Dola bilioni 2.54 zahitajika 2023 kukabiliana na dharura za kiafya duniani: WHO

Watu wengi wakisubiri kuwaona madaktari katika kliniki ya afya ya mpito iliyoanzishwa kwa ajili ya watu walioathirika na mafuriko makubwa katika mkoa wa Sindh, Pakistan.
© UNICEF/Shehzad Noorani
Watu wengi wakisubiri kuwaona madaktari katika kliniki ya afya ya mpito iliyoanzishwa kwa ajili ya watu walioathirika na mafuriko makubwa katika mkoa wa Sindh, Pakistan.

Dola bilioni 2.54 zahitajika 2023 kukabiliana na dharura za kiafya duniani: WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO leo limezindua ombi maalum la kifedha ili kukabiliana na dharura mbalimbali za kiafya duniani zinazowakabili mamilioni ya watu. 

Ombi hilo la WHO lililozinduliwa mjini Geneva Uswis ni kwa ajili ya mwaka  2023 na ni la dola bilioni 2.54 fedha ambao zitasaidia kutoa msaada kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji likisema kwamba idadi ya watu wenye uhitaji wa misaada ya kibinadamu imeongezeka kwa karibu robo ukilinganisha na mwaka 2022 na sasa idadi imefikia watu milioni 339. 

Hivi sasa, “WHO inakabiliana na idadi isiyokuwa ya kawaida ya dharura za kiafya zinazofungamana mfano majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi kama vile mafuriko nchini Pakistani na ukosefu wa uhakika wa chakula katika Ukanda wa Sahel na katika Pembe ya Afrika, vita nchini Ukraine na athari za kiafya za vita huko Yemen, Afghanistan, Syria na Ethiopia kaskazini.” 

Dharura hizi zote zinaingiliana na usumbufu wa mfumo wa afya unaosababishwa na janga la COVID-19 na milipuko ya surua, kipindupindu na wauaji wengine. 

Kampeni ya chanjo dhidi ya polio nchini Guinea-Bissau.
WHO Guinea-Bissau.
Kampeni ya chanjo dhidi ya polio nchini Guinea-Bissau.

Changamato ambazo hazijawahi kushuhudiwa 

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus "Muunganiko huu ambao haujawahi kushuhudiwa wa migogoro unahitaji jawabu ambalo halijawahi kushuhudiwa. Watu wengi kuliko wakati mwingine wowote wanakabiliwa na hatari ya magonjwa na njaa na wanahitaji msaada sasa. Ulimwengu hauwezi kufumba macho na kutumaini kuwa majanga haya yatajitatua yenyewe. Ninawasihi wafadhili kuwa wakarimu na kuisaidia WHO kuokoa maisha, kuzuia kuenea kwa magonjwa ndani na nje ya mipaka, na kusaidia jamii zinapojijenga upya." 

Ameongeza kuwa WHO kwa sasa inakabiliana na majanga 54 ya kiafya duniani kote, 11 kati ya hayo yameorodheshwa kama ya daraja la 3, kiwango cha juu zaidi cha dharura cha WHO, kinachohitaji hatua katika ngazi zote tatu za shirika, kama ilivyo mara nyingi, walio hatarini zaidi ndio walioathirika zaidi. 

Mwaka 2022, WHO ilitoa dawa, vifaa vingine, mafunzo kwa madaktari na wafanyikazi wengine wa afya, chanjo, ufuatiliaji wa magonjwa ulioimarishwa, kliniki zinazohama, msaada wa afya ya akili, mashauriano ya afya ya uzazi na mengi zaidi.  

WHO inatoa huduma ya gharama nafuu, yenye athari ya juu ambayo hulinda afya, maisha na riziki.  

Shirika hilo limesisitiza kwamba kila dola 1 ya Marekani iliyowekezwa katika WHO inazalisha angalau dola $35 kama malipo ya uwekezaji. 

WHO huchukua hatua za dharura za afya kwa ushirikiano wa karibu na nchi wanachama, mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya kiraia na washirika wengine katika jamii na katika nchi na kanda. 

Ombi hilo limezinduliwa katika hafla maalum kwenye makao makuu ya WHO huko Geneva, na mkurugenzi mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.