Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kupitia miradi ya kilimo ya UN Cabo Verde Guterres apata matumaini dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu wa UN akiangalia bidhaa zinazozalishwa kupitia miradi ya umoja wa Mataifa ya kujenga mnepo wa kilimo kwenye bonde la Paúl Valley, Cabo Verde
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN akiangalia bidhaa zinazozalishwa kupitia miradi ya umoja wa Mataifa ya kujenga mnepo wa kilimo kwenye bonde la Paúl Valley, Cabo Verde

Kupitia miradi ya kilimo ya UN Cabo Verde Guterres apata matumaini dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitumia siku ya leo Jumapili katika Kisiwa cha Cabo Verdean cha Santo Antão, ambapo, baada ya miaka mitano ya ukame mkali, miradi mbalimbali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inalengo la kusaidia kubadilisha sekta ya kilimo ya visiwa hivyo vya Atlantiki.

Kwa saa kadhaa, gari la Antonio Guterres lilikuwa linatembea kwenye barabara mbovu, ambayo ilifunguliwa katika eneo kame, lakini kona ya mwisho, futi mia chache juu ya mlima, mwonekano wa nje ya dirisha lake unashamiri kwa vivuli vingi vya kijani kibichi huku matuta madogo yaliyoegemezwa na kuta za mawe yaliyojaa migomba, mitende na miwa, yakionekana, na vijito vya maji ya rangi ya fedha vikipepea kwa mbali.

Bonde nyororo la Paúl linapatikana katika kisiwa cha milimani cha Santo Antão, kisiwa cha magharibi kabisa cha Cabo Verde, na linawakilisha chemchemi katika kisiwa ambapo ni asilimia 10 pekee ya ardhi ndiyo inayolimwa.

Kati ya eneo hilo ambalo tayari ni dogo, karibu asilimia 18 lilipotea kati ya miaka ya 2000 na 2020.

Sa moja ya visiwa vizuri na vya milima nto Antão, Cape Verde ni nyumbani kwa miradi ya UN ya kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
UN News/Mark Garten
Sa moja ya visiwa vizuri na vya milima nto Antão, Cape Verde ni nyumbani kwa miradi ya UN ya kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Bwana Guterres alipotembelea moja ya matuta, katika siku ya pili ya ziara yake nchini humo, alikaribishwa na kikundi cha wakulima.

Pamoja nao, mtaalam kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo (FAO), Katya Neves, ameeleza kuwa walikuwa katikati ya bustani ya majaribio, ambapo wanaume na wanawake wanajaribu aina mpya za mimea na kujifunza kuhusu mbinu endelevu za kilimo.

"Muitos Parabéns, au "kazi nzuri", Katibu Mkuu alipongeza kikundi hicho kwa Kireno, akionyesha meza ya rangi iliyojaa maharagwe ya kahawia, kabichi, nyanya, viazi vikuu, mihogo na bidhaa nyingine.

Fadhila inayokuzwa nchini ni adimu katika nchi ambayo inahitaji kuagiza kutoka nje asilimia 80 ya chakula inachohitaji kulisha wakazi wake.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameelezwa jinsi baadhi ya mimea inayokua katika bustani hiyo ni aina mpya ya mihogo, ambayo wataalam wanatumai itathibitika kustahimili ukame ulioathiri nchini humo kwa miaka mitano iliyopita. Pia amesikia jinsi wakulima wanavyojifunza njia mpya za kumwagilia au kurutubisha ardhi zao.

Mpango huo unawanufaisha takriban wakulima 285 na ni sehemu ya idadi kubwa ya miradi inayoongozwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine wanaotarajia kubadilisha kilimo nchini humo ili kulisha watu wengi zaidi na kuwa endelevu zaidi kwa sayari kwa ujumla.

Mradi wa Umoja wa Mataifa wa mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika kisiwa cha milima cha Santo Antão Cape Verde
UN Photo/Mark Garten
Mradi wa Umoja wa Mataifa wa mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika kisiwa cha milima cha Santo Antão Cape Verde

Udhibiti wa maji huku kukiwa na ukame

‘Gota a gota’ ni mojawapo ya miradi na umekuwa ukifanya umwagiliaji kwa njia ya matone kupatikana kwa mamia ya wakulima.

