kimataifa ni muhimu

Ripoti inatoa wito kwa serikali kuepuka ubanaji matumizi unaoweza kuathiri walio hatarini zaidi.

Inapendekeza upangaji upya vipaumbele kwenye matumizi ya fedha za umma kupitia hatua za moja kwa moja za kisera ambazo zitafungua fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Halikadhalika  uwekezaji wa kimkakati kwenye elimu, afya, miundombinu ya kidijitali, teknolojia mpya na hatua za kuhimili na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.