Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Sote tuwe mabingwa ambao bahari inawahitaji' – Katibu Mkuu wa UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa kilele wa mashindano ya baharini uliofanyika mjini Capo Verde.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa kilele wa mashindano ya baharini uliofanyika mjini Capo Verde.

'Sote tuwe mabingwa ambao bahari inawahitaji' – Katibu Mkuu wa UN

Tabianchi na mazingira

Katika siku ya mwisho ya ziara yake nchini Cape Verde, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amehutubia Mkutano wa Mashindano ya Baharini katika mji wa Mindelo huko kisiwa cha São Vicente, nchini Cape Verde, akisema "kukomesha dharura ya bahari ni mbio ambazo lazima tushinde."

Mkutano huo ambao unahitimishwa na mashindano ya mashua baharini ni sehemu ya mfululizo wa matukio ya hali ya juu ili kuongeza uelewa na kuendeleza usaidizi kuelekea Haki za Bahari.

"Na kwa kufanya kazi kama wamoja, ni mbio ambazo tunaweza kushinda. Hebu sote tuwe mabingwa ambao bahari inawahitaji. Tukomeshe dharura ya baharini na tuhifadhi zawadi hii ya thamani ya bluu kwa watoto na wajukuu wetu.” Akahimiza mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu amezungumza akiwa katika Kituo cha Sayansi cha Ocean Mindelo, huko São Vicente, kituo cha kisasa ambacho kinahifadhi vifaa vikubwa vya kisayansi vya baharini kama vile roboti za bahari kuu, karakana ya vifaa vya elektroniki, na maabara za kisasa.

Siku ya leo Jumatatu asubuhi, jengo lilipofungua milango kwa washiriki wa Mkutano huo, limekuwa kama uthibitisho dhahiri wa dau  linalotolewa na Cabo Verde katika kukuza uchumi wa bluu wa visiwa hivyo.

Mashindano kwa ajili ya bahari

Mbio za Bahari zilianza kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1973, zikichukua mabaharia kote ulimwenguni kila baada ya miaka mitatu au minne.

Kwa miongo minne iliyopita, kama mwanaharakati Danni Washington alivyobainisha leo kwenye Mkutano huo, mabaharia wangeona visiwa hivi kwa mbali, au kukimbia katikati yake. Wakati mwingine hata waliokolewa na raia wa Cape Verde, lakini mbio hazijawahi kusimama kwenye visiwa.

Siku ya Ijumaa usiku, nchi hiyo ilikuwa taifa la kwanza kabisa la Afrika Magharibi katika historia ya mashindano hayo kuandaa kituo cha mapumziko wakati wa mashindano.

Rasilimali muhimu iliyoko hatarini

Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mkutano huo pia ulikuwa njia ya kutoa tahadhari: “Bahari ni uhai. Bahari ni riziki. Na bahari iko katika shida."

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa baadhi ya asilimia 35 ya akiba ya samaki duniani wamevunwa kupita kiasi, joto duniani linasukuma joto la bahari kufikia kilele kipya, kikichochea dhoruba za mara kwa mara na kali, kupanda kwa kina cha bahari, na kujaa kwa chumvi katika ardhi ya pwani na vyanzo vya maji.

"Wakati huo huo, kemikali zenye sumu na mamilioni ya tani za taka za plastiki zinafurika katika mifumo ya ikolojia ya pwani - kuua au kuumiza samaki, kasa wa baharini, ndege wa baharini na mamalia wa baharini, wakiingia kwenye mnyororo wa chakula na hatimaye kuteketezwa na sisi." Bwana Guterres ameeleza.

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, ifikapo mwaka 2050, kunaweza kuwa na plastiki nyingi zaidi baharini kuliko samaki.

Hatua kubwa

Kutokana na hali hii, Katibu Mkuu anaamini dunia ilichukua hatua muhimu kurekebisha mwenendo mwaka jana.

Mafanikio haya yalijumuisha "makubaliano ya kihistoria" huko Nairobi kujadili mkataba wa kimataifa wa kudhibiti uchafuzi wa plastiki, Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Bahari huko Lisbon, ambapo nchi zilitoa mamia ya ahadi na ahadi mpya za hiari, na Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Bainuai huko Montreal, Canada uliomalizika kwa nchi kukubaliana juu ya lengo la kulinda asilimia 30 ya ardhi, maji, pwani na mifumo ikolojia ya bahari ifikapo 2030.

“Wengine wameuita mwaka wa 2022 ‘mwaka bora zaidi wa bahari.’ Lakini mbio hizo bado hazijaisha. Tunahitaji kuufanya mwaka 2023 kuwa mwaka wa "hatua bora," ili tuweze kumaliza dharura ya bahari mara moja na kwa wote." amebainisha Bwana Guterres.

Kwa mkuu wa Umoja wa Mataifa, dunia inahitaji hatua za haraka kwa njia nne za kimsingi: viwanda endelevu vya bahari; kutoa msaada mkubwa kwa nchi zinazoendelea; kushinda mbio dhidi ya mabadiliko ya tabianchi; na, mwisho, kupeleka sayansi, teknolojia na uvumbuzi kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea.

Akigeukia sekta ya fedha, Bwana Guterres amesema kwamba “nchi zinazoendelea ni waathirika wa mfumo wa kifedha wa kimataifa uliofilisika kimaadili, uliobuniwa na nchi tajiri kuzinufaisha nchi tajiri.”

Akifunga tukio hilo, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameshiriki katika hafla ya Relay4Nature, akipokea kijiti kilichoanza kuzunguka dunia karibu mwezi Mei wa 2021 ili kutoa wito kwa viongozi wa dunia kuongeza kwa kiasi kikubwa matarajio yao ya kulinda bahari.