"Ni ekari 3,000 tu zilizoenea katika visiwa 10 vinavyomwagiliwa, lakini tafiti zinaonyesha kuwa idadi hii inaweza kuongezeka hadi 5,000," ameelezea Bi. Neves, mwakilishi msaidizi katika FAO.

Angela Silva, ambaye anaishi karibu, pia alikutana na Katibu Mkuu. Yeye ni mmoja wa wanufaika wanaotarajia kuanza kuweka mfumo wa matone hivi karibuni.

“Nilizaliwa katika familia ya wakulima, wazazi wangu, mababu na mababu, wa mababu. Lakini hadi nilipotengana na mume wangu ndiye aliyekuwa akisimamia ardhi.”

Miaka miwili iliyopita, mwalimu huyo wa wakati wote aliamua kuanza kulima mashamba aliyorithi.

"Bado ninajifunza, lakini ninataka kujifunza zaidi na kuweza kubadilisha hii kuwa njia ya kupata pesa. Ndoto yangu ni kuugeuza kuwa msitu wa chakula, ambacho kinaweza kufurahiwa na watoto wangu na wajukuu."amesema.

Ardhi yake ilichukuliwa zaidi na uzalishaji wa miwa, zao ambalo halina faida kubwa au endelevu, kwa hivyo ameanza kubadilisha na kupanda migomba, mipapai na mboga zingine. Hili lilikuwa mojawapo ya somo alilojifunza katika kozi ya mafunzo iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Mradi wa UN wa kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Santo Antão, Cabo Verde
UN Photo/Mark Garten
Mradi wa UN wa kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Santo Antão, Cabo Verde

Kwa mfumo mpya wa umwagiliaji, ana matumaini ya kuepuka baadhi ya matokeo mabaya zaidi ya ukame na kutumia maji vizuri zaidi katika mwaka wa wastani. Tafiti zinaonyesha kuwa, hata mvua inaponyesha huko Cabo Verde, takriban asilimia 20 ya maji hupotea kupitia mkondo wa maji, asilimia 13 hupenya, huku asilimia 67 huyeyuka.

Hii ni moja ya changamoto kwa Dairson da Cruz Duarte, mkulima mdogo wa ndani aliyeleta kahawa ambayo ilimshangaza Katibu Mkuu -hakujua kisiwa  hicho kilikuwa kinaizalisha.

Akielekeza kidole kuelekea chini ya bonde, karibu na kijito kilichojaa viazi vikuu, mkulima huyo ameeleza kwamba maharagwe hayo yanakuzwa hadi huko Santa Isabel, eneo lililo juu ya mlima mrefu zaidi ambao jicho linaweza kuona, ukingo chakavu ambapo kijani cha ardhi hukutana na bluu ya anga.

Unaweza kufikia mji huu wa watu 100 tu kwa miguu, na kilimo chote kinategemea mvua.

Hiyo imefanya miaka mitano iliyopita ya ukame kuwa migumu sana kwa idadi ya watu hao.

Mvua ilipokoma, vijana ndio walikuwa wa kwanza kuondoka.

"Sijui endapo vijana 10 ndio wanaoishi huko kwa sasa," amesema Bwana Cruz Duarte na kuongeza kuwa "Wengine wote waliondoka kwenda sehemu zingine, kwa sababu ya ukosefu wa kazi, mvua, na ukame. Wakati mwingine, hata kama una mifugo, huna malisho ya kutosha kuwalisha. Hakuna riziki nyingine, hivyo waliondoka kwenda kutafuta maisha bora.”

Moja ya miradi ya Un wa umwagiliaji wa matone katika eneo lililokumbwa na ukame la Casa do Meio, manispaa ya Porto Novo, huko Santo Antão.
UN Photo/Mark Garten
Moja ya miradi ya Un wa umwagiliaji wa matone katika eneo lililokumbwa na ukame la Casa do Meio, manispaa ya Porto Novo, huko Santo Antão.

