Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutimiza ndoto za UN za Kale, kijana anayepambana na saratani

Mpokeaji wa Make-a-Wish akiwa ziarani makao makuu ya Umoja wa Mataifa na familia yake, hapa kwenye Jukwaa la Ukumbi mkuu wa mikutano wa kimataifa.
UN Photo/Mark Garten
Mpokeaji wa Make-a-Wish akiwa ziarani makao makuu ya Umoja wa Mataifa na familia yake, hapa kwenye Jukwaa la Ukumbi mkuu wa mikutano wa kimataifa.

Kutimiza ndoto za UN za Kale, kijana anayepambana na saratani

Masuala ya UM

Tamaa ya maisha ya Kaloenic Ilac, au Kale, mwenye umri wa miaka 16, imekuwa ni kusafiri hadi New York Marekani na kutembelea Umoja wa Mataifa.  

Mwezi huu wa Januari, Wakfu wa Make-a-Wish umefanya ndoto yake kutimia kwa ziara maalum iliyopangwa na kuhusisha balozi na mmoja wa maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa. 

Mwaka mmoja uliopita, Kale, anayeishi California nchini Marekani, alianza kuwa na uoni hafifu katika jicho lake la kulia.  

Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitababu, familia yake ilipokea habari zenye kuhuzunisha kwamba alikuwa na uvimbe kwenye mshipa wa macho wa jicho la kulia. 

"Mwaka huu umekuwa mgumu kwa Kale," amesema babake, William, akieleza kwamba, Pamoja na kupambana na saratani, mwanawe anapitia misukosuko ya kawaida inayowakabili wanafunzi barubaru wa shule ya upili. 

Akiwa ni kijana mkubwa kati ya wavulana wawili wa familia hiyo, Kale, ambaye wazazi wake wote ni walimu wa historia, anapendelea masuala ya kigeni na wa kimataifa, na ndoto za kuwa mwanadiplomasia.  

"Umoja wa Mataifa ni mojawapo ya nguvu kubwa za mahusiano ya kimataifa kwenye sayari dunia," ameiambia UN News.  

Na kuongeza kuwa “Inanivutia sana. Na kwa kuwa makao makuu yako hapa New York, jiji ambalo pia nataka kutembelea, niliona pangekuwa mahali pazuri sana kupata uzoefu”. 

Kaloenic Ilac, "Kale", amekuwa akikabiliana na ugonjwa wa saratani. Ndoto yake ya kufika UN ikatimia wakati Wakfu wa "Make-a-Wish" ulipompa yeye na familia yake matakwa yake, hapa akijivunia kukaa katika Ukumbi wa Baraza la Usalama.
UN News/Florence Westergard
Kaloenic Ilac, "Kale", amekuwa akikabiliana na ugonjwa wa saratani. Ndoto yake ya kufika UN ikatimia wakati Wakfu wa "Make-a-Wish" ulipompa yeye na familia yake matakwa yake, hapa akijivunia kukaa katika Ukumbi wa Baraza la Usalama.

Kuongeza fursa ya kupona 

Wakfu wa Make-A-Wish unaamini kwamba kutimiza matakwa ya mtu kunaweza kubadilisha uwezekano wa watoto wanaopambana na magonjwa, na kuwasaidia kutazama maisha zaidi ya mapungufu yao, kusaidia familia zinazokabiliana na wasiwasi, na kuleta furaha kwa jamii nzima. 

Wakfu huwezesha takriban matakwa 15,000 kutimia nchini Marekani kila mwaka, kwa kuzingatia mwongozo kutoka kwa timu za matabibu.  

"Kwa wastani, inachukua kati ya miezi sita hadi 18 ili matakwa yako yatimizwe", ameelezea Coleen Lee kutoka Wakfu wa Make-A-Wish. 

Na kuongeza kuwa  "Hii ni mara ya kwanza kwa mtoto kueleza nia ya kuja Umoja wa Mataifa!" 

"Umoja wa Mataifa ni muhimu kwangu kuutembelea kwa sababu ya kazi muhimu ambayo inafanywa hapa, kuanzia operesheni za kibinadamu hadi juhudi za kulinda amani zote kwa matumaini ya kuifanya dunia kuwa mahali bora," Kale aliandika katika ombi lake alilotuma kwa Wakfu.  

Akiongeza kuwa "Ndiyo maana nadhani itakuwa muhimu kuona mahali hapo ili niweze kuelewa vyema kazi inayoendelea huko, na jinsi maamuzi haya yanavyofanywa". 

Kale Ilac akiwa na familia yake na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
United Nations/Helena Lorentzen
Kale Ilac akiwa na familia yake na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Kuifanya siku kuwa ya kukumbuka 

Wakati Umoja wa Mataifa ulipopokea ombi hilo kutoka kwa Wakfu, walijaribu kuweka pamoja programu iliyopangwa vizuri ili kuhakikisha ziara yake itakuwa ya kukumbukwa. 

"Ili kufanya yote yawe na manufaa, tuliamua kuandaa sio tu ziara ya kuongozwa bali pia kumpa Kale fursa ya kukutana na wafanyakazi wa ngazi ya juu na wanadiplomasia," ameelezea Rula Hinedi, mkuu wa kitengo cha kuongoza watalii katika Umoja wa Mataifa. 

