Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miezi 11 ya vita nchini Ukraine imevuruga elimu kwa zaidi ya watoto milioni tano - UNICEF

Watoto wa Ukraine waliofurushwa wakicheza na kujifunza katika Kituo cha watoto cha Spilno cha Kharkiv, kinachoendeshwa na UNICEF na washirika.
© UNICEF/Christina Pashkina Watoto wa Ukraine waliofurushwa wakicheza na kujifunza katika Kituo cha watoto cha Spilno cha Kharkiv, kinachoendeshwa na UNICEF na washirika.

Miezi 11 ya vita nchini Ukraine imevuruga elimu kwa zaidi ya watoto milioni tano - UNICEF

Utamaduni na Elimu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya elimu, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) limeeleza na kuonya kuhusu namna vita inayoendelea nchini Ukraine imevuruga elimu kwa watoto zaidi ya milioni tano na likatoa wito wa kuongezwa msaada wa kimataifa ili kuhakikisha watoto hawabaki nyuma zaidi. 

Katika taarifa ya iliyotolewa leo katika miji mitatu duniani, Kyiv – Ukraine, Geneva – Uswisi na New York – Marekani UNICEF imesema athari za miezi 11 ya mgogoro inaongezea kwenye miaka miwili ya kupoteza kujifunza kutokana na janga la coronavirus">COVID-19, na zaidi ya miaka 8 ya vita kwa watoto mashariki mwa Ukraine. 

"Shule na mazingira ya elimu ya utotoni yanatoa hali muhimu ya muundo na usalama kwa watoto, na kukosa kujifunza kunaweza kuwa na madhara ya maisha yote," anasema Afshan Khan, Mkurugenzi wa UNICEF wa Kanda ya Ulaya na Asia ya Kati na akiongeza kusema, "hakuna kitufe cha kusitisha. Sio chaguo kuahirisha tu elimu ya watoto na kuirejelea mara tu vipaumbele vingine vinapokuwa vimeshughulikiwa, bila kuhatarisha mustakabali wa kizazi kizima.” 

Kuendelea kwa matumizi ya silaha za milipuko - ikiwa ni pamoja na katika maeneo yenye watu wengi - kumemaanisha kuwa maelfu ya shule, shule za awali au miundombinu mingine ya elimu kote nchini Ukraine imeharibiwa. Wakati huo huo, wazazi na walezi wengi wanasita kuwapeleka watoto shuleni kwa sababu za usalama. Inaeleza UNICEF.  

Ndani ya Ukraine, UNICEF inafanya kazi na Serikali kusaidia kuwarejesha watoto kujifunza katika  madarasa inapoonekana kuwa salama, na kupitia njia mbadala za mtandaoni au za kijamii ikiwa kujifunza ana kwa ana hakuwezekani. Wakati zaidi ya watoto milioni 1.9 walikuwa wakipata fursa za kujifunza mtandaoni, na watoto milioni 1.3 walijiandikisha katika mchanganyiko wa ana kwa ana na mtandaoni, mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya miundombinu ya umeme na nishati nyingine yamesababisha kukatika kwa umeme na kuacha karibu kila mtoto nchini Ukraine bila upatikanaji endelevu wa umeme kumaanisha kuwa hata kuhudhuria madarasa ya mtandaoni ni changamoto inayoendelea. 

UNICEF inaeleza kuwa pia hali ya nje ya Ukraine inatia wasiwasi. Inakadiriwa kuwa watoto wawili kati ya watatu wakimbizi kutoka Ukraine kwa sasa hawajaandikishwa katika mfumo wa elimu wa nchi inayowapokea. Kuna mambo kadhaa nyuma ya hili, ikiwa ni pamoja na uwezo wa elimu ambao tayari umelemewa  na ukweli kwamba, mwanzoni mwa shida na wakati wote wa majira ya joto, familia nyingi za wakimbizi zilichagua kujifunza mtandaoni, badala ya kuhudhuria shule za maeneo hayo, kwa kuwa walitarajia kuwa wanaweza kurudi nyumbani haraka. 

"UNICEF itaendelea kufanya kazi na Serikali ya Ukraine na Serikali za nchi zinazowakaribisha ili kutoa suluhu za kuwasaidia watoto katika maeneo yenye migogoro na wale ambao wamefurushwa kutoka makwao kuendelea na masomo." Amesema Khan. 

Ndani ya Ukraine, UNICEF inataka kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya elimu na maeneo mengine ya kiraia, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya nishati ambayo watoto na familia hutegemea. Pia tunatoa wito wa kuongezeka kwa usaidizi katika kuhakikisha watoto wanapata nyenzo na vifaa vya kujifunzia nje ya mtandao ili kuhakikisha wanaendelea kujifunza na wanaweza kubaki wameunganishwa na wenzao na walimu; pamoja na msaada kwa ajili ya mpango wa kurejesha Ukraine, na juhudi za kujenga upya na kukarabati shule na shule za chekechea. 

Katika nchi zinazohifadhi wakimbizi, UNICEF inataka kutangulizwa kipaumbele kwa ujumuishaji wa watoto wakimbizi wa Ukraine katika mifumo ya elimu ya kitaifa katika ngazi zote za elimu, hasa elimu ya awali kwa watoto na elimu ya msingi - kukiwa na walimu waliohitimu, vifaa vya kujifunzia na nafasi zinazopatikana ili kusaidia ujifunzaji wao wa ana kwa ana, maendeleo, na ustawi.  

Ni muhimu mamlaka husika kutambua na kushinda vikwazo vya udhibiti na utawala vinavyozuia watoto kupata elimu rasmi katika ngazi zote na kutoa taarifa wazi na zinazoweza kufikiwa kwa familia za wakimbizi. Ambapo ufikiaji wa mfumo wa elimu hauwezi kuhakikishwa mara moja, UNICEF inataka utoaji wa njia nyingi za kujifunza hasa kwa watoto wa umri wa shule ya sekondari.