Zaidi ya dola milioni 500 kuchagiza maendeleo bonde la Ziwa Chad

Picha ya maktaba ikiwaonesha akari wa Cameroon wakifanya doria katika maeneo ya Ziwa Chad ambayo yameathiriwa na shughuli za kigaidi. (Februari 2019)
UN Photo/Eskinder Debebe
Picha ya maktaba ikiwaonesha akari wa Cameroon wakifanya doria katika maeneo ya Ziwa Chad ambayo yameathiriwa na shughuli za kigaidi. (Februari 2019)

Zaidi ya dola milioni 500 kuchagiza maendeleo bonde la Ziwa Chad

Amani na Usalama

Mkutano wa 3 wa Ngazi ya Juu kuhusu Bonde la Ziwa Chad umehitimishwa leo kwa kuthibitishwa ahadi kutoka kwa nchi za Bonde la Ziwa Chad na wadau kwa mwitikio ulioratibiwa, wa kikanda na ulio endelevu.

Mkutano huo uliohitimishwa leo katika mji mkuu wa Niger, Neamey, ulilenga kuhakikisha usaidizi wa kibinadamu na ulinzi na kukuza fursa za ufumbuzi wa kudumu, ikiwa ni pamoja na kurejea, kuunganishwa tena katika jamii na kuwapa makazi wakimbizi wa ndani na wakimbizi kutoka nje kwa kuzingatia uamuzi wa wa hiari, wenye heshima na ufahamu kuhusu uamuzi huo.  

Mkutano huo wa siku mbili umeleta pamoja zaidi ya nchi 30, mashirika ya kimataifa na zaidi ya mashirika 100 ya kiraia ambapo wamekubaliana kufanya kazi pamoja kutatua changamoto zilizopo. 

Washiriki wametambua kuwa usalama unarejeshwa katika sehemu za kanda hiyo ya Ziwa Chad, kutokana na juhudi za nchi hizo nne - Niger, Nigeria, Cameroon na Chad. 

Hata hivyo mkutano huo umekumbushia hitaji muhimu la kushughulikia mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka, sababu za msingi za chanzo cha mgogoro wa Bonde la Ziwa Chad na kuimarisha mnepo wa mamilioni ya watu walioathirika. 

Eneo la Bonde la Ziwa Chad linaendelea kukabiliana na mgogoro wa muda mrefu na tata unaotokana na umaskini uliokithiri, mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya vurugu na ukosefu wa huduma za kijamii, licha ya mafanikio mengi. Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA inaeleza kuwa leo, zaidi ya watu milioni 24 katika eneo hilo la Bonde la Ziwa Chad wameathiriwa na mgogoro huo na takriban watu milioni 5.3 wamelazimika kuyahama makazi yao. 

Mwisho Nchi Wanachama na wafadhili wa kitaasisi wametangaza zaidi ya dola milioni 500 za kimarekani kusaidia hatu za kikanda zilizoratibiwa za kushughulikia mgogoro katika kanda ya Ziwa Chad.