Siku huanza mapema na ziara ya kuongozwa. "Ilikuwa safi sana, ninashangaa," Kale anasema, akitabasamu. “Nimependa sana Baraza Kuu. Niliweza kusimama kwenye mimbari na ilikuwa fursa ya kipekee kuwa katika sehemu moja na watu wa ngazi ya juu kuambatana nami. Hiyo ilikuwa ishara yenye nguvu sana”. 

Alipokelewa na wafanyakazi wa idara ya ulinzi na usalama, akiwemo Paula Goncalvez, afisa wa ngazi ya juu zaidi wa kike, ambaye ana tajriba ya zaidi ya miaka 25. "Tunataka ufurahie uzoefu hapa", anasema. “Ni shirika zuri sana, na tunafurahi kwamba ulituchagua!” 

Katika chumba cha mashauriano cha Baraza la Usalama, Kale alikutana na afisa Richard Norowski.  

Ziara ya Kale, na beji yake ya Make-a-Wish, ilirejesha kumbukumbu za kihisia kwa afisa Norowski, ambaye aliandamana na dada yake kwenye safari ya Make-a-Wish kwenda Disneyland, alipokuwa na umri wa miaka saba. “Dada yangu alikuwa na saratani ya damu. Sitasahau hilo, na beji hiyo ina maana kubwa kwangu”. 

Kale akipokea ushauri wa kikazi kutoka kwa Maher Nasser, mkuu wa Idara ya Ufikiaji wa Umoja wa Mataifa
United Nations/MHM
Kale akipokea ushauri wa kikazi kutoka kwa Maher Nasser, mkuu wa Idara ya Ufikiaji wa Umoja wa Mataifa

Ushauri wa hali ya juu wa kazi 

Sehemu iliyofuata ya ziara ilihusisha mfululizo wa mikutano ambayo inaweza kumsaidia Kale kufikia lengo hili katika siku zijazo. 

Maher Nasser, mkurugenzi wa kitengo cha uhamasishaji katika idara ya mawasiliano ya kimataifa, alielezea uzoefu wake binafsi wa kupanda vyeo katika Umoja wa Mataifa, na kupendekeza aina za masomo ya kitaaluma ambayo yanaweza kumsaidia Kale kufikia lengo la kufanya kazi kama mwanadiplomasia, au kama mtumishi wa umma wa kimataifa katika Umoja wa Mataifa. 

"Fuata ndoto yako hata iweje", amesema Bw. Nasser, "na nyota zitajipanga ili kutimiza ndoto yako", akiongeza kuwa anatumai kumuona Kale kwenye vibaraza vya Umoja wa Mataifa katika miaka michache ijayo. 

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Nicolas de la Rivière, na Diarra Dime-Labille, mshauri wa kisheria katika ujumbe huo, na mkuu wa kitengo cha Haki za Kibinadamu, masuala ya kibinadamu na ushawishi pia walitoa ushauri kwa Kale, na kuelezea uzoefu wao. 

"Unapaswa kuwa na mawazo yaliyo wazi kwa sababu muda mwingi unapaswa kufanya kazi na kujadiliana na nchi ambazo zina malengo tofauti, na maono tofauti na yetu," ameeleza Bi Dime-Labille na kuongeza kuwa “ Lengo letu kuu ni kuunda dunia yenye amani, lengo ambalo nchi hizo zilikuwa nalo wakati zinaunda Umoja wa Mataifa”. 

Kale ana matumaini kwamba atapona na atashinda ugonjwa wa saratani
UN Photo/Mark Garten
Kale ana matumaini kwamba atapona na atashinda ugonjwa wa saratani

Jitahidi kila uwezavyo kuwa bora zaidi 

Kale na familia yake wamejaa matumaini kwa siku zijazo. "Tuna takriban miezi sita hadi 12 kabla ya kufikia kile walichokiita mpango wa ukarabati", anasema mama yake, Robin. 

"Katika ripoti mbili zilizopita uvimbe ulipungua, na Kale amepata tena uwezo wa kuona kwenye jicho lake la kulia, anasema baba yake. "Tunatumai, mwezi ujao tutapata matokeo chanya zaidi". 

Rula Hinedi anakiri kwamba aliguswa moyo na uzoefu wa kukutana na Kale na familia yake. “Ilinigusa sana. Ilinifedhehesha sana,” anasema. “Nadhani ombi la kijana mwenye umri wa miaka 16 kutembelea Umoja wa Mataifa ni ujumbe mzito kwetu sote kwamba kazi inayoendelea hapa bado inafaa, haswa kwa kizazi kipya. Mambo si rahisi kila mara, lakini dunia hakika ni mahali pazuri zaidi kwa sababu ya Umoja wa Mataifa”. 

Akitafakari juu ya safari hiyo, Kale anasema kwamba kujifunza kuhusu mema ambayo Umoja wa Mataifa hufanya duniani kote, kumemtia moyo kufanya kazi katika kuhudumia wengine. 

“Fanya tu uwezavyo kuwa bora zaidi,” anasema, “kwa sababu unapokuwa bora, unaweza kuwasaidia wengine kuwa bora zaidi, na itakuwa tu mwitikio chanya wa kuigwa. Kuwa na msaada na kuwa mkarimu. Huo ni ujumbe wangu”.