Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa ahadi wa kusaidia bonde la ziwa Chad waanza Niger: OCHA

Kanda ya Ziwa Chad ni mojawapo ya mazingira ambapo yamekabiliwa na machafuko na migogoro ya muda mrefu duniani.
© UNOCHA/Naomi Frerotte
Kanda ya Ziwa Chad ni mojawapo ya mazingira ambapo yamekabiliwa na machafuko na migogoro ya muda mrefu duniani.

Mkutano wa ahadi wa kusaidia bonde la ziwa Chad waanza Niger: OCHA

Amani na Usalama

Serikali za Niger, Ujerumani na Norway, pamoja na Umoja wa Mataifa zinashiriki kwa pamoja mkutano wa 3 wa ngazi ya juu kuhusu Kanda ya bonde la ziwa Chad, ambao umeanza leo tarehe 23-24 Januari  katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mahatma Gandhi huko Niamey, Niger. 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA tangu mkutano wa mwisho uliofanyika Berlin Ujerumani mwaka 2018, mgogoro katika bonde la ziwa Chad umezidi kuwa mbaya, na kuongezeka kwa vurugu, upungufu wa maendeleo, mahitaji ya kibinadamu, na vikwazo vya upatikanaji wa huduma za msingi za kijamii, mifumo ya uzalishaji na usaidizi wa kibinadamu na matokeo yake watu milioni 5.3 wamesalia bila makazi katika eneo hilo. 

Shirika hilo limeongeza kuwa matokeo ya pamoja ya kuongezeka kwa ukosefu wa utulivu, athari za muda mrefu za janga la COVID-19, athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga ya kiuchumi yamezidisha hali mbaya ya kibinadamu. 

Familia zikipokea mgao wa chakula kwenye mkoa wa kaskazini mwa Cameroon katika eneo la Ziwa Chad.
© WFP/Glory Ndaka
Familia zikipokea mgao wa chakula kwenye mkoa wa kaskazini mwa Cameroon katika eneo la Ziwa Chad.

Ahaadi ya msaada wa kibinadamu 

Katika mkutano huo wa ahadi nchi za pembezoni zimesisitiza dhamira yao isiyoyumba katika kushughulikia changamoto hizi tata ikiwa ni pamoja na kupambana na ugaidi na itikadi kali za kivita. 

OCHA inasema maendeleo yaliyopatikana yanadhihirisha kuwa changamoto kubwa ya watu kulazimika kufurushwa unaweza kukomeshwa. 

Mahitaji ya fedha kwa ajili ya kukabiliana na dharura katika bonde la ziwa Chad yameongezeka kwa dola za Marekani milioni 259 tangu mwaka 2018.  

Mahitaji ya ufadhili wa uimarishaji yanakadiriwa kuwa dola za bilioni 1.8. 

Naibu msaidizi wa Katibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu, Joyce Msuya, yuko Niger kuanzia kuanzia leo Januari 23 hadi 27 kushiriki katika mkutano huo wa tatu wa ngazi ya juu wa bonde la ziwa Chad. 

Picha ya maktaba ikiwaonesha akari wa Cameroon wakifanya doria katika maeneo ya Ziwa Chad ambayo yameathiriwa na shughuli za kigaidi. (Februari 2019)
UN Photo/Eskinder Debebe
Picha ya maktaba ikiwaonesha akari wa Cameroon wakifanya doria katika maeneo ya Ziwa Chad ambayo yameathiriwa na shughuli za kigaidi. (Februari 2019)

Kuhusu bonde la ziwa Chad 

Eneo la ziwa Chad ni mojawapo ya maeneo yenye mazingira ya migogoro na migogoro ya muda mrefu zaidi duniani.  

Licha ya baadhi ya matukio chanya, viwango vya juu vya vurugu vinaendelea kuwa na athari mbaya kwa mamilioni ya watu nchini Cameroon, Chad, Niger na Nigeria.  

Baada ya takriban miaka 13 ya vita, makundi yenye silaha yanaendelea kueneza ghasia na watu milioni 11 wanahitaji msaada wa aina mbalimbali.

Takriban watu milioni 5.6 walikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula wakati wa msimu wa muambo wa mwaka 2022 ikiwa ni idadi kubwa zaidi katika miaka minne.  

OCHA inasema zaidi ya hayo, watu milioni 2.9 ni wakimbizi wa ndani (IDPs), ikiwa ni pamoja na milioni 2 nchini Nigeria pekee. 

Mzunguko wa ngazi ya juu wa mkutano wa ziwa Chad ni jukwaa muhimu la kisiasa la kimataifa linaloweza kuwezesha maelewano ya kikanda, ya kuvuka mpaka kuhusu marekebisho yanayohitajika kwa ajili ya kukabiliana kwa ufanisi na changamoto za pande nyingi zilizopo katika kanda hiyo

Watoto huko Maroua, Domayo, kaskazini mwa Cameroon, eneo lililoathiriwa na mzozo katika eneo la Ziwa Chad pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.
UNOCHA
Watoto huko Maroua, Domayo, kaskazini mwa Cameroon, eneo lililoathiriwa na mzozo katika eneo la Ziwa Chad pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.

Malengo ya mkutano huo 

Malengo makubwa ya mkutano huu wa 3 wa bonde la ziwa Chad ni pamoja na  

kuimarisha umiliki wa Afrika katika hatua zilizoratibiwa za kikanda, za pamoja ndani ya mfumo wa LCBC/AU RSS na utekelezaji wake kulingana na kanuni, na usaidizi wa kibinadamu ulioratibiwa na Umoja wa Mataifa; 

Kuimarisha masuala  ya kibinadamu, maendeleo, amani ndani ya mfumo mmoja wa Umoja wa Mataifa, katika hatua hii kwa msisitizo maalum wa ushirikiano zaidi kati ya wahusika wa kibinadamu, uimarishaji na maendeleo, ikiwa ni pamoja na kukuza mazungumzo kati ya watendaji wa kibinadamu, uthabiti na maendeleo ili kutambua vyema fursa za pamoja za kukuza uhusiano na kutambua maeneo yanayokabiliwa na utekelezaji wa suluhu endelevu, faida za kulinganisha na kulingana na maeneo ya utaalamu wa kila nguzo. 

Pia kubadilishana mbinu na mifano mizuri kama vile kituo cha kuleta utulivu wa kikanda, changamoto na fursa za kukuza uimarishaji wa hali katika muktadha wa bonde la ziwa Chad. 

Kuimarisha uratibu kati ya wahusika wa misaada ya kibinadamu na uimarishaji kwa ajili ya maendeleo zaidi ya ufumbuzi wa kudumu, hasa kwa nia ya kufikia mapato ya kudumu, ya hiari, salama na yenye heshima kwa wakimbizi wa ndani  IDPs, kwa mujibu wa sheria za kimataifa hasa mkataba wa Kampala na ajenda ya utekelezaji ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi wa ndani. 

Mengine ni pamoja na   

• Kuboresha ufikiaji wa usaidizi wa kibinadamu kwa watu wote wanaohitaji na kukuza heshima kwa sheria ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu 

• Kutia nguvu na kurahisisha juhudi za ujumuishaji na upatanisho kote katika kanda. 

• Kuandaa njia za kushughulikia suala la vikundi vya kujilinda vya jamii 

• Na kushughulikia athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi kama sehemu ya juhudi za kujenga amani na za kibinadamu.