Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IAEA yapanua wigo wa shughuli zake Ukraine

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Gross (kulia) akikutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Kyiv.
Ikulu ya Ukraine
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Gross (kulia) akikutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Kyiv.

IAEA yapanua wigo wa shughuli zake Ukraine

Amani na Usalama

Mkurugenzi Mkuu wa shirka la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA, Rafael Mariano Grossi amemfahamisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Kyiv kuhusu upanuzi wa wigo wa shughuli za shirika hilo nchini humo ili kuisaidia kuhakikisha ulinzi na usalama wa nyuklia katika kinu chake wakati huu ambapo operesheni na mashambulizi ya kijeshi yanaendelea kutoka Urusi.

Ofisi za IAEA Chernobyl na Pivdennoukrainsk

Mathalani mapema siku ya Jumatano, Mkuu huyo wa IAEA alizindua ofisi ya ujumbe wa IAEA wa kusaidia Chernobyl au Chornobyl (ISAMICH) kaskazini mwa Ukraine, eneo ambalo kulikuwa na tukio la kuvuja kwa gesi mwaka 1986.

Akizungumza na wanahabari, siku hiyo, Bwana Grossi amesema uzinduzi huo ni tukio la kihistoria kwa IAEA. “Ni siku muhimu kwa Ukraine na kwa Chernobyl. IAEA inaanza programu ya kina ya usaidizi kuhusu usalama wa mtambo huu.”

Amesema ni muhimu kuona kuwa mwaka mmoja baada ya Chernobyl kutwaliwa, hatimaye sasa umerudi kwenye umiliki halali. “Shughuli muhimu zimerejeshwa, na sasa tunaelekea kwenye hatua muhimu. Kwa hiyo ni siku muhimu. Lakini tuna kazi kubwa mbele yetu.”

Amesema ni matumaini yake kuwa hakutakuweko na kutwaliwa au kushambuliwa tena kwa mtambo huo na kwamba “juhudi zetu zinalenga kuepusha hilo na kwa kuweko kwa IAEA hapa tunachukua hatua ya dhati kwenye mwelekeo huo. Uwepo wa watu wetu hapa ni njia bora ya kujulisha jumuiya ya kimataifa kuhusu kinachoendelea na ichukue hatua zinazohitajika.”

Kabla ya kwenda Chernobyl Bwana Grossi alizindua pia ofisi ya IAEA kwenye mtambo wa nyuklia wa Pivdennoukrainsk na kusema “tunashirikiana na msimamizi, tunafanya kazi na watumishi wote kwa hiyo sasa tunaweka ofisi yetu ya kudumu hapa. Tutajadili hatua zifuatazo. Hii sehemu ya ujumbe wetu tunaanza leo hapa Kusini mwa Ukraine. Tutaendelea huko Rivine wiki ijayo.”

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Gross alipotembelea mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhya nchini Ukraine
© IAEA
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Gross alipotembelea mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhya nchini Ukraine

Grossi na Zelensky wamejadili pia kuhusu mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhya

Viongozi hao wawili pia wameendelea kujadili mapendekezo ya Bwana Grossi ya kuanzisha eneo la ulinzi kwa ajili ya usalama wa nyuklia karibu na mtambo wa nguvu za nyuklia wa Zaporizhzhya (ZNPP).  


Mtambo au kinu hicho kikubwa zaidi cha nishati ya nyuklia barani Ulaya  kimekuwa kikikabiliwa na moto mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni, na kusababisha wasiwasi wa ulinzi na usalama wa nyuklia.


Mkurugenzi huyo wa IAEAamesisitiza kwamba eneo hilo ni muhimu kwa kuzuia ajali mbaya ya nyuklia na akasema atasonga mbele na juhudi zake ili kutendeka haraka iwezekanavyo.