Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres awasili Cape Verde kwa mkutano wa bahari na vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (Katikati) akipokelewa na waziri wa mambo ya nje wa Cabo Verde Rui Alberto Figueiredo Soares São Vicente
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (Katikati) akipokelewa na waziri wa mambo ya nje wa Cabo Verde Rui Alberto Figueiredo Soares São Vicente

Guterres awasili Cape Verde kwa mkutano wa bahari na vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Je, nchi inawezaje kupata mustakabali endelevu wakati asilimia 99.3 ya eneo lake ni maji? Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amewasili leo Jumamosi huko Cabo Verde ili kuangalia baadhi ya majibu na suluhu bunifu zinayoendelea katika taifa hilo la visiwa 10 vilivyoko katikati ya bahari ya Atlantiki.

Jawabu linarudi nyuma hadi mwaka 2015, wakati serikali ya kitaifa ilipoelezea mpango mkakati wa jinsi uchumi wa bluu ambavyo ungekuwa sehemu kuu ya mustakabali wa taifa hilo la visiwa, na pia kwa safu ya uwekezaji ambayo imefanywa tangu wakati huo.

Lakini jioni ya leo, akitazama boti 11 zinazoshiriki mbio za baharini zilizotia nanga katika bandari ya Mindelo, huku milingoti yao yenye urefu wa ghorofa 10 ikipasua angani juu ya kisiwa cha São Vicente, Bwana Guterres ameshuhudia mojawapo ya malipo yanayoonekana zaidi ya dau hili.

Awali, Katibu Mkuu aliuita uchumi wa bluu kama ni "fursa ya msingi ya kukuza maendeleo endelevu katika visiwa hivyo" na kusema Umoja wa Mataifa unatarajia kufanya kazi na serikali yake na watu wake ili "kutafsiri azma hii kuwa ukweli."

Waziri Mkuu wa Cape Verde, José Ulisses Correia e Silva, amesema kuwa nchi yake inataka "kujulikana zaidi na kuwa na umuhimu zaidi" katika nyanja ya kimataifa, na bahari ni sekta ambayo wanataka sauti yao isikike.

Ameongeza kuwa "Inaleta maana kujiweka katika eneo hili maalum na kulifanya kuwa muhimu na inaleta maana kwamba ujumbe huu unatoka hapa.”

Katika miaka mitano iliyopita, kama sehemu ya juhudi hizi, nchi hiyo imekuwa na 'Wiki ya bahari' kila mwaka na, Jumatatu ijayo, Cabo Verde inashirikiana na mbio za bahari kufanya mkutano wa kilele ambao utajumuisha wazungumzaji kutoka pande zote duniani akiwemo Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu wa UN akiwa Cabo Verde kushiriki juhudi za kupiga jeki uchumi wa bluu kwenye mashindano ya mbio za boti katika bandari ya Mindelo, kisiwani São Vicente.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN akiwa Cabo Verde kushiriki juhudi za kupiga jeki uchumi wa bluu kwenye mashindano ya mbio za boti katika bandari ya Mindelo, kisiwani São Vicente.

Tishio lililopo

Ahadi ya Cabo Verde inaweza kuwa haitoshi ameonya Bwana Guterres kwamba nchi iko "katika mstari wa mbele wa mgogoro uliopo wa mabadiliko ya tabianchi”

Ameendelea kusema kwamba "Kupanda kwa kina cha bahari na upotevu wa bioanuwai na mfumo wa ikolojia kunaleta vitisho kwa visiwa hivyo. Nimechanganyikiwa sana kwamba viongozi wa ulimwengu hawapei dharura hii ya maisha na kifo hatua na uwekezaji unaohitajika."

Baadhi ya matokeo haya tayari yanaweza kuhisiwa katika bandari inayoandaa Mbio, mojawapo ya bora zaidi katika pwani yote ya Afrika Magharibi, sababu iliyowavutia wafanyabiashara na maharamia karne nyingi zilizopita na sasa inakaribisha changamoto kubwa zaidi ya meli duniani kote.

Katika miaka michache iliyopita, amesema wavuvi wa Cabo Verde wamebaini kupungua kwa ukamataji wa mackerel weusi, moja ya samaki maarufu zaidi miongoni mwa wenyeji.

Mwaka 2022, tasnia ya vifungashio iliripoti kupunguzwa kwa kunasa Samaki aina ya jodari na kutokuwepo kwa malighafi ya mackerel Weusi.

Kulingana na matokeo ya awali ya tathmini iliyoongozwa na Umoja wa Mataifa ambayo inapaswa kuwasilishwa na kujadiliwa na wadau wakuu wa kitaifa mapema mwaka huu, ifikapo biomasi 2100, ya samaki wakubwa wa pelagic wale wanaoishi katika ukanda wa pelagic wa bahari au maji ya ziwa, wakiwa karibu na chini wala karibu na ufuo kama vile albacora, aina ya tuna, inatarajiwa kupungua kwa hadi asilimia 45 Katika bonde jirani la Senegali na Mauritania, punguzo litakuwa kubwa zaidi.

Mabadiliko kama haya yanaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa visiwa vya taifa hilo.

Mwaka wa 2018, sekta ya uvuvi ilitoa ajira kwa watu 6,283, na ilikuwa msingi wa lishe ya watu 588,00.

Bidhaa hizi pia zilichangia karibu asilimia 80 ya mauzo ya nje ya nchi.