Mwiba wa kutokuwa na uhakika wa chakula

Baada ya miaka mingi ya ukame usioisha, hakukuwa na uzalishaji kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021-2022.

Kufikia wakati huo, mabadiliko ya tabianchi, janga la COVID-19 na kuzuka kwa vita vya Ukraine vyote vilikuwa vimeunganishwa na kuzusha dhoruba kubwa kwa nchi zinazoendelea za visiwa vidogo (SIDS), na Serikali ya Cabo Verde ililazimika kufanya uamuzi mgumu.

Mwezi Juni mwaka jana, mamlaka kuu ilitangaza dharura ya kijamii na kiuchumi ya kitaifa.

Hadi hivi majuzi, visiwa hivyo, ambavyo viko katika bahari ya Atlantiki karibu na pwani ya Afrika Magharibi, vingeweza kuchukuliwa kuwa bingwa katika juhudi za kupunguza umaskini miongoni mwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Makadirio ya Benki ya Dunia yanaonyesha kuwa viwango vya umaskini vilipungua kwa asilimia sita kati ya mwaka 2015 na 2019, kutoka asilimia 41 hadi 35.

Lakini kufikia Juni mwaka jana, idadi ya watu walioathiriwa na uhaba wa chakula iliongezeka, kulingana na takwimu kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP).

Zaidi ya wanawake, wanaume na watoto 46,000, ikiwa ni karibu asilimia 10 ya wakazi wote wa Cape Verde walikuwa wanakabiliwa na kuzorota kwa uhakika wa chakula kati ya  mwezi Juni na Agosti.

Hii ilileta tishio kwa mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana kwa bidii katika miaka ya hivi karibuni.

Cape Verde imejitolea kukomesha umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2026, na Jumamosi, Waziri Mkuu wa nchi hiyo alimhakikishia Katibu Mkuu kwamba nchi inashikilia lengo hilo, lakini, alikiri, miaka michache iliyopita imefanya iwe vingumu zaidi.

Mwakilishi msaidizi wa FAO Cape Verde Katya Neves anasaidia katika maendeleo endelevu Santo Antão, Cape Verde.
UN Photo/Mark Garten
Mwakilishi msaidizi wa FAO Cape Verde Katya Neves anasaidia katika maendeleo endelevu Santo Antão, Cape Verde.

Katya Neves, mtaalam kutoka FAO, ameiambia UN News kwamba mgogoro wa mwaka jana umetoa hisia mpya ya uharaka kwa juhudi za Umoja wa Mataifa na mashirika yake. "Tunaweza kufikia malengo haya, na tunaweza kufanya hivyo kwa kuboresha njia za kilimo."

Tukirejea kwenye bonde, Bwana. Cruz Duarte pia hakati tamaa. Hata baada ya kuona wengi wa marafiki zake wakiondoka katika mji wake mdogo, alifanya kinyume baada ya miaka katika kisiwa jirani, São Vicente, mkulima huyo alirudi kufanya kazi katika ardhi ya mababu zake. "Kilimo ni wito wangu," anasema.

Ana watoto wawili, ambao walilazimika kukaa kwenye kisiwa kingine, kwa sababu eneo la mbali lilifunga shule yake miaka michache iliyopita, lakini ameweza kuwahudumia tangu wakati huo.

Anajivunia kuorodhesha mazao yote anayolima viazi vitamu, maharagwe, maboga na kahawa ambayo inauzwa katika visiwa vingine kwa bei ya juu na jinsi inavyobadilika kulingana na misimu.

"Sasa najua jinsi ya kuifanya kazi ya kilimo, naweza kuendelea,” anasema.

Hiyo si kazi rahisi katika visiwa hivi. Lakini hata baada ya mazao kufanikiwa, bado kuna njia ndefu mbele.

Kutoka shamba hadi kenye mgahawa wa shule

Kwa Amilcar Vera Cruz, "ugumu mkubwa zaidi ni kuiuza," anasema kuhusu mazao ambayo hukua.

Sara Estrela, msaidizi wa malengo ya maendeleo endelevu katika mradi wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), anaeleza kuwa, kihistoria, wakulima kwa kawaida hawapangiwi katika vyama au vyama vya ushirika huko Cabo Verde.