"Mabadiliko ya tabianchi ni tishio dhahiri kwa mustakabali wa uvuvi, lakini pia bioanuwai zote," amesema Katibu Mkuu baadaye jioni, aliposhiriki katika msururu wa wazungumzaji uliondaliwa na waziri mkuu, katika kituo cha kitaifa cha sanaa ufundi na usanifu cha Cabo Verde.  

“Ukweli ni kwamba, kuna uhusiano wa wazi kabisa kati ya sekta ya uvuvi na ulinzi wa hali ya hewa. Uzoefu umeonyesha kuwa unapolinda eneo fulani, kuna athari ya kuzidisha katika maeneo mengine, na kila mtu anafaidika,” ameongeza Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu wa UN General António Guterres akiwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari na waziri mkuu wa Cabo Verde José Ulisses Correia e Silva
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN General António Guterres akiwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari na waziri mkuu wa Cabo Verde José Ulisses Correia e Silva

Kukabiliana na changamoto

Wanaume hao wawili waliketi wakiiangalia kituo cha kitaifa, ambacho mbele yake kulifunikwa na maumbo ya mviringo ya vifuniko kutoka kwenye mapipa ya mafuta yaliyopakwa rangi za msingi.

Huo ni ujumbe wa dhamira ya nchi hiyo katika kudumisha uendelevu, lakini pia ni ishara ya kuunga mkono idadi yake kuwa ya walio ughaibuni ambao ni  zaidi ya watu milioni moja, mapipa haya mara nyingi hutumiwa na wahamiaji kutuma zawadi kwa familia zao.

"Changamoto za mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuwa na nguvu mara kwa mara, lakini siku zote tumekabiliana na matatizo na kila mara tumepata njia ya kukabiliana nayo," amesema waziri mkuu.

Kulingana na Bwana Correia e Silva, kupotea kwa viumbe kunaweza kuathiri Cabo Verde kwa njia nyingine.

Visiwa hivyo vinachukuliwa kuwa moja ya maeneo 10 ya juu ya viumbe hai vya baharini ulimwenguni na, kwa miongo kadhaa, aina 24 za nyangumi na pomboo waliorekodiwa katika maji haya, karibu asilimia 30 ya viumbe vyote hivyo  zimevutia wageni wengi ambao wameufanya utalii kuwa ngome ya uchumi wa nchi hiyo.

Mwaka 2022 pekee, baada ya miaka michache kutawaliwa na janga la COVID-19, visiwa vilipokea karibu watalii 700,000 na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwa karibu asilimia 25 ya pato la taifa.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akishiriki kwenye mjadala na waziri mkuu wa Cabo Verde  José Ulisses Correia e Silva,
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akishiriki kwenye mjadala na waziri mkuu wa Cabo Verde José Ulisses Correia e Silva,

Haki kwa Cabo Verde

Cabo Verde imeanza kupambana dhidi ya mabadiliko haya. Katibu Mkuu amesema nchi "imeonyesha uongozi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa maneno na vitendo kwa juhudi za kubadilisha deni kuwa miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na katika uchumi wa bluu."

Hadi asilimia 20 ya uzalishaji wa nishati wa Cabo Verde sasa unatoka kwa vyanzo vinavyoweza kurejerewa ikiwa ni mojawapo ya kiwango cha juu zaidi Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na lengo ni kuongeza matumizi ya nishati mbadala kwa hadi asilimia 50 ifikapo 2030.

Waziri mkuu amesema nchi yake inahitaji "kupatanisha mahitaji ya uchumi, mazingira, na jamii kwa sababu inahitaji rasilimali hizi kuzalisha mali kwa nchi."

Bwana. Correia e Silva ametoa mfano wa jinsi ambavyo hii inaweza kufanywa. Katika jumuiya ya São Pedro, kwenye kisiwa cha São Vicente, sehemu ya wakazi wamebadilika katika miaka ya hivi karibuni kutoka kwenye sekta ya uvuvi hadi kutoa huduma ambapo watalii wanaweza kuogelea kwa usalama na kasa.

Ameendelea kuangazia mfululizo wa mipango ya kupambana na uchafuzi wa taka za plastiki na kukuza uchumi wa mzunguko.

Pia alikumbuka jinsi nchi ilivyodhinisha kudai sheria mpya inayosimamia uvuvi na inafanya kazi kupanua eneo lililohifadhiwa kutoka asilimia sita hadi 30.

"Tunataka kwenda mbali zaidi, lakini tunahitaji rasilimali kufanya hivyo," amesema.

Katibu Mkuu akikubalian na hilo amesema "Tunahitaji haki kwa wale ambao kama Cabo Verde hawakufanya hata kidogo kusababisha mgogoro huu, lakini ndio ambao wanalipa gharama kubwa".

Maongezi yalipofikia tamati, sehemu chache, pale bandarini, wafanyakazi wa mbio za bahari walikuwa wakipumzika.

Ndani ya siku chache tu, wanaanza mkondo wa pili wa shindano hilo, ambalo litawatoa kutoka Cabo Verde, kuvuka Ikweta, chini ya pwani ya Amerika Kusini, na kuelekea Cape Town kwenye ncha ya kusini mwa Afrika Kusini.

Saa chache zilizopita, mabaharia walikutana na Bwana Guterres, ambaye aliwaeleza jinsi mtoto wake, miaka michache tu iliyopita, alivyojiunga na marafiki zake watatu kwenye safari ya meli kuvuka bahari ya Atlantiki.

Hadithi hiyo ilimfanya mmoja wa manahodha, Kevin Escoffier, kumuuliza: "Je, unaweza kufanya kitu kama hicho?"

Alicheka na kusema "Labda siku moja ninapostaafu."