Sara Estrela msaidizi wa mpango wa maendeleo endelevu wa shirika la UNDP anashughulika na mradi wa kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Santo Antão
UN Photo/Mark Garten
Sara Estrela msaidizi wa mpango wa maendeleo endelevu wa shirika la UNDP anashughulika na mradi wa kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Santo Antão

"Kwa kanuni kuwa kilimo cha kujikimu au biashara ndogo za familia, inakuwa vigumu kuuza kwa bei nzuri wakati unapofika," amesema.

Moja ya miradi ambayo mfumo wa Umoja wa Mataifa umeunga mkono ni uundaji wa chama cha wazalishaji katika bonde hili.

Mashirika hayo pia yamesaidia ujenzi wa maghala mawili ya biashara ambapo mazao yanaweza kukusanywa, kuoshwa na kutayarishwa kwa ajili ya kuuzwa.

Kwa Bi. Estrela, "lengo kubwa zaidi ni kulenga sekta nzima na kujaribu kupanga mlolongo mzima, tangu kupanda mbegu ardhini hadi kuweka chakula kwenye sahani."

Ameongeza kuwa "Tunawawezesha wazalishaji kwa ujuzi na vifaa."

 

Bwana Vera Cruz amepokea usaidizi huu na, baada ya miongo kadhaa ya kuhangaika na uuzaji wa mazao yake, anatumai “chama ni njia ya kufungua upeo mpya katika masuala ya masoko. Tuna matatizo mengine, lakini hiyo ndiyo imechelewesha maendeleo ya kilimo, uuzaji wa bidhaa, na mabadiliko ya bei. Wakati mwingine haitoshi kufidia gharama za uzalishaji.”

Mkulima amefikiria siku hii kwa muda mrefu. Ana ndoto kubwa, ambazo zinaona mazao yake yakisafiri vizuri zaidi katika jiji kubwa la kisiwa hicho, Porto Novo, hadi nchi za mbali, wakati neno kuhusu ubora wa bidhaa hizi linapotoka. Mchanganyiko wa miradi iliyofadhiliwa na serikali na Umoja wa Mataifa, anasema, inaweza kusaidia kugeuza ndoto hizi kuwa kweli.

Kwa miaka mingi baada ya uhuru wa nchi hiyo, mwaka 1975, WFP iliwajibika kwa chakula cha wanafunzi wote huko Cabo Verde.

Lakini nchi hiyo ilihitimu kutoka katika orodha ya nchi zenye maendeleo duni ya Umoja wa Mataifa hadi nchi yenye kipato cha kati mwaka 2007 na, miaka michache baadaye, serikali ilichukua jukumu hilo.

Mojawapo ya maamuzi iliyofanya ni kwamba asilimia 25% ya vyakula vyote shuleni vinavyotumika vinunuliwe ndani ya nchi.

Kwa uamuzi huo ukaja mtihani mkubwa wa kwanza kwa chama cha watayarishaji wa Vale do Paúl kilichoundwa hivi karibuni.

Kwa mwaka mzima wa shule wa 2021-2022, wazalishaji hawa waliuza ndizi zote zilizotumiwa katika shule za visiwa vya Santo Antão, São Vicente na Santa Luzia. Mpango huo ulifikia wanafunzi 20,000.

Sasa, chama kinajiandaa na, baadaye mwezi huu, kitafanya kusanyiko lake la kwanza.

Wanaume wawili wakifanyakazi kwenye mradi wa UN wa kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Santo Antão
UN Photo/Mark Garten
Wanaume wawili wakifanyakazi kwenye mradi wa UN wa kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Santo Antão

Baadaye mwezi wa Machi, mtihani wa mwisho utafika. Vyakula vinavyolimwa na wakulima hao, sawa na alivyojaribu Katibu Mkuu leo, vitaoshwa na kufungwa kwenye maghala mapya, na kupakiwa kwenye boti, na hatimaye kuwafikia watoto katika visiwa vyote.

Katika wiki chache tu, chemchemi ya Paúl itasaidia kulisha karibu wanafunzi 90,000, takriban asilimia 20 ya idadi ya watu wote nchini humo.